Home » » Basi laua watu 10 Lindi

Basi laua watu 10 Lindi


WATU 10 wamekufa na wengine 44 kujeruhiwa katika ajali ya basi la Kampuni ya Barcelona lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Newala mkoani Mtwara jana.
Ajali hiyo ni ya jana saa 5 asubuhi katika kijiji cha Miteja wilayani Kilwa mkoani Lindi, umbali wa kilometa 30 kutoka mkoa wa Pwani na miongoni mwa waliopoteza maisha wamo watoto wadogo watatu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, Renata Mzinga akizungumza kwa simu na gazeti hili jana, alisema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa dereva ambaye bado wameshindwa kumhoji kwa kuwa ni miongoni mwa majeruhi na mpaka jana jioni alikuwa amepoteza fahamu.
“Ni kweli ajali imetokea asubuhi saa tano leo (jana), dereva alikuwa katika mwendo kasi, basi likapasuka tairi la mbele, likapinduka. Majeruhi wapo 44 na waliokufa ni 10, wanawake sita na mwanamume mmoja, mtoto wa kike mmoja na wakiume wawili,” alisema Kamanda Mzinga.
Kamanda Mzinga alilitaja basi hilo kuwa ni lenye namba za usajili T110 CUU Youtong, mali ya Kampuni ya Barcelona.
Alisema majeruhi wote wapo katika Hospitali ya Wilaya ya Kilwa iliyopo eneo la Kivinje na miili pia ipo katika hospitali hiyo. Hata hivyo, alisema waliokufa itachukua muda kuwatambua kwa kuwa basi lilikuwa linapita, halikuwa linaishia Lindi. Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, alieleza kuwa,
“basi limepinduka, abiria wamelaliwa, matairi yapo juu, wataalamu wanasema itafutwe gesi lichomwe ili watu wapate kuokolewa. Huwezi kuangalia mara mbili, ajali mbaya. Tairi la mbele limepasuka.”
Ajali zimeendelea kupoteza maisha ya Watanzania na hivi karibuni, mwishoni mwa Septemba, ajali nyingine iliua watu 13 jijini Mwanza na wengine 11 wakijeruhiwa.
Ajali hiyo ilihusisha basi dogo (Hiace) lenye namba za usajili T368 CWQ lililokuwa likotokea kijiji cha Shirima kwenda Mwanza mjini na basi aina ya Scania lenye namba za usajili T874 CWE, Super Shem.

CHANZO GAZETI LA HABARI LEO

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa