Home » » WEREMA AKOSOLEWA

WEREMA AKOSOLEWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Jaji Frederick Werema
 
Wadau kadhaa wamepingana na kauli zilizotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, kuhusiana na mchakato wa Katiba mpya.
Wadau hao wamekosoa kauli kuwa Rais hana mamlaka ya kuliahirisha Bunge Maalum la Katiba na suala la kuifanyia marekebisho Katiba ya mwaka 1977 kwa mara ya 15.

Jaji Werema alisema Ijumaa iliyopita kuwa, Rais Jakaya Kikwete hana mamlaka kisheria ya kulivunja Bunge Maalum la Katiba na kwamba ikiwa Bunge hilo litashindwa kupata theluthi mbili ya wajumbe kutoka pande zote za Muungano kupitisha Katiba inayopendekezwa, itabidi liitishwe Bunge la Jamhuri ya Muungano kufanya marekebisho ya 15 ya Katiba ya mwaka 1977 kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Mambo matatu yatakayoingizwa kwa mujibu wa Jaji Werema ni kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi, kuruhusu mgombea binafsi na kupunguza madaraka ya Rais.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimesema Rais anayo mamlaka kisheria kulivunja Bunge Maalum la Katiba na kupinga kauli ya  Jaji Frederick Werema (pichani) kuwa hana mamlaka hayo kisheria.

Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Harold Sungusia, alisema kifungu cha 22 sura ya 83 katika sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo inampa Rais mamlaka ya kuteua na kwamba kama anaweza kuteua pia anaweza kufuta uteuzi huo.

Alisema kilichosemwa na Werema ni siasa huku akijua kwamba mamlaka ya Rais ni makubwa na kwamba hashindwi kusitisha mchakato wa kuandika Katiba mpya.

“Werema anajua mamlaka ya Rais, lakini aliamua kufanya siasa ili kuonyesha kwamba hakuna mtu yoyote mwenye uwezo kusimamisha mchakato wala kulivunja Bunge," alisema Sungusia.

Hata hivyo, alisema kwamba sheria kuhusu mchakato mzima ilitungwa kimtego mtego na kwamba Bunge la Jamhuri bado lina uwezo wa kuzirekebisha ili kuondoa utata uliopo.

Aliongeza kuwa, kama hakuna dhamira ya kweli ya kupata Katiba Mpya ni bora Bunge likasitishwa ili kuokoa fedha za walipa kodi ambazo zinaendelea kuteketea Dodoma.

Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amemjia juu Jaji Werema, akimtaka kuacha kisingizio kuwa Bunge hilo haliwezi kuahirishwa kwa kuwa lipo kisheria.

Alisema sheria na kanuni zilizotumika kuahirisha awamu ya kwanza ya Bunge hilo, ambalo lilipewa siku 70, lakini likaahirishwa kabla ya siku hizo, ili kupisha Bunge la Bajeti, zinapaswa kutumika pia kulisitisha sasa.

“Kuna dhana kuwa Bunge hilo linaloendelea lipo kisheria na Rais hawezi kulivunja. Awali lilipewa siku 70 na Rais akaliongezea muda wa siku 20, lakini lilitimiza siku 68 tu na likaahirishwa. Sasa sheria iliyotumika kuliahirisha ilitoka wapi?” alihoji Mbatia na kuongeza:

 “Viongozi hawa wanahitajika kuacha unafiki kwa kuwa maslahi ya Taifa ni zaidi ya Werema, Sitta, Mbatia na Rais Kikwete. Sheria iliyotumika kuahirisha Bunge la awali itumike sasa. Katiba haiwezi kuundwa kwa maslahi ya watu wa upande mmoja.”

Akizungumzia kauli ya Jaji Werema kuwa iwapo mchakato huo utakwama itabidi kurudi bungeni ili kubadili sheria, alisema siyo sahihi, kwani linaweza kuchukua muda mrefu, ikiwamo uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu, kuchelewa kufanyika.

Mbatia alisema endapo mchakato huo utapita kutahitajika kura ya maoni kutoka kwa wananchi na kuhoji ni daftari gani litakalotumika kuweka kumbukumbu, kwani Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imekwishasema haina daftari la kudumu la wapigakura.

Alisema iwapo suala la daftari la kudumu la wapigakura lisipowezeshwa kutumika katika mchakato huo kunaweza kuhatarisha amani ya nchi na kuleta machafuko.

“Tume inalazimisha kubadili mfumo wa daftari kieletroniki. Ni jambo lisilowezekana kutokana na nchi yetu kutokuwa na umeme wa uhakika. Mfano nchi za Kenya, Afrika Kusini, Malawi, Ghana na nchi nyingine za Kiafrika hawakuweza kufanikiwa na kusababisha vurugu nchini mwao,” alisema Mbatia.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, alisema kauli ya Jaji Werema haina  tofauti na aliyotangulia kusema  kuwa nchi haihitaji kupata katiba mpya.

Dk. Slaa alisema hakuna mwanachi yeyote atakayeshangazwa na kauli za kiongozi huyo kwa kuwa hazina tofauti na hazina faida kwa Watanzania.
Alisema ikiwa mwanasheria huyo aliwahi kusema nchi hahitaji kupata katiba mpya, leo anasema ikishindikana kupatikana, Bunge la Tanzania litaitishwa.

“Tunahitaji yanayosemwa yatekelezwe, kama kurekebisha baadhi ya vifungu basi tushuhudie kwa vitendo siyo maneno matupu,” alisema.
Mkuu wa Idara ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Mohammed Bakari, alisema kauli hiyo  inaonyesha dhahiri kuwa serikali  na chama tawala wasivyo tayari kupatikana kwa Katiba mpya.

“Kauli zinazoendelea kutolewa na viongozi wa serikali zinakatisha tamaa kwani hazina mashiko, zinaonyesha wazi jinsi serikali isivyoona haja ya kupatikana katiba mpya, ingekuwa vyema  Bunge hilo likaahirishwa kwa manufaa ya wananchi,” alisema Prof. Bakari.

“Tangu mwaka 1977 serikali iliyopo madarakani imeng’ang’ania kuvifanyia marekebisho madogo madogo kwenye  baadhi ya vifungu vilivyomo badala ya kukazia upatikanaji wa Katiba inayohitajiwa na wananchi,” aliongeza.

Aidha, alisema ucheleweshwaji wa Katiba mpya unaweza kusababisha kama yaliyotokea  Kenya, ambapo maelfu ya watu walipoteza maisha na makazi mwaka 2008.

Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa chuo hicho, Jackson Isdory, alisema ni vyema Bunge hilo likaahirishwa kwa manufaa ya Watanzania kwani kuendelea na mjadala huo bila maridhiano ni kufuja fedha za kodi za wananchi baada ya wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Umoja wa wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udomasa), Paul Loisulie, alisema yeye anaunga mkono hatua hiyo aliyoisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ndiyo msimamo aliokuwa akiufikiria siku zote ambao utasaidia kutoharakisha upatikanaji wa Katiba ambao kwa sasa umeonekana kukwama kwa kukosa maridhiano.

Alisema kuwa dalili zinaonyesha uwezekano wa wajumbe wa Katiba wanaounda Ukawa kurudi haupo na hivyo uwezekano wa kupatikana theluthi mbili haupo pia.

“Kwa sababu Katiba yenye mwafaka haitakuwapo ni bora Bunge Maalum la Katiba liahirishwe ili kuepuka mtego wa kuandika katiba isiyo na mwafaka na kuitisha Bunge la Jamhuri ili waweze kufanya marekebisho ya Katiba ya zamani,” alisema Loisulie.

Kuhusu Rais kutokuwa na mamlaka ya kuvunja Bunge, Mwenyekiti huyo alisema Waswahili husema busara hushinda sheria, kama ilivyokuwa wakati wa Bunge la bajeti busara hiyo itumike kuahirisha hilo Bunge la Katiba maana haliwezi kuendelea bila Ukawa.

Askofu wa Kanisa la PHAM Kanda ya Kati, Julius Bundala, alisema Rais ana mamlaka ya kulivunja Bunge kwa kuwa aliunda kitu ambacho hakina mwisho na kuhoji kuwa kama hana mamlaka kulivunja litavunjwa na nani?.

 “Mimi naona tusomewe ni nani mwenye mamlaka ya kuvunja, maana mimi naona Rais bado ana mamlaka ya kuvunja maana ndiye aliyeliunda,” alisema Askofu Bundala.

PROFESA MKUMBO
Hata hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kishiriki cha Elimu  (Duce), Prof. Kitila Mkumbo, aliungana na wanaotaka Rais Kikwete asitwishwe mzigo unaohusu kuvunja au kusitisha Bunge Maalumu la Katiba, akisema ingawa kisheria Bunge hilo linaweza kusitishwa, lakini mwenye mamlaka hayo ni Bunge hilo lenyewe.

Alisema hata lilipositishwa kupisha Bunge la Bajeti, aliyewezesha hilo ni Kamati ya Uongozi na ile ya Kanuni na Haki za Bunge Maalumu baada ya kuungwa mkono na wajumbe na kwamba, kinyume cha hivyo, hata Rais asingeweza.

Prof. Mkumbo alisema kete ya mwisho iliyobaki ni Ukawa kujipanga kuhakikisha wanaelewesha vizuri wananchi ili waikatae rasimu itakayopendekezwa na Bunge hilo.

Alisema wakishindwa na CCM ikapita kwenye kura ya maoni, hawatakuwa na ujanja kwa kuwa itakuwa imepata uhalali kisheria na kisiasa.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Nchemba, amesema  kama maridhiano kati ya CCM na Ukawa hayatapatikama katika Bunge Maalum la Katiba uwezekano wa kupata Katiba mpya itakuwa ndoto.

Aidha, amesema kama maridhiano hayatafanyika na kushindwa kupatikana theluthi mbili katika Bunge hilo, Watanzania hawatawaelewa wajumbe wa Bunge hilo na itakuwa kazi ngumu kwa CCM wakati wa kura za maoni za kuamua katiba zitakazopigwa na wananchi.

Alisema mataifa mengi yamepata matokeo mabaya (machafuko) kutokana na suala la katiba ambalo  linahitaji maridhiano.

“Hata kama mtu atabeza, Bunge hili la katiba hata likakaa siku 90 halafu likakosa theluthi mbili hakuna Mtanzania atakayefurahia, Taifa letu limeleta umoja, kwa hiyo kuna umuhimu wa kuifanya rekodi ya amani iendelee kudumu nchini,” alisema.

Mwigulu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, alisema wakati wa mikutano ya Bunge Maalum la Katiba, amekuwa akisisitiza kuwa bunge hilo linatakuwa kujiridhisha kama kweli theluthi mbili zitapatikana.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa