WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII 872 KUPATIKANA RUANGWA
Na. Elimu ya Afya kwa Umma.
Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa Kushirikiana na Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetoa nafasi 872 kwa wananchi watakaowania nafasi ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi ambao watatambuliwa kupitia Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngzi ya Jamii.
Akizungumza katika Kikao na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ruangwa leo tarehe 9, 2024 katika Ofisi ya Mkurugenzi, Afisa Mpango wa Taifa wa Wahudumu wa AfyabNgazi ya Jamii Bi.Orsolina Tolage kutoka Wizara ya Afya, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma amesema kila kitongoji kutakuwa na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wawili.
"Katika kuhakikisha huduma za Afya zinakuwa karibu zaidi na wananchi Serikali imejipanga ambapo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa tunatarajia kupata Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii 872, wawiliwawili kila kitongoji jinsi ya kiume mmoja na jinsi ya kike mmoja , hivyo wataomba nafasi na watachaguliwa kupitia mikutano ya kijiji au mtaa"amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Frank Chonya ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweka kipaumbele suala la Afya hasa kwa kuweka Mkakati wa kuwa na Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii katika kata 22, vijiji 90 na vitongoji 436 katika Halmashauri hiyo.
"Naishukuru Serikali kwa kuimarisha miradi mbalimbali ya maendeleo katika katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa na hili suala la Mpango Jumuishi wa Wahudumu Ngazi ya Jamii limekuja katika muda mwafaka hivyo tutashirikiana kuhakikisha uchaguzi wa CHW's unafanyika kwa ufasaha.
Ikumbukwe kuwa Uchaguzi wa kuwachagua Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii katika Halmashauri ya Ruangwa unatarajia kuanza mwezi huu ikiwa ni katika Utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii Ulilozinduliwa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango tarehe 30,Januari,2024 na lengo ni kupata Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wapatao 137,294 katika Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara ambapo Utekelezaji wa Mpango huo utafanyika katika kipindi cha miaka mitano kwa awamu .
Katika mwaka wa kwanza (2023/24) zaidi ya Wahudumu 28,000 watafikiwa na baadaye wastani wa Wahudumu 27,324 kila mwaka kwa kipindi cha miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2024/25 hadi 2027/28 nchi nzima.
Utekelezaji wa Mpango huo kwa utaanza katika Mikoa 10 ya kuanzia ikiwemo Kigoma,Kagera,Tabora Lindi, Pwani, Tanga, Songwe, Mbeya, Njombe na Geita.
Mpango huo umelenga kusaidia eneo la Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii na kupunguza idadi ya wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa kuimarisha huduma za afya kinga pamoja na kuongeza tija na ufanisi katika kutoa huduma za afya kufikia lengo la afya kwa wote.
0 comments:
Post a Comment