Na Jacquiline Mrisho
Serikali
imetenga jumla ya shilingi bilioni 48.3 kwa ajili ya kujenga Mahakama
40 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ili kuongeza ufanisi na kuharakisha
hukumu za kesi katika ngazi mbalimbali nchini.
Kutokana
na fedha itakayotumika kujenga mahakama, shilingi bilioni 36 zinatokana
na Bajeti ya mwaka huu wa fedha wakati shilingi bilioni 12.3 zilitolewa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe
Magufuli.
Hayo
yamebainishwa leo mjini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria,
Dkt. Harisson Mwakyembe alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Iramba
Mashariki Mhe. Allan Kiula aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itatoa
fedha kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama za Wilaya na uteuzi wa Mahakimu
katika ngazi hiyo.
Waziri
Mwakyembe amesema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha Mahakama
zinakuwepo kila wilaya ili kuwaondolea usumbufu wananchi, kurahisisha
usikilizwaji wa kesi pamoja na kupunguza gharama kwa wananchi kutoka
sehemu moja kwenda nyingine kufuata Mahakama zilipo.
“Kwa
mujibu wa Katiba ya Nchi, Sheria na Kanuni inaeleza kuwa kila Mahakama
ina mipaka yake hivyo hatuwezi kubadilisha mahakama ya mwanzo kutumika
kama ya wilaya” amesema Dkt. Mwakyembe.
Ameongeza
kuwa mpaka sasa bado kuna wilaya zinapata huduma ya Mahakama kupitia
wilaya nyingine ambapo amewahakikishia Wabunge na wananchi kuwa Serikali
itajenga mahakama 40 kwa mwaka huu wa fedha.
Akifafanua
mgawanyiko wa Mahakama 40 zinazotarajiwa kujengwa nchini, Dkt.
Mwakyembe amesema kuwa Serikali itajenga Mahakama Kuu nne, Mahakama za
mikoa sita, Mahakama za Wilaya 14 na Mahakama za Mwanzo 16 katika wilaya
mbalimbali nchini.
Aidha,
Mhe. Mwakyembe ametaja baadhi ya vigezo vinavyotumika kuanzisha
Mahakama katika eneo lolote kuwa pamoja na uwepo wa hati ya kisheria ya
kuwepo kwa wilaya, mkoa, kata na kijiji, umbali wa upatikanaji wa huduma
za Mahakama, idadi ya wakazi wa eneo husika pamoja na uwepo wa huduma zingine za kipolisi na magereza.
Ameongeza
kuwa kutokana na changamoto hizo za kukosekana kwa mahakama katika
maeneo ambayo yamekidhi vigezo ndiyo yaliyopelekea Serikali kujipanga
kujenga Mahakama hizo ambapo ametoa rai kwa wananchi kuwa na subira
wakati wakikusubiri kujengwa kwa Mahakama hizo.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment