Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa shule ya msingi Ng’au, katika
kata ya Mnacho, Wilayani Ruangwa, alipokuwa kwenye ziara ya kikazi ya
siku moja Wilayani Ruangwa, Novemba 5, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua
ujenzi wa shule ya msingi Ng’au, iliyopo kata ya Mnacho Wilayani
Ruangwa, Novemba 5, 2017.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akimpongeza mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa
Shule ya msingi Ng’au iliypo Wilayani Ruangwa, Daniel Chilemba kwa
kusimamia ujenzi kikamilifu, wakati alipoenda kukagua ujenzi wa shule,
Novemba 5, 2017.
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema wilaya ya Ruangwa inahitaji kuwa na shule
ya sekondari ya wasichana ambayo ni ya bweni ili kupunguza tatizo la
wasichana kukosa elimu.
Ametoa
wito huo jana (Jumapili, Novemba 5, 2017) wakati akizungumza na wakazi
wa kijiji cha Ng’au, kata ya Mnacho wilayani Ruangwa mkoani Lindi ambako
alienda kukagua ujenzi wa shule mpya ya msingi ambayo ujenzi wake
ulianza wiki mbili zilizopita.
“Mpango
wetu ni kujenga shule ya msingi mpya hapa kijijini Ng’au ili watoto
wanaotoka ng’ambo hii wasome hapa hapa. Wakati wa masika nyote mnajua
taabu wanayopata watoto wetu kukatisha kwenda ng’ambo ile,” alisema.
“Nimefurahi
kukuta msingi wa vyumba tisa uko tayari na hii idadi inaweza
kuongezeka. Wanakijiji tushirikiane kujaza kifusi ili kazi ya ujenzi
iende haraka,” alisema.Waziri Mkuu alisema ng’ambo ya pili
kuna shule ya msingi Mnacho ambayo ina madarasa 11 na wanafunzi waliopo
ni karibu 500, na ndoto yake ilikuwa ni kuona ile shule inabadilika na
kuwa ya sekondari.
“Ile
shule ina historia na wakazi wengi kutoka Nandagala, Namahema, Chimbila
‘A’ na Chiemeka wamesoma pale. Mimi mwenyewe nimesoma pale kuanzia
darasa la kwanza hadi la saba. Shule ilishazeeka, ndipo tukatafuta fedha
ili ifanyiwe ukarabati na sasa ina miundombinu mizuri ndiyo sababu
inaonekana inafaa kuwa ya sekondari,” alisema.
“Kwa
vile shule ina miundombinu ya kutosha, ni vema ikawa ya bweni ambayo ni
mahsusi kwa wasichana wa wilaya hii kwani tunalo tatizo la watoto wa
kike kupata elimu, na wanahangaika sana,” alisema.
“Ujenzi
wa hii shule ukikamilika, watoto wale 500 watahamia hapa na walimu wao
na ile pale itapokea wanafunzi sekondari za wilaya hii ili tuwe na
kidato cha kwanza hadi cha nne na ianze mara moja,” alisema.
Alisema
shule hiyo itaitwa Lucas Malia kwa heshima ya mwalimu mkuu wa zamani wa
shule hiyo ambaye alisomesha watu wengi katika wilaya hiyo na wengine
sasa hivi ni viongozi Serikalini na jeshini. Mwalimu Malia hivi sasa ni
marehemu.
Waziri Mkuu amerejea Dodoma leo asubuhi kuendelea na vikao vya Bunge vinavyotarajiwa kuanza kesho (Jumanne, Novemba 7, 2017).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 - DODOMA.
JUMATATU, NOVEMBA 6, 2017.
0 comments:
Post a Comment