Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Habari
zilizotufikia hivi punde zinaarifu kuwa Mwanasiasa Mkongwe nchini
Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi (74)
amefariki dunia hii leo mchana.
Dk Makaidi pia alikuwa ni Mwenyekiti Mwenza wa Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na vyama vya NLD, Chadema, CUF, na NCCR Mageuzi.
Kifo cha Makaidi kimethibitishwa na Viongozi wenzake wa NLD ambao wanadai kupata taarifa kutoka kwa mjane wa marehemu Modesta Ponera.
Dk Emmanuel Makaidi ni mhandisi aliyebobea. Alizaliwa Aprili 10, 1941 huko
wilayani Masasi mkoani Mtwara. Baba yake mzazi alikuwa ni katekista wa Kanisa
la Anglikana.
Alianza elimu katika Shule ya Msingi Namalenga
wilayani Masasi kati ya mwaka 1948 – 1952, mwaka 1953 – 1954 alisoma katika
Shule ya Kati (Middle school) iitwayo Luatala hukohuko Masasi. Baadaye
alijiunga na Shule ya Sekondari ya Chuo cha Mtakatifu Joseph na kusoma kidato
cha kwanza hadi cha nne kati ya mwaka 1953 hadi 1956.
Makaidi alisoma darasa la 13 na 14 (kidato cha
tano na sita) katika Shule ya Sekondari Luhule, Uganda kati ya mwaka 1957 –
1958. Alipelekwa Uganda si kwa sababu ya kipato cha baba yake, la hasha,
alisaidiwa na Askofu wa Anglikana baada ya kuona anafaulu mitihani yake kwa
alama za juu sana. SOMA ZAIDI BOFYA HAPA
Makaidi aliendelea kufadhiliwa na askofu huyo
ambaye alimuunganisha na mashirika mengine na kumtafutia chuo Afrika ya Kusini.
Akapelekwa Chuo Kikuu cha Witwatersrand na kuhitimu Shahada ya Uendeshaji na
Usimamizi kati ya mwaka 1958 – 1960.
Baada ya kuhitimu vizuri pale Witts, aliendelea
kupata ufadhili wa masomo ya shahada ya uzamili, mara hii alielekea Marekani na
kusoma masuala ya Menejimenti na Utawala kwa ngazi ya uzamili kati ya mwaka
1960 – 1962. Alisoma pia katika Chuo Kikuu cha Howard kilichoko jijini
Washington, Marekani.
Baada ya kurejea nchini akiwa mhitimu wa M.A,
Makaidi alianza kazi serikalini mwaka 1966 hadi mwaka 1973 akiwa mchambuzi kazi
mkuu, katika kitengo cha Utumishi.
Kati ya mwaka 1974 na 1975 (miaka miwili).
Alirudi tena Marekani na kusoma Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sayansi ya
Siasa katika Chuo Kikuu cha Howard akipata kuwa karibu na mmoja wa maprofesa
nguli duniani, Wamba Dia Wamba. Makaidi ameniambia kuwa hata tabia ya kuandika
vitabu na kutunga mambo ya ubunifu, alifundishwa na profesa huyu mahiri.
Aliporejea nchini kwa mara ya pili mwaka 1976
aliendelea na kazi yake pale Utumishi hadi mwaka 1985 alipopewa kazi nyingine
kubwa zaidi, akawa Mkurugenzi wa Miundo na Mishahara kwenye kamati iliyokuwa
inashughulikia mashirika ya umma nchini.
Wakati anaendelea na kazi utumishi, alipata
fursa nyingine ya kusomea stashahada ya Kuchakata Taarifa za Kielektoniki
katika Chuo Kikuu cha Trinity, Ireland. Alikwenda huko na kuhitimu mwaka huohuo
1977.
Kabla hajafanya kazi katika kamati maalum ya
kusimamia mashirika ya umma akapandishwa cheo na kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara
ya Kazi na Ustawi wa Jamii na mwaka huohuo 1985 akafukuzwa kazi.
Kisa cha Makaidi kufukuzwa kazi serikalini, tena
akiwa na wadhifa huo ilikuwa ni kwa sababu ya kuandika kitabu cha Kiingereza
chenye jina “mwanasiasa mwenye roho ya shetani”. Serikali ikamzonga vilivyo,
ikamtuhumu kuwa kitabu kile kinamtukana Mwalimu Julius Nyerere. Mwisho wa siku
“kazi ikaota mbawa”.
Bahati nzuri, mwaka huohuo 1985 akaajiriwa na
Shirika la Finwork Directory kuwa Mkurugenzi Mtendaji, kazi aliyoifanya hadi
mwaka 1991.
Kuanzia mwaka 1992 hadi hivi leo, Dk Makaidi
hajajishughulisha tena na kazi za serikalini wala mashirika binafsi. Amejiajiri
akiwa na kampuni kadhaa zilizoajiri Watanzania wa vipato vya kawaida, lakini
pia ameendelea kutoa ushauri wa kitaalamu kwa kampuni za ndani na nje ya nchi
huku akiongoza chama cha NLD akiwa Mwenyekiti.
Dk Makaidi ni mwandishi mzuri wa vitabu, ameshaandika
zaidi ya 10. Amemuoa Modesta Ponela na wana watoto wanane.
MBIO ZA
UBUNGE
Dk Makaidi alijitosa katika mbio za ubunge kwa
mara ya kwanza mwaka 2010 katika Jimbo la Masasi, Mtwara akipambana na Mariam
Kasembe wa CCM (aliyeibuka mshindi wa jumla kwa asilimia 63.7) na Clara Mwatuka
wa CUF (aliyepata asilimia 15.2). Katika uchaguzi huo Dk Makaidi alishika
nafasi ya tatu kwa kupata kura 5,384 sawa na asilimia 11.7 ya kura zote
zilizopigwa.
Januari 2014, Dk Makaidi alikuwa mmoja wa
Watanzania walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba ambalo liliendeleza mchakato wa kikatiba, ulioanzishwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
MBIO ZA URAIS
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Dk Makaidi
alipitishwa na chama chake, NLD, kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Ni mmoja wa wagombea waliofika katika maeneo kadhaa ya nchi kuomba
kura pamoja na kuwa chama chake hakikuwa na nguvu kubwa ya kisiasa na hata
uchumi. Kwenye uchaguzi ule ambao mshindi alikuwa Kikwete, Dk Makaidi alipata
asilimia 0.19 ya kura zote zilizopigwa na kushika nafasi ya saba kati ya wagombea
10 waliokuwa wanashindana.
0 comments:
Post a Comment