Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mgombea
Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Mke wa
Rais na Mjumbe wa NEC, Mama Salma Kikwete mara baada ya kumwombea kura kwa
wananchi wa Manispaa ya Lindi kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye
uwanja wa Mpilipili Aliyesimama kulia ni Mgombea Ubunge
katika Jimbo la Mtama Ndugu Nape Nnauye.
Na Anna Nkinda – Maelezo,
Liwale
Wananchi wa
mkoa wa Lindi wameaswa kufanya kazi kwa bidii ili waweze kujiletea mabadiliko ya
kweli katika maisha yao kwani kuna baadhi ya watu hawapendi kufanya kazi huku
wakisubiri mabadiliko.
Rai hiyo imetolewa jana
na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Ngunichile na Mbaya vilivyopo
katika majimbo ya Nachingwea na Liwale waliohudhuria mkutano wa kampeni ya kuwanadi wagombea wa
nafasi za udiwani, ubunge na urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mama Kikwete ambaye ni Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia wilaya ya Lindi mjini alisema mabadiliko
ya kweli hayawezi kupatikana bila ya kufanya kazi kwani kuna baadhi ya watu
hasa vijana hawafanyi kazi wakiamka asubuhi kitu wanachokifanya ni kucheza pool huku wakisubiri mabadiliko.
“Hata katika vitabu vya
dini imeandikwa asiyefanya kazi na asile kwani kazi ni msingi wa maendeleo, hata ukipiga kelele kiasi gani kama hufanyi
kazi huwezi kupata mabadiliko katika maisha yako”.
“Ndugu zangu Mwenyezi
Mungu ametupa akili ya kutambua mema na mabaya tusikubali kudanganywa, mabadiliko
ya siku hizi siyo mazuri yanaleta uvunjifu wa Amani kwani watu wamepandikizwa
maneno ya chuki wanafanya vurumai na kuharibu vya kwao, wanawachukia ndugu zao imefikia
hatua watu hawazikani, hawasalimiani. Lakini hao aliowapandikiza chuki kwao
kuna maendeleo”, alisisitiza.
Mama Kikwete alisema yeye
kama MNEC anadhamana kubwa ya kuhakikisha anakisemea na kukipigania chama
chake na kuwataka wananchi hao kushikamana na kuwa kitu kimoja kwa kufanya
hivyo wataitunza Amani ya nchi na kuzidi kudumisha upendo katika jamii yao.
Aidha aliwasihi wananchi
hao kutokubali kurubuniwa na kitu chochote bali wazitunze kadi zao za kupigia
kura na siku ya uchaguzi ikifika wasipoteze haki yao ya msingi ya kupiga kura
wajitokeze kwa wingi na kuwachagua viongozi kutoka CCM ambao watawaletea
maendeleo ya kweli.
Kwa upande wake mgombea
ubunge jimbo la Nachingwea Hassan
Massala aliahidi kama atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo atasimamia ilani ya
uchaguzi ya CCM na kuhakikisha huduma za
elimu zinaboreshwa hii ni pamoja na shule
kuwa na vitabu na walimu wa kutosha na
kujenga nyumba za walimu ili watoto wapate elimu bora. Ataboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
kila kijiji kinakuwa na Zahanati na dawa zinapatikana kwa wakati.
Massala alisema, “Katika
jimbo hili, maeneo ya mjini kuna maji ya kutosha lakini kijiji cha Ngunichile kuna
tatizo ingawa vyanzo vya maji vipo. Nitahakikisha maji yanapatikana. Kuhusu
umeme Serikali inampango wa kusambaza katika
vijiji vyote, nguzo zimeanza kusambazwa kinachohitajika
ni kusimamia ili zoezi hili liende haraka”.
Mgombea huyo wa nafasi ya
Ubunge alimuomba Mama Kikwete awasaidie ili mnara wa mawasiliano ya simu uweze
kujengwa katika kata ya Ngunichile kwani eneo hilo linashida ya
mawasiliano.
“Ukiwa katika kijiji hiki
huwezi kuwasiliana na mtu yeyote kwa
njia ya simu kwa kuwa hakuna mnara wa mawasiliano. Hivi sasa simu ni pesa na simu ni Benki
tunaomba Mama yetu utusaidie ili mnara wa mawasiliano ujengwe katika kijiji
hiki”, Massala aliomba.
Kuhusu ombi la kujengewa
mnara wa mawasiliano ya simu katika kijiji hicho ambacho ni kata ya Ngunichile Mama Kikwete aliahidi
kulifanyia kazi na kulifikisha kunakohusika.
Naye mgombea
ubunge wa jimbo la Liwale Faith Mitambo aliwaomba wananchi wamchague ili
aendelee kuwatumikia kwa kipindi kingine cha miaka mitano na kuhakikisha
maendeleo yanazidi kupatikana katika jimbo hilo.
Mitambo alisema, “Ilani ya uchaguzi ya CCM
inasema itaendelea kuboresha huduma ya afya na ndani ya mwaka mmoja baada ya
uchaguzi Zahanati ya kijiji cha Mbaya itakuwa kituo cha Afya. Aidha Serikali
imetenga zaidi ya shilingi bilioni tatu kwa
ajili ya kuhakikisha umeme unapatikana vijijini kati ya vijiji hivyo kimojawapo
ni kijiji hiki.
“Nawaomba kura zenu ili mtuchague viongozi
kutoka CCM ambao ni madiwani, mbunge na rais ili tuweze kusimamia na kutekeleza
kwa vitendo na kuhakikisha yale yote yaliyoandikwa katika ilani ya uchaguzi
yanatekelezwa”,.
0 comments:
Post a Comment