Home » » VIJANA MSITUMIKE KATIKA VURUGU

VIJANA MSITUMIKE KATIKA VURUGU

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi Mjini, Mama Salma Kikwete amewataka vijana kuwa na msimamo na kutokubali kutumika katika vurugu zinazohatarisha amani na usalama wa nchi.
Alitoa rai hiyo hivi karibuni wakati akifungua shina la vijana wakereketwa la kikundi cha zahanati Kempu lililopo Kata ya Rasibura wilaya ya Lindi Mjini.
Alisema vijana wengi hawajui historia ya nchi, hivyo basi baadhi ya watu wasio na nia njema wanaitumia nafasi hiyo kuwarubuni na kuwashawishi kufanya vurugu zinarudisha nyuma maendeleo ya eneo husika.
“Msikubali mkoa wetu wa Lindi kuwa kichaka cha majaribio na kutumika katika vurugu, kuweni na msimamo wa kuitetea amani yetu kwani mkifanya vurugu matatizo yanapotokea ninyi ndiyo mnaoangamia na hao waliowashawishi wanawakimbia. Kama atakuja mtu hapa na kuwashawishi kwa ajili ya shughuli za maendeleo ni sawa hakuna atakayezuia tunahitaji kuwa na maendeleo katika mkoa wetu, lakini kuwashawishi ili mfanye vurugu na kuharibu vichache tulivyonavyo msikubali”, alisema Mama Kikwete.
Aidha, aliwasisitiza vijana kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili waweze kujiletea maendeleo yao na ya mkoa huo kwa kuwa vijana ndiyo wanaotegemewa na ni nguvu kazi ya Taifa.
Akisoma taarifa ya kikundi hicho, Hidaya Chivii ambaye ni mtunza fedha, alisema kikundi hicho kilianzishwa Julai 5, 2014 kikiwa na wanachama 23, kati ya hao wanaume ni 18 na wanawake ni watano.
Chivii alisema madhumuni ya kuanzishwa kwa kikundi hicho, ambacho kinajihusisha na kazi ya kuendesha pikipiki (bodoboda) kwa upande wa wanaume na ususi kwa upande wa wanawake ni kujikwamua na hali ngumu ya maisha na kuweza kujiendeleza.
“Waendesha pikipiki tunakabiliwa na changamoto ya kunyang’anywa pikipiki hasa ifikapo wakati wa uchaguzi, kwani wamiliki wengi ni wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) na sisi ni wanachama wa CCM au wanatupa pikipiki zao kwa masharti magumu yakiwemo ya kukipigia kura chama chao”, alisema Chivii.
Alitaja changamoto nyingine zinazowakabili kuwa ni kutokuwa na vitendea kazi vyao wenyewe na kutokupata mafunzo ya ujasiriamali.
Wakati huo huo, Mama Kikwete alifanya vikao na viongozi wa Halmashauri Kuu ya tawi ya CCM katika matawi ya Kilimahewa na barabara ya Kawawa na kuwahimiza wajumbe kuendelea kushikamana na kuwa kitu kimoja ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Akiwa katika tawi la Kilimahewa lililopo Kata ya Mwenge, aliwapokea vijana wanne kutoka Chama cha Wananchi (CUF) ambao walijiunga na CCM.
Chanzo:Habari Leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa