Home » » KILA MMOJA ANA WAJIBU KUSIMAMIA MPANGO JUMUISHI WA HUDUMA ZA AFYA NGAZI YA JAMII-DC NGOMA.

KILA MMOJA ANA WAJIBU KUSIMAMIA MPANGO JUMUISHI WA HUDUMA ZA AFYA NGAZI YA JAMII-DC NGOMA.

Na. Elimu ya Afya kwa Umma.

Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi Mhe. Hassan Ngoma amewataka Viongozi Serikali za Mitaa katika Wilaya hiyo wakiwemo Maafisa Watendaji wa Vikiji na Kata kuhakikisha wanasimamia vyema Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kwani utakuwa na Manufaa makubwa katika Sekta ya Afya.

Mhe. Ngoma amebainisha hayo tarehe 17, Julai, 2024 Wilayani Ruangwa katika Kikao cha Kuutambulisha Mpango huo kilichokwenda sambamba na Mafunzo kwa Waganga Wafawidhi wa Vituo vya Afya, Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji vyote vya Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa.

"Mpango Jumuishi huu ni mzuri na utaleta matokeo chanya kwenye sekta ya afya ngazi ya Jamii hapa Ruangwa, hivyo tuusimamie ili kupata matokeo tarajiwa"amesema.

Aidha, Mhe. Ngoma amesema katika kuchagua Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ni muhimu kuzingatia sifa muhimu kama zilivyoainishwa kwenye Mpango huo.

"Sifa zilizopo kwenye Mpango huu ni muhimu, tutakosea sana kama tutaamini kuwa matokeo ya kwenye vyeti yatatupa matokeo bora, sifa zilizosema kwenye Mpango mfano utayari wa kujitolea na kushirikiana na jamii ni za muhimu sana kuliko kutegemea matokeo mazuri kwenye vyeti utekelezaji wa kiuhalisia sifuri"amesisitiza.

Halikadhalika, Mhe.Ngoma amempongeza Mbunge wa Jimbo la Ruangwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kwa kuwa Mstari wa mbele katika kuhakakisha Mpango huo unatekelezwa Wilayani Ruangwa.

Afisa Programu kutoka Wizara ya Afya ,Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Mpango wa Taifa wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii Orsolina Tolage amesema katika kuwasogezea huduma za afya wananchi serikali imeamua kuja na Mpango huo ili kuhakikisha kila kaya inafikiwa na huduma za afya.

"Lengo la Serikali ni kuwa na Mpango Jumuishi mmoja maana mwanzoni kulikuwa na huduma tofauti,ukatili, haki za watoto lakini sasa tunataka tuunganishe Afya,Lishe na Ustawi wa Jamii "amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Maafisa Watendaji Kata Wilaya ya Ruangwa Said Seleman amesema wako tayari kutekeleza Mpango huo.


 

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa