Home » » TAS YAJA JUU MAUAJI YA ALBINO

TAS YAJA JUU MAUAJI YA ALBINO

Mwenyekiti wa chama cha watu wenye ulemavu Tanzania (TAS) �Tanzania Albino Society� ndugu Ernest Kimaya.
 
Chama cha Albino Tanzania (TAS) kimeitaka serikali kufanya utafiti juu ya mauaji yanayoendelea kutokea dhidi yao, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii ili wafahamu kuwa viungo na ngozi za watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) hazina utajiri.
Pia kimeitaka serikali kutumia nguvu zilezile inazozitumia kuwasaka vijana wahalifu, maarufu kama “Panya road” kuwatafuta vinara wa mauaji na utekaji wa albino.

Afisa Uhusiano wa TAS, Josephat Toner, alisema hayo alipozungumza na NIPASHE kuhusiana na matukio ya mauaji dhidi ya albino pamoja na tukio la kutekwa nyara kwa mtoto, Pendo Shilinde, mwenye umri wa miaka minne, lililotokea Desemba 28, mwaka jana, katika Kijiji cha Ndami, mkoani Mwanza.

Alisema mpaka sasa albino zaidi ya 73 wamefariki dunia, huku 56 wakiwa wamejeruhiwa na wengine 11 wakiachwa na ulemavu wa kudumu.

Toner alisema waliojeruhiwa ni wale walionusurika katika matukio ya mauaji.

Alisema mbali na hayo, pia watoto watatu wamepotea, ambao mpaka sasa hawajulikani waliko.

Toner alisema watu zaidi ya 200 walikamatwa kutokana na vitendo hivyo, lakini cha kushangaza kesi 11 ndizo zilizopelekwa mahakamani, kati ya hizo, tano ndizo zimekwisha kutolewa hukumu.

“Hii ni wazi kuwa nguvu ya ziada inahitajika kunusuru kizazi cha watu wenye ualbino Tanzania,” alisema Toner.

Alisema inasikitisha kuona Watanzania wakiwawinda kama wanyama wenzao albino kwa lengo la kuwaua, huku wakiwa na imani za kishirikina kuwa viungo vya watu hao vinaleta utajiri.

“Sisi tuna imani kuwa serikali yetu ina nguvu kubwa. Hivyo, tunaomba iongeze bidii za kuwasaka wauaji na watekaji wa watu wenye ualbino, kwani tunaishi kama wakimbizi ndani ya nchi yetu,” alisema Toner.

Alisema watuhumiwa wanaokamatwa kuhusika na mauaji hayo siyo wahusika wakuu wa biashara haramu ya viungo vya binadamu, kwani upo mtandao mkubwa, ambao unawatuma watu kuyafanya.

Toner alisema serikali iliamua kuanzisha kambi za albino baada ya kuona hali inakuwa mbaya.

Hata hivyo, alisema kambi nyingi zipo katika hali mbaya, ikiwamo ya Shinyanga na Kigoma, kutokana na kupokea idadi kubwa ya watu.

“Serikali inabidi iliangalie hili kwa umakini sana. Kwani kuwakimbiza katika kambi watu wenye ualbino siyo njia ya kutatua matatizo yao ya kuwindwa, bali tunapaswa kujiuliza, nani yupo nyuma ya wauaji?” alihoji Toner.

Alisema wimbi la mauaji dhidi ya albino limesababisha ndoa nyingi kuvunjika kutokana na baadhi ya watu ulemavu huo kuogopa kuolewa na kuishi na wasiokuwa albino.

Hata hivyo, alisema kuna dalili kubwa ya kudumaza elimu kwa watoto, kwani wazazi wanaogopa kuwapeleka watoto zao shule wakihofia kutekwa au kuuliwa na mara nyingine wanakuwa na kipato kidogo, hivyo kushindwa kumudu kuwapeleka shule za kulala.

Alisema albino wamekuwa wanakosa ajira kutokana na ulemavu wao, kwani waajiri wengi wamekuwa wakiogopa kuwaajiri wakihofia kutekwa au kuuawa.
 
SOURCE: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa