KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) jana kimepokea nyaraka za maombi
ya usajili wa kampuni za kuzalisha mbolea ambazo uwekezaji wake una
thamani ya dola za Marekani bilioni 1.9 ambazo ni sawa na zaidi ya Sh
trilioni 4.
Kampuni hizo ni Ferrostaal kutoka Ujerumani na Haldor Topsoe ya
Denmark ambazo zimekuja kuwekeza katika uzalishaji wa mbolea ya chumvi
katika eneo la Kilwa Masoko mkoani Lindi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Geoffrey Mwambe
wakati wa hafla fupi ya upokeaji wa nyaraka za usajili wa mradi huo.
Alisema mradi huo wa mbolea utatumia rasilimali ya gesi asilia
inayopatikana hapa nchini katika shughuli zake za uzalishaji na utakuwa
ukizalisha tani milioni 1.3 za mbolea kwa mwaka.
“Mbali na kiwango cha tani milioni 1.3 za mbolea zitakazokuwa
zikizalishwa kila mwaka, mradi huo pia utaajiri Watanzania 4,500 na
wageni 300,” alisema Mwambe. Akifafanua zaidi kuhusu mradi huo, Mwambe
alisema kuwa mradi huo utasajiliwa hapa nchini kwa jina la Tanzania
Mbolea Petrochemicals (TAMCO).
“TIC tutasimamia na kuhakikisha kila taasisi inayohusika na utoaji wa
vibali kama vile vinavyohusu mazingira au vibali vya kufanya kazi na
ukaazi kwa ajili ya wataalamu wa kufunga mitambo na mashine vinapatikana
kwa wakati ili kampuni itumie muda mfupi kujenga kiwanda chake na sisi
tuanze kuona mapema matunda ya mradi huu,” alisema Mwambe.
Mwambe alisema ukubwa wa mradi ni ujumbe tosha kwa wawekezaji
mbalimbali duniani kwamba Tanzania ni mahali panapofaa kwa uwekezaji kwa
kuwa kuna mazingira rafiki, serikali inayoaminika na kuwepo kwa mfumo
unaosaidia kupata uwekezaji mwingi.
Alisema uwekezaji huo ni kichocheo kikubwa katika ukuaji wa sekta ya
viwanda lakini pia kwa kipindi kirefu kumekuwa na changamoto katika
sekta ya kilimo kutokana na kiasi kikubwa cha mbolea kuagizwa kutoka
nje, jambo ambalo kiuchumi halina afya.
“Kuzalisha mbolea hapa nchini kwa kutumia rasilimali zetu, ina maana
kuwa mbolea itakuwa inapatikana kwa wakati, itawafikia wakulima kwa
urahisi na bei nafuu na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni zilizokuwa
zikitumika kuagiza mbolea kutoka nje, lakini pia itaunganisha sekta
nyingine za kiuchumi,” alisema Mwambe.
Mwambe alisema mradi huo utasaidia kupunguza tatizo la upatikanaji wa
mbolea nchini kwa kuwa mahitaji halisi ya bidhaa hiyo ni zaidi ya tani
350,000. Huu ni uwekezaji mkubwa katika uzalishaji wa pembejeo za kilimo
hapa nchini na kuwa uzaishaji wake utapunguza mahitaji ya mbolea ambayo
ni tani lakini 3.5.
Kiwanda cha mbolea cha Minjingu huzalisha tani 100,000 kwa mwaka
ikiwa ni wastani wa asilimia 20 ya mahitaji yote. Kwa upande wake
msimamizi wa mradi huo hapa nchini, Wilfread Wineam alisema kuwa kiwanda
hicho kina uwezo wa kuzalisha tani milioni 1.3 kwa mwaka na asilimia 30
ya mbolea itauzwa hapa nchini na itakayobaki itauzwa nje ya nchi.
Naye Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Detlet Waecheter alisema
kutokana na dira ya Tanzania ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka
2025, hivyo uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni nao ni muhimu katika
kufikia malengo hayo.
Alisema kuwa uwekezaji wa kiwanda cha mbolea ni mwanzo kwa wawekezaji
wengine wengi kuja kuwekeza Tanzania na kuahidi kuleta ujumbe mkubwa wa
wawekezaji kutoka Jimbo la Bavaria ili kuja kujionea fursa mbalimbali
za uwekezaji.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mbolea ya Minjingu iliyopo
mkoani Manyara, Pardeep Singh Hans alisema kuwa ni vyema mradi huu
ukatekelezwa kwa haraka ili kukamata soko la bidhaa hiyo mapema.
CHANZO HABARI LEO
hatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment