Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mbunge huyo anayesifika kwa kujenga hoja bungeni, anahoji wanapokwenda
nusu ya wanafunzi wanaomaliza shule kila mwaka na kushindwa kuendelea na
masomo
Kila baada ya matokeo ya mitihani ya taifa kutolewa, taifa hugubikwa na mijadala mingi kuhusu hali ya elimu nchini.
Hata hivyo, mijadala hiyo hupita kama upepo, japo
mara nyingi matokeo hayo huacha simanzi kubwa kuhusu hali halisi ya
sekta ya elimu ilivyo nchini.
Ni simanzi itokanayo na matokeo mabaya ambayo pia yanaonyesha kuwepo kwa walakini katika sekta ya elimu.
Walakini huu kwa mujibu wa mbunge wa Kigoma
Kaskazini, Zitto Kabwe haujatafutiwa mwarobaini na kibaya zaidi haoni
jitihada zozote za dhati za kurekebisha hali ya mambo kabla
hayajaharibika.
“Kwa jumla, sekta ya elimu imetelekezwa na watu
wanazungumza kama elimu haina mwenyewe. Iko haja ya kuzungumza kwa
umakini kabla mambo hayajaharibika kabisa,’’ anasema.
“Tunahitaji kuhakikisha kwamba kuna usimamizi
mzuri katika elimu. Hivi sasa yanatoka matokeo mabaya kidato cha nne au
sita watu wanapiga kelele, lakini baada ya wiki tunaendelea na maisha
kama kawaida.”
Zitto, mbunge kijana aliyejizolea sifa kubwa
katika duru za siasa nchini, anasema hali duni ya elimu inajidhihirisha
katika shule za umma ambazo miaka ya nyuma zilikuwa kimbilio la wengi,
lakini sasa zinakimbiwa.
Enzi hizo, anasema Zitto kuwa wazazi walifikia
hatua ya kufanya hila na udanganyifu, alimradi watoto wao wasome katika
shule hizo zilizokuwa zikitamba kwa taaluma.
Hali ya sasa ya elimu
Zito anataja masuala kadhaa yaliyosabaisha sekta
ya elimu kuwa katika hali mbaya kuwa ni pamoja na uamuzi wa Serikali
kuwaondoa wakaguzi wa elimu shuleni.
“Kuua wakaguzi wa elimu kumeshusha kiwango cha
elimu. Nakumbuka wakati nasoma, mkaguzi alikuwa anaingia darasani
anasimama nyuma, anamwangalia mwalimu wakati anafundisha. Hii ilichochea
uimara wa elimu wakati ule,” anasema.
Suala jingine ni walimu na mchango katika kukuza kiwango cha elimu nchini.
Anasema taifa haliwezi kuzungumzia elimu bila kuwatazama walimu anaosema ni roho ya taifa katika kuandaa rasilimali ya taifa.
“Ndiyo maana wengine tunaona tukiachana na siasa
tutakwenda kufundisha, kwa sababu ni kazi inayosaidia kuzalisha
rasilimali watu,” anaeleza.
Hata hivyo, anasema badala ya kujali wajibu huu
walio nao walimu, watumishi hao wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira
yanayosikitisha, hivyo kuathiri maisha na ustawi wao.
“Tutapata pesa za rada tutanunua vitabu, zitakuja
nyingine zitanunua madawati, lakini kama maisha ya walimu wetu
hayataboreshwa ni nani atakayewaelimisha watoto? “ anahoji.
Kwa kuwa anaamini walimu ndiyo nguzo ya elimu,
anasema aliwahi kushauri walimu hasa wanaofundisha maeneo ya vijijini
kulipwa mara mbili ya mishahara ya kawaida.
“Niliwahi kutoa wazo kuwa kwa nini elimu isiwe na
mfumo wake peke yake. Niliwahi kuwahoji wenzangu kwa nini tusiwape
walimu wa vijijini mshahara mara mbili ya kawaida ili kuwavutia
kuendelea kubaki, lakini wenzangu wakasema ‘aah sijui nini na nini’.
Nikawaambia elimu siyo majengo, bali ni hawa wenzetu wanaofundisha,”
anasema.
Walimu kunyonywa
Zitto anasema pamoja na walimu kuwa katika hali
ngumu, bado wanaandamwa na madeni mengi kutoka katika taasisi za fedha
nchini zinazowatoza riba kubwa.
“Jimboni kwangu kuna tatizo kubwa la walimu na
mikopo, naamini hili lipo nchi nzima kwa sababu nimeshawahi kulisikia,
yaani, mwisho wa mwezi mwalimu mshahara wake ni sifuri,’’ anasema.
“Niliongea na Mukoba (Gratian), wakati ule akiwa
Chama cha Walimu Tanzania (CWT), huyu ambaye sasa yupo Tucta,
nikamuuliza kwa nini chama chenu kisiwe na benki yake wenyewe ili
imkopeshe kwa riba ndogo?
“Nikamwambia hivi nyinyi mnakusanya fedha za walimu, PSPF (Mfuko) wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma wanakusanya fedha za walimu.
Asilimia 60 ya wachangiaji wa mfuko huo ni walimu,
nikamwambia lazima CWT na PSPF wakutane waone jinsi wanavyoweza
kuwasaidia wateja wao (walimu) katika kukabiliana na janga la mikopo.
Kwenye vikundi wanawatoza mpaka riba za asilimia 40.
Swali la kujiuliza
Mbunge huyo anayesifika kwa kujenga hoja bungeni,
anahoji wanapokwenda nusu ya wanafunzi wanaomaliza shule kila mwaka na
kushindwa kuendelea na masomo.
“Asilimia 50 ya watoto wanafeli mitihani,
wanakwenda wapi? Hapa tunapozungumza watoto milioni 12 wapo shuleni,
yaani msingi na sekondari. Tujiulize, wanakwenda wapi baada ya hapa?”
anahoji.
Ili kujinusuru na hili, anashauri serikali na
wadau kuwekeza ipasavyo katika mfumo wa elimu ya ufundi kama njia ya
kuwasaidia wanafunzi hao wanaoshia njiani.
“ Hiki kitu hakitakuwa kipya, kulikuwa na shule za
ufundi za Dar Tech, Mbeya, Moshi, Tanga na nyinginezo. Waanzilishi wa
taifa hili walikuwa na maono kwamba si kila mtu tunaweza kumpeleka chuo
kikuu,” anaeleza.
Anakumbushia ahadi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya
kujenga chuo cha ufundi kila wilaya na kwamba hata sasa inawezekana
kufanya mabadiliko kwa kuzijenga nyingine kwa kuzitumia kambi za mafunzo
ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
“Kila kambi ya JKT iwe ni chuo cha ufundi,
unahitaji Sh796 bilioni ili kuwa na chuo kila wilaya. Fedha hizi huwezi
kuzipata mara moja, ila unachoweza kufanya ni kuiunganisha Veta (Mamlaka
ya Elimu ya Ufundi) na JKT,”anafafanua.
Anasema kuwa faida ya mfumo huu ni kuwa kila
kijana anayehitimu atakuwa na uhakika wa kujiajiri na baadaye
anaunganishwa na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa manufaa ya baadaye.
“Kama ni seremala anapewa vifaa, yaani anatoka
anakwenda moja kwa moja kujiajiri. Pia, hiyo mifuko ya jamii inakuwa
imepata wanachama wa uhakika,” anasema na kuongeza:
“ Hivi sasa kuna kiwango cha hali ya juu cha
uhalifu, hii yote inatokana na ukweli kwamba vijana wengi hawana kazi.
Kila siku tunasikia watu wanapigwa risasi, kama hatutalifanyia kazi hii,
ipo siku tutaamka, watu wa Manzese watavamia Masaki na kwa kuwa wanajua
hawana cha kupoteza.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment