Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba.
Chama cha Wananchi (CUF) kimebaini kuwapo dosari
lukuki katika uandikishaji wapigakura katika Daftari la Kudumu la
Wapigakura unaondelea katika mikoa ya kusini ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,
Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, alisema viongozi wa
CUF walifanya ziara katika mikoa hiyo na kukuta changamoto mbalimbali
zikiwamo waandishi kutokuwa na uzoefu na mashine za BVR kutofanya kazi,
hali iliyosababisha wananchi wengi kukosa haki zao za msingi.
“Katika vituo vingi, uandikishaji ulisuasua kwa sababu waandishi
wengi walionekana kukosa uzoefu, mashine kushindwa kufanya kazi
inavyotakiwa,” alisema na kuongeza:
“Hali hii ilisababisha wananchi kuachwa bila kuandikishwa. katika daftari la wapigakura.”
Prof. Lipumba alisema walibaini kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi(Nec)
haikufanya jitihada za kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi
kushiriki kujiandikisha huku akisisitiza taarifa zilichelewa kufikishwa
kwa wakati.
Aidha, alisema muda wa siku saba uliotengwa na Nec haukutosha
kuandikisha wananchi wote wenye haki ya kuwa wapigakura akiiomba Nec
iongeze angalau wiki mbili.
Alisema bajeti iliyotengwa kwa ajili ya kuandikisha wapigakura
haitoshelezi kuweka waandishi wengi katika vituo kwa kuwa kwenye vituo
hivyo kuna waandishi wawili wanaofanya kazi kuanzia saa 2:00 asubuhi
mpaka saa12:00 jioni hali inayosababisha kushindwa kuwahudumia wananchi
ipasavyo.
Prof. Lipumba alisema katika baadhi ya wilaya kama Tunduru BVR kits
hazitumiwi kutokana na Nec kutokuwa na fedha za kutosha za kuwalipa
waandikishaji huku akitaja waandishi hulipwa Sh. 100,000 kwa wiki wengi
wao wakiwa wanakaa katika maeneo ambayo siyo nyumbani.
Aliongeza kuwa baadhi ya vituo kulikuwa na matatizo ya
kutotambuliwa kituo ambacho mpiga kura amejiandikisha na kitambulisho
alichopewa akitolea mfano wilaya ya Newala kituo cha kuandikisha cha
Mahoha, kadi ya mpigakura ilisomeka Nambari A wakati kijiji cha Nambali
kiko kilometa 15 kutoka kituoni hapo.
Alisema katika Kata ya Michemo kituo cha kuandikisha cha Mchemo A
kadi ya mpiga kura ilisomeka kata ya Mpwapwa huku waandikishaji
waliondolewa wakiwa wameandikisha watu 31 wakati makadirio ya kata nzima
ni wapiga kura 3059.
Alifafanua katika Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Naibu Katibu
Mkuu wa CUF Bara, Magdalena Sakaya, alishuhudia wananchi wengi ambao
hawakuandikishwa katika vituo wiki ya kwanza, lakini mashine za BVR
zilondolewa na kwamba alipomuuliza mkurugenzi wa wilaya hiyo hakuwa na
majibu kwa wananchi.
Pia, katika kijiji cha Mlonde kata ya Mtemanga wilaya ya Tunduru,
alisema asilimia 60 ya wananchi wenye haki ya kuwa wapigakura
hawakuandikishwa na cha kushangaza mashine zilihamishwa.
Alisema idadi ya wapiga kura ni 2,260, lakini walioandikishwa ni
920 tu huku katika Kata ya Namwinyu kiyuo cha Uliya na Ndenyenge siku
mbili za mwanzo walaindikishwa watu wanne tu.
Prof. Lipumba alisema ugawaji wa BVR kit hauna uwiano na idadi ya
wapiga kura waliopo kwenye vituo akitolea mfano Kata ya Majimaji
wilayani Tunduru, kituo cha shule ya msingi na Chalinze kina wapigakura
8,000, lakini kila kituo kilipewa mashine moja.
Alisema kuna vituo vyenye wapigakura 200 mpaka 1,000 vimepewa BVR
kit mbili hadi nne wakati vituo vyenye watu 2,000-2,800 vilipewa BVR
kits moja.
Hata hivyo, Prof. Lipumba alisema kuna mikakati ya kuonekana tume
imefikia mikoa yote bila kuwapa fursa wananchi wote wenye haki ya kuwa
wapigakura kujiandikisha akibainisha kuna hatari wengi wakanyimwa fursa
ya kuwa wapigakura.
Aliitaka serikali iipe Nec fedha za kutosha kukamilisha mchakato
wa kuandikisha na kuacha kupoteza fedha nyingi katika maandalizi ya kura
ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
Alipoulizwa Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, alisema
mchakato wa uandikishaji unaendelea vizuri na dosari hizo zitatatuliwa
daftari litakapokamilika kwa kuangalia maeneo husika.
“Niko mkoani Mtwara wilayani Masasi, uandikishaji unaendelea vizuri
hakuna dosari kubwa ni ndogo ndogo ambazo haziwezi kuathiri,
zitarekebishwa mara tu daftari likapokamilika, alisema Jaji Lubuva.
Alisema katika maeneo ambayo mashine za BVR zilionekana
kutokutosheleza idadi ya wapiga kura zilichukuliwa sehemu nyingine na
kupelekwa katika maeneo hayo.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment