Home » » WAOMBA OPERESHENI TOKOMEZA MAUAJI YA ALBINO

WAOMBA OPERESHENI TOKOMEZA MAUAJI YA ALBINO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

SHIRIKISHO la vyama vya watu wenye ulemavu Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi (SHIVYAWATA) limeiomba Serikali kuendesha operesheni maalumu ya kutokomeza vitendo vya mauaji dhidi ya walemavu wa ngozi (albino) ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati kwa ajili ya kuwabaini watu wanaojihusisha na matukio hayo ili sheria ichukue mkondo wake.
Mwito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Shirikisho hilo, Hamisi Jabiri wakati anazungumza na Habari- Leo ofisini kwake kuhusu mfululizo wa matukio ya kuuawa na kukatwa viungo kwa watu wenye ulemavu wa ngozi nchini.
Alisema pamoja na shirikisho hilo wilayani Ruangwa kulaani na kusikitishwa na mwendelezo wa matukio hayo na kutaka uchunguzi wa kina ufanyike, ipo haja Serikali ikaendesha operesheni ya kuwasaka watu wanaojihusisha na matukio ya kuuawa kwa walemavu wa ngozi.
Jabiri ameiomba Serikali kuwawekea mazingira yaliyobora kiusalama zaidi ili kudhibiti matukio ya kuuawa albino yasiendelee kutokea kwani yanawafanya waishi kwa wasiwasi na kushindwa kufanya shughuli za maendeleo kwa amani.
“Mbona operesheni kimbunga kuhusu ujangili imefanyika kwa mafanikio kwanini Serikali pia isifanye operesheni kuhusu matukio ya walemavu wa ngozi?” Alihoji Jabiri.
Alisema ukosefu wa chombo maalumu kinachoshughulikia changamoto za walemavu hapa nchini ni sababu moja wapo ya kushindikana kwa udhibiti wa matukio hayo ya kukatwa viungo na kuuawa kwa walemavu wa ngozi na kwamba Serikali sasa inapaswa kutilia mkazo wa kuanza kutafuta mwarobaini wa vitendo hivyo.
Chanzo;Habari Leo 

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa