Home » » WAMA WAKABIDHI KONTENA LA VIFAA TIBA KWA HOSPITALI YA MKOA WA LINDI

WAMA WAKABIDHI KONTENA LA VIFAA TIBA KWA HOSPITALI YA MKOA WA LINDI

Mama Salma Kikwete.
Na Anna Nkinda – Maelezo, aliyekuwa Lindi
Taaasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) imeikabidhi hospitali ya mkoa wa Lindi Sokoine  kontena lenye  urefu wa futi 40 lenye mitambo na vifaa vya huduma ya afya vya kisasa vyenye thamani ya milioni mia saba, ilivyochangiwa na Shirika linayoshughulika na utoaji wa huduma za kibinadamu la  Project C.U.R.E la nchini Marekani vyenye thamani  ya shilingi milioni mia saba .
Makabidhiano hayo yalifanyika jana katika viwanja vya Hospitali hiyo ambapo Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye pia  Mwenyekiti wa Taasisi hiyo aliwataka wafanyakazi wa hospitali hiyo kuvitunza na kuvitumia vifaa hivyo kwa matumizi yaliyokusudiwa ya kuwahudumia wananchi na si vinginevyo.
Akiongea na wananchi wa mkoa huo pamoja na wahudumu wa afya waliohudhuria hafla hiyo  Mama Kikwete alisema kuwa moja ya sababu za vifo vya kina mama wajawazito na watoto ni ukosefu wa huduma bora ya afya.
Alisema kuwa kutokana na tafiti mbalimbali imeonyesha  kwamba kuna maeneo matatu ya ucheleweshaji ambayo huchangia vifo vingi vya akina mama vinavyotokana na uzazi, ucheleweshaji wa kutoa maamuzi majumbani, umbali kutoka vituo vya afya na ucheleweshaji wa kutoa huduma katika vituo vya afya.
“Eneo linalowahusu wahudumu wa afya ni ucheleweshaji wa kutoa huduma ya afya, katika Hospitali hii bado kuna vifo vingi vinavyotokana na tatizo hili nawaombeni mtathmini  tatizo hili na  muweke mikakati ya kuharakisha utoaji wa huduma kwa kuwa hivi sasa vifaa vingi mnavyohitaji vipo”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA aliendelea kusema kuwa upatikanaji wa huduma bora sio wajibu wa Serikali pekee bali ni wa kila mmoja  kwa nafasi aliyonayo . Kama kila mtu  atatoa mchango wake kikamilifu kwa malengo mengine ya maendeleo ya nchi hakuna mwanamke atakayefariki kwa kukosa huduma ya afya.
Akisoma taarifa ya Hospitali hiyo Kaimu Mganga Mfawidhi Dk. Nicholaus Mmuni alishukuru kwa mitambo na vifaa tiba walivyopewa ambavyo vitasaidia kutoa huduma bora zaidi na kuokoa maisha ya  wananchi kwani walikuwa wanakabiliwa na upungufu wa vifaa hasa vya uchunguzi na vile vya kusaidia kumuhudumia mgonjwa wakati anaendelea kupata huduma ya ndani.
Dk. Mmuni alisema kuwa wastani wa mahudhurio ya wagonjwa kwa siku ni kati ya 80 hadi 100 na wastani wa wagonjwa wanaolala wodini kwa usiku mmoja ni kati ya 70 hadi 100 na huduma wanazozitoa ni kutibu magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukia na utoaji wa chanjo na elimu ya afya kwa umma.
“Changamoto tunazokabiliana nazo ni upungufu wa watumishi hasa madaktari bingwa kwa vitengo vya upasuaji, magonjwa ya wanawake, tiba, watoto na mifupa hata hivyo huduma hizo zinatolewa na watumishi waliopo  kwa kadri ya uwezo na upeo  wa kitaalamu  walionao. Pale ambapo utaalamu zaidi unahitajika  mgonjwa hupewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika hospitali kubwa zenye wataalamu wa tatizo husika”, alisema Dk. huyo.
Kwa upande wake mwakilishi wa Shirika la Project C.U.R.E Dk. Abdul Kimario alimpongeza Mke wa Rais kwa jitihada alizozifanya kwa muda mrefu hadi kuhakikisha kuwa vifaa hivyo vimefika nchini na kuwaomba watanzania wamuunge mkono kukabiliana na upungufu wa vifaa tiba mahospitalini kwani jitihada alizofanya ni kubwa na  amepanda mbegu ambayo itaota kwa miaka mingi.
Dk. Kimario alisema kuwa kabla ya kutumwa kwa vifaa hivyo nchini alikuja kufanya tathimini na kuangalia ni Hospitali gani inamahitaji makubwa zaidi na kugundua kuwa hospiatali za Rukwa (Sumbawanga) na Lindi zinamahitaji makubwa kwa upande wa Lindi mashine yao ya X- ray ilikuwa imeharibika baada ya kupigwa na radi.
“Shirika letu linafanya kazi katika nchi 125 zinazoendelea, tumieni nafasi hii kwa kushirikiana na WAMA ili muweze kupata vifaa tiba katika Hospitali zenu za wilaya na mikoa kwani vifaa tunavyo vingi nyie mnachotakiwa kutoa ni  gharama za kusafirisha kontena tu.
Gharama za kusafirisha kontena moja ni shilingi milioni 30  na vifaa unavyopata vinathamani ya milioni 700 kupatikana kwa vifaa hivyo kutawasaidia wagonjwa kupata matibabu hadi  wilayani  na wale wa warufaa watakuwa wachache”, alisema Dk. Kimario.
Kupatikana kwa vifaa hivyo ni jitihada ya Mama Kikwete za kuhakikisha kuwa vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinapungua hapa nchini kutokana na hilo Shirika la Project C.U.R.E ilifanya harambee ya kumuunga mkono mwezi wa nne mwaka 2011 na kumchangia makontena matano ya vifaa vya afya vyenye thamani ya dola za kimarekani milioni tatu sawa na shilingi bilioni 4.5 za kitanzania.
Kabla ya kutumwa  kwa vifaa hivyo wataalamu kwa afya kutoka Project C.U.R.E walikuja  nchini kufanya tathimini ya vifaa vinavyohitajika katika Hospitali na Kliniki ambazo zilipendekezwa  na wizara ya Afya na Ustawi wa jamii ili kutambua mahitaji mahususi, tecknolojia na nishati iliyopo kwani  kila kifaa kilichotolewa kinahitajika mahali husika  na kinaweza kutumika katika mazingira na tecknolojia iliyopo.
Baadhi ya mitambo iliyokabidhiwa ni  mashine ya X-ray, mitambo na kitanda maalum cha ICU kwajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa mahututi, mitungi ya gesi ya Oxygen ambayo itasaidia kutoa huduma ya dharula hasa wakati ambao umeme utakuwa  umekatika, mitambo na vifaa vya huduma ya tiba ya kinywa na meno, vifaa vya upasuaji mkubwa na mdogo, mashine ya  Ultra sound, Oxygen Concentrators, taa ya meza maaluma ya upasuaji na  mashine ya usingizi.
Makontena mengine yenye mitambo na vifaa tiba vitasambazwa kati Hospitali za mikao ya Simiyu, Tabora, Tumbi, Mtwara  na  Rukwa.

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa