WAWEKEZA TRILIONI 4/- KATIKA MBOLEA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com Imeandikwa na Matern Kayera
Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Geoffrey Mwambe
KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) jana kimepokea nyaraka za maombi ya usajili wa kampuni za kuzalisha mbolea ambazo uwekezaji wake una thamani ya dola za Marekani bilioni 1.9 ambazo ni sawa na zaidi ya Sh trilioni 4.
Kampuni hizo ni Ferrostaal kutoka Ujerumani na Haldor Topsoe ya Denmark ambazo zimekuja kuwekeza katika uzalishaji wa mbolea ya chumvi katika eneo la Kilwa Masoko mkoani Lindi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Geoffrey Mwambe wakati wa hafla fupi ya upokeaji wa nyaraka za usajili wa mradi huo. Alisema mradi huo wa mbolea utatumia rasilimali ya gesi asilia inayopatikana hapa nchini katika shughuli zake za uzalishaji na utakuwa ukizalisha tani milioni 1.3 za mbolea kwa mwaka.
“Mbali na kiwango cha tani milioni 1.3 za mbolea zitakazokuwa zikizalishwa kila mwaka, mradi huo pia utaajiri Watanzania 4,500 na wageni 300,” alisema Mwambe. Akifafanua zaidi kuhusu mradi huo, Mwambe alisema kuwa mradi huo utasajiliwa hapa nchini kwa jina la Tanzania Mbolea Petrochemicals (TAMCO).
“TIC tutasimamia na kuhakikisha kila taasisi inayohusika na utoaji wa vibali kama vile vinavyohusu mazingira au vibali vya kufanya kazi na ukaazi kwa ajili ya wataalamu wa kufunga mitambo na mashine vinapatikana kwa wakati ili kampuni itumie muda mfupi kujenga kiwanda chake na sisi tuanze kuona mapema matunda ya mradi huu,” alisema Mwambe.
Mwambe alisema ukubwa wa mradi ni ujumbe tosha kwa wawekezaji mbalimbali duniani kwamba Tanzania ni mahali panapofaa kwa uwekezaji kwa kuwa kuna mazingira rafiki, serikali inayoaminika na kuwepo kwa mfumo unaosaidia kupata uwekezaji mwingi.
Alisema uwekezaji huo ni kichocheo kikubwa katika ukuaji wa sekta ya viwanda lakini pia kwa kipindi kirefu kumekuwa na changamoto katika sekta ya kilimo kutokana na kiasi kikubwa cha mbolea kuagizwa kutoka nje, jambo ambalo kiuchumi halina afya.
“Kuzalisha mbolea hapa nchini kwa kutumia rasilimali zetu, ina maana kuwa mbolea itakuwa inapatikana kwa wakati, itawafikia wakulima kwa urahisi na bei nafuu na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni zilizokuwa zikitumika kuagiza mbolea kutoka nje, lakini pia itaunganisha sekta nyingine za kiuchumi,” alisema Mwambe.
Mwambe alisema mradi huo utasaidia kupunguza tatizo la upatikanaji wa mbolea nchini kwa kuwa mahitaji halisi ya bidhaa hiyo ni zaidi ya tani 350,000. Huu ni uwekezaji mkubwa katika uzalishaji wa pembejeo za kilimo hapa nchini na kuwa uzaishaji wake utapunguza mahitaji ya mbolea ambayo ni tani lakini 3.5.
Kiwanda cha mbolea cha Minjingu huzalisha tani 100,000 kwa mwaka ikiwa ni wastani wa asilimia 20 ya mahitaji yote. Kwa upande wake msimamizi wa mradi huo hapa nchini, Wilfread Wineam alisema kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha tani milioni 1.3 kwa mwaka na asilimia 30 ya mbolea itauzwa hapa nchini na itakayobaki itauzwa nje ya nchi.
Naye Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Detlet Waecheter alisema kutokana na dira ya Tanzania ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, hivyo uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni nao ni muhimu katika kufikia malengo hayo.
Alisema kuwa uwekezaji wa kiwanda cha mbolea ni mwanzo kwa wawekezaji wengine wengi kuja kuwekeza Tanzania na kuahidi kuleta ujumbe mkubwa wa wawekezaji kutoka Jimbo la Bavaria ili kuja kujionea fursa mbalimbali za uwekezaji.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mbolea ya Minjingu iliyopo mkoani Manyara, Pardeep Singh Hans alisema kuwa ni vyema mradi huu ukatekelezwa kwa haraka ili kukamata soko la bidhaa hiyo mapema.
CHANZO HABARI LEO
hatsapp namba +255765056399.

‘RUANGWA INAHITAJI SEKONDARI YA WASICHANA’-WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa shule ya msingi Ng’au, katika kata ya Mnacho, Wilayani Ruangwa, alipokuwa kwenye ziara ya kikazi ya siku moja Wilayani Ruangwa, Novemba 5, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua ujenzi wa shule ya msingi Ng’au, iliyopo kata ya Mnacho Wilayani Ruangwa, Novemba 5, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpongeza mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Shule ya msingi Ng’au iliypo Wilayani Ruangwa, Daniel Chilemba kwa kusimamia ujenzi kikamilifu, wakati alipoenda kukagua ujenzi wa shule, Novemba 5, 2017.
 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema wilaya ya Ruangwa inahitaji kuwa na shule ya sekondari ya wasichana ambayo ni ya bweni ili kupunguza tatizo la wasichana kukosa elimu.

Ametoa wito huo jana (Jumapili, Novemba 5, 2017) wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Ng’au, kata ya Mnacho wilayani Ruangwa mkoani Lindi ambako alienda kukagua ujenzi wa shule mpya ya msingi ambayo ujenzi wake ulianza wiki mbili zilizopita.

“Mpango wetu ni kujenga shule ya msingi mpya hapa kijijini Ng’au ili watoto wanaotoka ng’ambo hii wasome hapa hapa. Wakati wa masika nyote mnajua taabu wanayopata watoto wetu kukatisha kwenda ng’ambo ile,” alisema.

“Nimefurahi kukuta msingi wa vyumba tisa uko tayari na hii idadi inaweza kuongezeka. Wanakijiji tushirikiane kujaza kifusi ili kazi ya ujenzi iende haraka,” alisema.Waziri Mkuu alisema ng’ambo ya pili kuna shule ya msingi Mnacho ambayo ina madarasa 11 na wanafunzi waliopo ni karibu 500, na ndoto yake ilikuwa ni kuona ile shule inabadilika na kuwa ya sekondari.

“Ile shule ina historia na wakazi wengi kutoka Nandagala, Namahema, Chimbila ‘A’ na Chiemeka wamesoma pale. Mimi mwenyewe nimesoma pale kuanzia darasa la kwanza hadi la saba. Shule ilishazeeka, ndipo tukatafuta fedha ili ifanyiwe ukarabati na sasa ina miundombinu mizuri ndiyo sababu inaonekana inafaa kuwa ya sekondari,” alisema.

“Kwa vile shule ina miundombinu ya kutosha, ni vema ikawa ya bweni ambayo ni mahsusi kwa wasichana wa wilaya hii kwani tunalo tatizo la watoto wa kike kupata elimu, na wanahangaika sana,” alisema.

“Ujenzi wa hii shule ukikamilika, watoto wale 500 watahamia hapa na walimu wao na ile pale itapokea wanafunzi sekondari za wilaya hii ili tuwe na kidato cha kwanza hadi cha nne na ianze mara moja,” alisema.

Alisema shule hiyo itaitwa Lucas Malia kwa heshima ya mwalimu mkuu wa zamani wa shule hiyo ambaye alisomesha watu wengi katika wilaya hiyo na wengine sasa hivi ni viongozi Serikalini na jeshini. Mwalimu Malia hivi sasa ni marehemu.

Waziri Mkuu amerejea Dodoma leo asubuhi kuendelea na vikao vya Bunge vinavyotarajiwa kuanza kesho (Jumanne, Novemba 7, 2017).


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 - DODOMA.
JUMATATU, NOVEMBA 6, 2017.
 

WAZIRI MKUU AWAPOKEA WANACHAMA 37 WA UPINZANI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea wanachama wapya 37 kutoka vyama vya CUF na CHADEMA ambao wameamua kurejea Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kwa mujibu wa Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Bw. Barnabas Essau wanachama 35 kati ya hao wametoka CUF na wawili wametoka CHADEMA.Wanachama hao walipokelewa jana (Jumapili, Novemba 5, 2017) kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Mbekenyera, wilayani Ruangwa mkoani Lindi.

Bw. Essau alisema wanachama hao wote wametoka kata za Mbekenyela na Matambalale. Walikabidhiwa kadi mpya za CCM, na kula kiapo cha uaminifu.

Akizungumza kwa niaba ya wanachama wenzake wapya, Bw. Mohammed Issa Ndogoro ambaye amehamia kutoka CHADEMA, alisema wamejiunga na CCM baada ya kuridhishwa na mwelekeo wake. Alisema wameguswa na jinsi Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dk. John Pombe Magufuli inavyofanya kazi ya kutatua kero za wananchi. 

Alisema amekaa upinzani kwa miaka 23 lakini anaikubali CCM sababu ya uwazi wake na ameshangaa kuona akipewa kadi na stakabadhi ya walipo yenye jina lake, jambo ambalo hajawahi kuliona katika vyama vingine vya upinzani.

“Sote sisi tumehamia CCM, uhai wa chama ni michango. Nani aseme hapa kama aliwahi kupewa stakabadhi katika chama chake, na kama yupo nampa sh. 5,000/- sasa hivi,” alisema Bw. Ndogoro na kuamsha kicheko kwenye mkutano huo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 - DODOMA.
JUMATATU, NOVEMBA 6, 2017.

WAZIRI MKUU AHIMIZA LINDI WAJIPANGE MAANDALIZI YA BARAZA LA MAULID KITAIFA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wana-Lindi na wana-Ruangwa watumie fursa zilizopo ili kufanikisha maandalizi ya sherehe za Maulid na Baraza la Maulid Kitaifa mwaka huu.
Ametoa wito huo leo (Jumapili, Novemba 5, 2017) wakati akizungumza na viongozi wa dini ya Kiislamu wa Mkoa wa Lindi na wilaya ya Ruangwa mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ziara ya siku moja.
Waziri Mkuu amesema sherehe hizo zitafanyika Desemba mosi kwa mkesha wa Maulid na kufuatiwa na Baraza la Maulid litakalofanyika Desemba 2, saa 3 asubuhi kwenye viwanja vya shule ya msingi Likangale.
Aliwataka wana-Ruangwa waharakishe kujenga nyumba za kulala wageni na sehemu za kula ili waweze kupokea ugeni huo mkubwa wa kitaifa. “Kila mmoja anayeona hapo kuna fursa, ni lazima aitumie vizuri,” alisisitiza.
“Kwa niaba ya wana-Ruangwa, tunamshukuru Mheshimiwa Mufti na Baraza la Maulamaa kwa kuridhia sherehe hizi zifanyike kitaifa hapa wilayani kwetu. Nitumie fursa hii kuwaomba Waislamu wote tuungane katika sherehe hizi licha ya tofauti za madhehebu yetu tuliyonayo,” alisema.
Alisema uamuzi huo wa BAKWATA ulitangazwa kwenye Baraza la Maulid lililofanyika Singida, mwaka jana ya kwamba wameamua kuadhimisha sherehe hizo kwenye ngazi ya wilaya badala ya kuwa inafanyika makao makuu kila mwaka.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaarifu viongozi hao kwamba maandalizi yanaendelea na kwamba vifaa mbalimbali kama mchele, vitoweo, unga wa ngano, sukari, maji, juisi, mahema, mikeka na mazulia vimekwishapatikana.
“Ninaomba Kamati ya Uhamasishaji iifanye kazi hii kwa kutambua kuwa jambo hili si la kwenu peke yenu, bali linaungwa mkono na Serikali, na hii ni kwa sababu Serikali yenu inafanya kazi kwa karibu sana na viongozi wa dini,” alisema.
Alisema misingi ya amani katika nchi hii imejengwa na mahubiri ya viongozi wa dini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Uhamasishaji, Sheikh Ali Mohammed Mtopa alisema Ruagwa iko tayari na imepokea wito huo wa kitaifa. “Tunakuhakikishia wewe Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wawakilishi wa Mufti waliopo hapa kwamba tumepokea hiyo heshima,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Itifaki kutoka BAKWATA Makao Makuu na Msimamizi wa Malidi za Kitaifa, Sheikh Mohammad Nassir ambaye alisema wana Ruangwa an wana Lindi wanalo jukumu la kuhamasisha watu washiriki sherehe hizo.
“Hamasa haitatoka Morogoro au Dar es Salaam bali hapahapa Lindi. Tunataraji watu wasiopungua 10,000 watahudhuria sherehe hizi za Maulid kutoka wilaya zote za mkoa wa Lindi na hii ni mbali wawakilishi kutoka kila mkoa wapatao 100 -150,” alisema.
Waziri Mkuu anatembelea vijiji vya jimboni mwake ambako atahutubia wananchi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
JUMAPILI, NOVEMBA 5, 2017.

WATAKAOKWAMISHA MALIPO YA KOROSHO KUKIONA- WAZIRI MKUU MAJALIWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itawashughulikia watu wote watakaokwamisha malipo ya wakulima wa zao la korosho.

“Hatutamuacha mtu yeyote atakayesababisha wakulima kuchelewa kulipwa fedha zao. Tutawakamata wote na kuwachukulia hatua stahiki.”

Ametoa kauli hiyo jana (Jumapili, Novemba 5, 2017) alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Mbekenyera wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Waziri Mkuu alisema wakulima hao ni lazima walipwe fedha zao kwa wakati na asitokee mtu wa kuzitamani fedha hizo.

“Mkulima amelima mikorosho mwenyewe, ameokotoa na kukodoa mwenyewe wao wamepewa dhamana ya kuziuza, hivyo wahakikishe wanawapelekea fedha zao na wala wasizitamani.”

Pia Waziri Mkuu amewataka viongozi wa vyama vya Ushirika vya Msingi wahakikishe mkulima hakosi sh. 3,500 katika kilo moja ya korosho atakayoiuza baada ya kukatwa michango.

Alisema bei ya juu ya korosho katika minada ya mkoa wa Lindi sh. ni 3,970 na ya chini sh. 3,800. “Vyovyote itakavyokuwa mkulima hawezi kukosa sh. 3,500, viongozi wa AMCOS mnisikie.” Waziri Mkuu alisema hatua hiyo inatokana na kuongezeka kwa bei ya zao la korosho pamoja na kupungua kwa makato ya mkulima ambapo kwa sasa hayazidi sh. 300 katika kilo moja ya korosho.

NAPE AGEUKA MBOGO BAADA YA KUDHIHAKIWA MTANDAONI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mbunge wa jimbo la Mtama (CCM) Nape Nnauye ameonyesha kukasilishwa na moja ya shabiki katika mtandao wake wa Twitter ambaye amemzihaki na kumwita mnafiki kutokana na ujumbe alioweka, Nape amedai watu wa namna hiyo ni zaidi wa wachawi. 

Leo asubuhi Nape aliweka ujumbe kupitia mtandao wake unaosomeka "Usivunje mtungi kwa sababu ya panya aliyemo ndani ya mtungi, inamisha taratibu, fanya 'timing', utaua panya na mtungi utabaki salama" 
Baada ya kuandika ujumbe huo ndipo moja ya mtu akaja na kumwambia kuwa kiongozi huyo amekua mnafiki baada ya kuvuliwa nafasi ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na kudai kuwa kiongozi huyo amekuwa akiomkosoa boss wake, jambo ambalo Nape Nnauye wiki iliyopita alisema anachukizwa kuona watu wakichukua mambo yako na kuyahusisha na kumsema au kumkosoa Rais jambo ambalo si la kweli. 

"Mkuu we mnafiki sana yote hayo umeanza baaada ya kuvuliwa uwaziri 'come on' kiongozi bora si  yule anaonekana mkosoaji kwa boss wake" aliandika Majdy Wiliam 

WATENDAJI WANAOCHUKUA RUSHWA KWENYE VITUO VYA UKAGUZI WA MAZOA YA MISITU KUKIONA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Prof Dos Santos Silayo akiwa kwenye mkutano na watendaji wake wa Kanda ya Kusini (hawapo pichani) muda mfupi kabla ya kuwataka meneja kuchukukua hatua kwa watendaji wasio waadilifu mapema hivi leo.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Kanda ya Kusini Ebrantino Mgiye (mwenye koti jeusi) akiwasolisha mafanikio na changamoto zinazoikabili kanda huku akifuatiliwa kwa umakini na Meneja Msaidizi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu Bw. Gaudence Kilasi (aliyekaa) mapema hivi leo.
Baadhi ya Watendaji wa TFS Kanda ya Kusini wakichukua kumbukumbu katika Kikao cha Wafanyakazi kilichoendeshwa na Mtendaji Mkuu wa TFS Prof Dos Santos Silayo kuanza kuzungumza nao mapema hivi leo hii.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Prof Dos Santos Silayo akimfuatilia kwa umakini Kaimu Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Kanda ya Kusini Ebrantino Mgiye (hayupo pichani) alipokuwa akiwasilisha mafanikio na changamoto ya miaka mitatu ya kanda hiyo mapema hivi leo.

Na Tulizo Kilaga Lindi

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Prof Dos Santos Silayo amewataka meneja wa misitu nchini kusita kuchukua hatua pale wanapokuwa na ushahidi dhidi ya watendaji wanaojihusisha na vitendo vya rushwa kwenye vituo vya ukaguzi wa mazao ya misitu.

Ametoa agizo hilo leo tarehe 04/10/2017, alipotembelea na kuzungumza na wafanyakazi wa TFS Kanda ya Kusini katika ofisi za Wilaya ya Lindi ya Taasisi hiyo.

“Kuna tuhuma za hovyo nimesikia, watu wanakamatwa na mazao ya misitu yaliyovunwa ama kusafirishwa kinyume na sheria, wanaombwa kitu kidogo na baadhi ya watumishi wasio waaminifu ili kuhalalisha mizigo hiyo na wakigoma, mizigo yao hukamatwa, nataka kuwaona mnachukua hatua stahiki,”amesema.

Mtendaji Mkuu ameeleza kuwa licha ya TFS kuwa na changamoto nyingi anaimani na taasisi hiyo na amewataka watendaji wake kufanya kazi kwa kushirikiana na kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya na kuzingatia weledi, uzalendo na uadilifu, akiahidi Serikali kufanyia kazi changamoto zinazowakabili.

Awali, Kaimu Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Kanda ya Kusini Ebrantino Mgiye alisema miongoni mwa changamoto zinazokabili taasisi hiyo ni pamoja na uhaba wa watendaji.

Hata hivyo, Mtendaji Mkuu amewataka watendaji wa TFS kujikita katika utendaji wa kimkakati ili kuboresha usimamizi na uhifadhi wa raslimali za misitu na Nyuki kwa ajili ya kuchangia katika mahitaji ya kijamii, kiuchumi, ki-ikolojia, na ki-utamaduni kwa kizazi cha sasa na kijacho.


RAIS WA CHAMA CHA WAUGUZI TANZANIA (TANNA) AONGOZA KIKAO CHA WAUGUZI HAO MKOANI LINDI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Rais wa Chama Cha Wauguzi Tanzania (TANNA), Paul Magesa (katikati) akifungua kikao cha kamati ya Mkutano Mkuu wa 45 wa maandalizi ya chama hicho Mkoani Lindi jana. kulia ni Mwenyekiti wa chama cha hicho Mkoa wa Lindi, Patrick Achimpota na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Sebastian Luziga. 
Mwenyekiti wa chama cha Wauguzi (TANNA) Mkoa wa Lindi, Patrick Achimpota (kulia), akizungumza jambo wakati wa kikao hicho, kushoto ni Katibu Mkuu wa Chama hicho, Sebastian Luziga na Rais wa Chama Cha Wauguzi Tanzania (TANNA), Paul Magesa.
Viongozi mbalimbali na wajumbe wakisikiliza kwa makini wakati Rais wa Chama cha Wauguzi (TANNA), Paul Magesa alipokuwa akizungumza jambo.
Viongozi na wajumbe wakifuatilia kwa umakini.
Wajumbe wa Mkutano huo wakisikiliza kwa umakini.
Dokt. Sophia Khaify (kulia) akisalimiana na Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania, Paul Magesa mara baada ya kufunga kikao hicho cha Kamati ya Maandalizi jana.
Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA), Paul Magesa (kulia) akisalimiana na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Lindi, Ngwechele Makenge, anaye shuhudia katikati ni Makamu wa Rais wa Chama hicho, Ibrahim Mgoo.
Makamu wa Rais wa Chama cha Wauguzi (TANNA), Ibrahim Mgoo (kulia), akisalimiana na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Lindi, Ngwechele Makenge.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Lindi, Ngwechele Makenge akizungumza jambo na viongozi mbalimbali wa chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA), pichani hawapo.
(PICHA ZOTE NA KHAMISI MUSSA).

WAJUMBE MKUTANO MKUU WA 45 CHAMA CHA WAUGUZI TANZANIA (TANNA) SAFARINI LINDI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Wauguzi Tanzania  (TANNA)  kutoka sehemu mbalimbali wakiungana na wajumbe wenzao pamoja na viongozi wa Tanna Mkoa wa Lindi jana katika kufanya maandalizi ya Mkutano Mkutano Mkuu  wa 45 unao tarajiwa kufanyika Oktoba 4-6 Kitaifa  ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mh. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.( PICHA ZOTE NA KHAMISI MUSSA)

 Mwenyekiti wa Chama Cha Wauguzi Tanzania (TANNA) Mkoa wa Lindi, Patrick Achimpota (kulia) mwenyeshati la kitenge akisalimiana na mjumbe wa Kamati kuu ya Chama hicho kutoka Arusha, Hosea Naman mara alipofika Mkoani humo kwa niaba ya Mkutano Mkuu wa Chama hicho.


 Wajumbe wa Chama Cha Wauguzi (TANNA) wakiwa katika safari kuelekea Mkoa wa Lindi katika Mkutano Mkuu wa Chama hicho  unao tarajiwa kufanyika Oktoba 4-6 Kitaifa ambapo unatarajiwa kufunguliwa na Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa. Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Mkoa Lindi, Damasiana Msala (kulia)  akizungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Wauguzi (TANNA) mara walipowasili katika mkoa huo jana
 Makamu wa Rais wa Chama hicho, Ibrahim Mgoo (wa katikati) akisalimia wajumbe mara baada ya kuwasili katika Mkoa huo jana, kulia ni Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Mkoa Lindi, Damasiana Msala na kushoto ni Katibu Mkuu wa Chama hicho, Sebastian Luziga. 

JENGENI UTAMADUNI WA KUWAPENDA NA KUWAHESHIMU WAGONJWA-MAKINDA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

 Madaktari Bingwa wakiendelea kumpa huduma mmoja wa wangonjwa wa macho katika hospitali ya Sokoine Lindi.
Baadhi ya vifaa tiba na dawa zilizotumika katika zoezi hilo vikikabidhiwa kwa mkuu wa mkoa wa Lindi Bwana Godfrey Zambi.
 Daktari Bingwa wa watoto Martha Mkonyi akimuhudumia mmoja wa watoto waliokuja kupata huduma.

MWENYEKITI wa Bodi  ya Wakurugenzi wa Mfuko  wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Spika Mstaafu  Anne Makinda amewahimiza watoa huduma katika vituo vya matibabu kujenga utamaduni wa kuwapenda na kuwaheshimu wagonjwa ili kuwapa faraja na huduma bora wanapokwenda kupata matibabu katika vituo vyao.

Akizunguza wakati wa uzinduzi wa huduma za madaktari bingwa katika mikoa ya Mtwara na Lindi, Mama Makinda amesema wagonjwa wengi hususan wanawake wajawazito wanaogopa kwenda kupata huduma za mazitbabu katika vituo hivyo kutokana na mapokezi mabaya wanayopata hivyo wanaamua kwenda kwa wakunga wa jadi au kujifungulia majumbani ambako hakuna mazingira salama.

Amesisitiza kuwa wahudumu wa vituo vya matibabu wanawajibika kuwa na lugha nzuri na huruma kwa wagonjwa kwani kazi wanayofanya inaweza kuwa na mafanikio au madhara makubwa kwa afya za watu wanapwahudumia.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bwana Bernald Konga amesema Mfuko huo umepania kufikisha huduma bora kwa kila mtanzania hivyo hatua ya kupeleka madaktari bingwa katika mikoa yenye mahitaji makubwa ya huduma hiyo ni hatua mojawapo ya kusogeza huduma karibu na watanzania wengi.

Amesema kuanzia mwaka 2013 hadi sasa Mfuko umeshapeleka madaktari bingwa katika mikoa 17 ambapo mikoa minne imepata huduma hizo mara mbili. Mikoa hiyo ni pamoja na Kigoma, Rukwa, Lindi na Mtwara. 

Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka minne cha utekelezaji wa mpango huo katika mikoa ya pembezoni zaidi ya wananchi Elfu Kumi na Tisa wamehudumiwa na madaktari bingwa ambapo zaidi ya Mia saba wamefanyiwa upasuaji wa kibingwa.

TUMEANZA KUIONJA SHUBIRI YA VITA YA UCHUMI.


Na Bashir Yakub. 

Tumegusa uchumi wa bepari. Mara zote, na kote duniani bepari alipoguswa kwenye uchumi wake basi ametumia mbinu hizi hapa chini kuhakikisha anapambana na waliomzuia.

[a] Kumwita kiongozi anayeongoza vita ya uchumi Mvunjaji wa haki za binadamu na asiyefaa. Imetokea kwa Gaddafi baada ya kumnyima bepari mafuta, halikadhalika kwa Saddam Hussein.Pia ndilo tatizo la Mugabe na bepari baada ya kurudisha mashamba kwa wazawa ili wafaidi uchumi wao.

[b] Kuratibu na kufanikisha matukio ya ajabu kwenye jamii ili kuleta faraka,taharuki, chuki, uadui, na sintofahamu.Bepari analiweza sana hili hasa nchi za Afrika kutokana na uwezo wake mkubwa wa fedha na teknolojia.

Lengo la mbinu hii ni :
Mosi,kuwatoa kwenye ajenda ya vita dhidi yake na kuwaelekeza kwenye mijadala mingine.
Pili, kuchonganisha watu, serikali na viongozi wao.
Tatu, kupeleka ujumbe duniani kuwa kiongozi fulani na serikali yake hawafai tena.
Nne, kuligawa taifa kati ya upande unaoamini matukio kutekelezwa na fulani na upande unaoamini vingine.

[c] Kuandaa mapinduzi kwa kuwatumia wasaidizi wa rais na viongozi wenye tamaa.

[d] Kuandaa maandamamo makubwa ambayo mwisho wake ni kuuondoa utawala uliodhibiti uchumi .

Utaona waandamanaji wanalalamika kuchoshwa na mambo mbalimbali lakini nyuma yao ni fedha, mbinu na mipango ya bepari.

Bila hata waandamanaji kujua isipokuwa wachache/viongozi wao. Mbinu hii imetumika hivi karibuni kuondoa viongozi wengi wa Afrika ya Kaskazini waliodhibiti uchumi wao kwa mda mrefu.

[e] Kufadhili makundi ya waasi Mf. Congo, Sudani Kusini, Sierra Leone, Liberia nk. Mnajua kuwa hadi baadhi ya makundi ya kigaidi hufadhiliwa na hawa jamaa.

Badala ya kujadili udhibiti wa rasilimali zenu mnajadili amani itapatikana vipi huku bepari akitumia nafasi hiyo kuiba.

[f] Kufadhili na kuviimarisha vyama vya upinzani hasa vyenye tamaa ili hatimaye na kwa namna yoyote ile viondoe madarakani viongozi waliombana bepari.

[g] Kutafuta sababu na hatimaye kuweka vikwazo vya kiuchumi kwa nchi husika ili kulainisha au kumaliza kabisa misimamo ya serikali na viongozi dhidi ya rasirimali anazozitaka bepari.

Pia lengo ni kuwafanya wananchi wapate taabu ili wachoshwe na utawala uliombana bepari na hivyo kufanya maamuzi ya kuuondoa kwa namna yoyote. nk, nk, nk............


NINI MFANYE KTK KIPINDI KAMA HIKI.


[a] Kushikamana na kutokubali kutenganishwa kwa matukio.

[b]Kutokuwa na majibu ya haraka katika mambo makubwa.

[c] Vyombo vya usalama kujiimarisha kiulinzi na kuhakikisha vinafika kwenye majibu ya mzizi wa kila tukio na kutoa taarifa kwa wakati kwa umma.

[d] Vyombo vya usalama kutokubali kusaidiwa upelelezi na nchi za mabepari kwakuwa mwanya huo hutumika kutoa majawabu aidha yanayokwepesha(divert) ukweli au yanayokamilisha malengo yaliyokusudiwa.

[e] Kuepuka kabisa kuchanganya tofauti zetu za kisiasa za tokea huko nyuma na yanayotokea sasa.

YAPI MADHARA YA KUTOSHIKAMANA KIPINDI KAMA HIKI.

Bepari hana hasara, wenye hasara ni mimi na wewe. Mpango wa wagawe uwatawale "divide&rule" haikuishia kwenye ukoloni. Bado ungalipo.

Kama tutakubali kugawanywa na majaribu ya bepari , sawa na tugawanywe tu , ila ahadi ni hii kuwa kila mmoja ataonja joto la jiwe.

Wewe uliyekubali kugawanywa utaonja na ambaye hakukubali ataonja. Mtaona Iraq na Libya aliyeshiriki na ambaye hakushiriki wote wanaonja.

Hakuna atakayekuzuia kukomaa na msimamo wako. Hakuna atakayekuzuia  kuamini mbowe ndiye aliyefanya tukio fulani ili kumzuia fulani kugombea uenyekiti. Hakuna atakayekuzuia kuamini kuwa Lowassa ndiye aliyefanya tukio fulani ili kumzuia fulani kugombea urais 2020. Lakini pia hakuna atakayekuzuia kuamini kuwa serikali ndiyo iliyofanya tukio fulani kwasababu yule au ofisi ile kuna wabaya au wakosoaji wake. 

Wewe amini hivyohivyo unavyoamini ila kaa ukijua kuwa ikiwa tutagawanyika tu, basi kila mtu, kila familia, kila kundi, kila chama, na imani yako hiyohiyo uliyonayo yatakufika. Madhara ya bepari yanapokuja hayaangalii nani alikuwa akiamini nini, ama nani alitumia gani tukio kumsema nani. 

Mtaona Libya kusini ina serikali yake, kaskazini ina serikali yake , magharibi yake na mashariki yake.Ni vipandevipande, shida juu ya shida. Na humo wamo wote walioshiriki na ambao hawakushiriki. Madhara ya bepari hayaangalii aliyeshiriki na ambaye hakushiriki. 

Kwahiyo wewe msaidie tu bepari kwakujua au kutokujua kueneza propaganda zake kwa matukio anayoyaandaa ila ujue kuwa mwisho wa tamthilia tutakuwa wote tuu. Wala huna pa kwenda ndugu tutalia wote humuhumu. 

Na mkishakuwa nyang’anyang’a, bepari ameshawashinda, na hamna tena la  kumfanya, na sasa anawageuza anavyotaka, basi hapo bepari atakuja na kusema ukweli kuwa si fulani aliyefanya tukio fulani bali ni sisi kwa lengo fulani. 

Mnakumbuka wale walioiharibu Iraq baadae walisema ukweli. Waliandika vitabu kuwa vita ile ilikuwa ya makosa na kule hakukuwa na silaha za sumu kabisa. Ni baada ya kuiharibu vibaya sana nchi hiyo na kuiletea dhiki na mashaka makubwa.

Mnakumbuka walioiharibu Libya nao baadae walisema ukweli. Sasa wanasema wazi kuwa makundi waliyoyatumia kumg’oa Gaddaffi hayakuwa makundi sahihi bali ya imani kali. 

Lakini mwanzoni walikataa kuwa hawako nyuma ya makundi yaliyoanzisha  maandamano na kusema kuwa wananchi waliochoka udikteta wa Gaddaffi ndio wanaoandamana. Bepari akishakumaliza anakiri. Basi kwa kiwango gani mnakuwa mmedhalilika na kudharauliwa ndugu zangu. Ni lini wananchi wa Afrika tutajifunza kutoka matukio haya. 

Tunawalaumu viongozi wetu waafrika lakini pia sisi wananchi wa Afrika kwa nafasi zetu kama wananchi tunayo mambo ya kujifunza na kushughulikia lakini hatufanyi hivyo. Ni lini basi tutaacha kudhalilishwa na bepari. Toka ukoloni mpaka uhuru hatujifunzi tuu ndugu zangu. Basi tutajifunza lini , makaburini ama.

Tujihadhari kwani kwetu tayari bepari ameanza kwa matukio ya hapa na pale. Tukimuunga mkono kwa vinywa vyetu huku tukijua tunamkomoa kiongozi fulani au chama fulani, basi atatuvuta taratibu taratibu mpaka huko Libya na Iraq halafu yeye aendelee kuiba kama alivyokuwa amezoea awali.

Ndugu zangu, tunawasifia Angola na Botswana kwa kumbana bepari na hatimaye kufaidi rasimali zao sasa.

Lazima tujue wamefikia hapo baada ya kushikamana na kuzishinda hila, fisadi, fitna,na mitihani ya bepari. Na sisi tunaweza.


TUTARAJIE MATUKIO ZAIDI.

Matukio bado , huu ni mwanzo tu. Hivi mlitarajia bepari abanwe halafu tubaki salama. Haiwezekani. Historia inakataa jambo hilo. Bepari lazima akutingishe.

Kama ingekuwa tumbane bepari halafu tubaki
salama basi isingeitwa Vita ya Uchumi bali Sherehe ama tafrija ya Uchumi. Yanini iitwe vita kama mmembana bepari na bado mkaendelea kuwa salama na kufurahia maisha. Hii ni vita na sasa mnaweza kuanza kuona taswira ya vita yenyewe.

Vitimbi na matukio yatakuja mengi. Lengo ni moja tu , kuua vita hii ili bepari aendeleze alikoishia.

Msishangae wakaanza kudhuliwa hata wanaoonekana wana mtazamo tofauti na mwenyekiti ndani ya chama tawala ili chama kigawanyike na hatimaye serikali igawanyike. Bepari anajua ukigawa chama kinachotawala  umeigawa serikali kwakuwa wanachama wa chama tawala ndio huunda serikali.

Hivyo kwa kufanikiwa kukigawa chama kinachotawala bepari anajua atakuwa amefanikiwa kuigawa serikali.

Ukifanikiwa kuigawa serikali maana yake bepari amepunguza kasi ya vita dhidi yake lakini maana yake pia anakaribia kumwondoa kabisa adui aliyebana uchumi wake.

Bepari haoni tabu kumdhuru yeyote ama chochote ili kutimiza malengo yake. Bepari anajua ukimdhuru kiongozi mwenye mawazo tofauti ndani ya chama ama serikali , basi watanyoosheana vidole. Yule aliyedhuriwa atapata kundi lake wanaoamini ameonewa na wale wengine watabaki kundi jingine. Bepari  anajua kuwa hata kiongozi awe mkali ama na msimamo kiasi gani hawezi kusimama kama wasaidizi wake wamegawanyika. 

Ni vita ya uchumi , na sasa tunaonja shubiri yake. Ila tutashinda.


MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MCHAMBUZI WA MASUALA YA SIASA. 0784482959.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa