Home » » UCHIMBAJI JASI WAWATESA WAZAWA KILWA

UCHIMBAJI JASI WAWATESA WAZAWA KILWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Jasi (Gypsum) ni moja ya madini yanayopatikana nchini, yamekuwa yakitumika zaidi kwa shughuli za ujenzi.
Moja ya maeneo ambayo madini haya yanapatikana ni katika Kijiji cha Makangaga, wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi.
Uchimbaji wa madini hayo katika kijiji hicho ulianza rasmi mwaka 2006 na bado unaendelea.
Hadi sasa kuna kampuni 12 zinazochimba jasi katika kijiji hicho, zikiwamo Go On, Anglo African Gypsum, Tanzania Gypsum, Pita Ludovick, Kimambo , Agnes & Michael , Kwanza Kilwa , Mazongela , Kawina , Ruben Investment na Mdhs Investment zote za Dar es Salaam.
Hata hivyo baadhi ya wananchi wamekuwa wakilalamikia uchimbaji huo kuwa umesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, hasa kwa vyanzo vya mto Makangaga hivyo kuharibu ukuaji na mazalia ya samaki.
Kwa kuzingatia uharibifu huo wa mazingira mwaka 2012 aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alifanya ziara katika Mkoa wa Lindi na kujionea hali hiyo ya uharibifu na kusimamisha uchimbaji hadi wachimbaji wafanye mazungumzo na kijiji.
Hata hivyo hadi sasa wachimbaji wanaendelea na kazi bila suluhu na wanakijiji.
Athari za mazingira na uchumi.
Baadhi ya wananchi wanaoishi katika kijiji hicho wametoa ushuhuda wao wakisema kabla ya uchimbaji huo kulikuwa na maji mengi, sasa mto huo umepungua kwa kiasi kikubwa hivyo kutishia upatikanaji wa maji siku za usoni.
Selemani Lingumbe, Mkazi wa kijiji hicho anasema kuwa hapo awali mto huo ulikuwa na maji mengi.
Lakini siku zinavyozidi kusonga mbele maji yake yamekuwa yakipungua kutokana na baadhi ya kampuni kuchimba madini hayo pembezoni mwa mto huo licha ya kwamba walishalalamikiwa na wanakijiji.
Shughuli za uchimbaji zinafanyika karibu na kuharibu mto huo, pia maji yake huchafuliwa kutokana na ufuaji wa nguo na kuoga.
“Wananchi hao wamekuwa wakifanya vitendo hivyo licha ya kujua kuwa maji hayo yanatumiwa na wakazi wa kijiji hicho chenye jumla ya watu 4245,” anasema Lingumbe na kuongeza:
“Mto huu ni wa muda mrefu na umekuwa chanzo cha maisha yetu na uchumi wetu kwani pamoja na mambo mengine maji ya mto huu tunayatumia kwa kilimo cha umwagiliaji wakati wa kiangazi. Hivyo kupungua kwa maji haya kunaaathiri pia shughuli za kiuchumi. Serikali inapaswa kuwachukulia hatua kali baadhi ya kampuni zinazochimba madini karibu na vyanzo vya mito.”
Naye Mohamed Mnonya (53) anasema: “Sisi wanakijiji cha Makangaga tunashida sana maana hawa wachimbaji hawasikii. Wamekuwa wakiendelea kuchimba madini karibu na mto ambao unazidi kukauka. Serikali inajua hilo lakini haifuatilii kabisa,” anasema na kuongeza:
“Tangu mwaka 2006 wachimbaji hao walipoanza uchimbaji wa madini, tumeshuhudia kupungua kwa maji ya mto na bila hatua yoyote kuchukuliwa na Serikali.”
Kwa upande wake Hamisi Mbegwa ambaye shughuli zake ni kilimo anasema wakati wa kiangazi huwa analima kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia maji ya mto huo. Lakini mazao yake sasa yamepungua kutokana na kushindwa kupata maji ya kutosha kwa ajili ya kilimo chake cha umwagiliaji.
“Nilikuwa nalima ekari tatu za mpunga kipindi cha nyuma na kupata gunia karibu 60 kama nimelima kitaalamu. Lakini kuanzia mwaka 2012, nimelima ekari moja tu na mwaka huu siwezi kulima kwa sababu ya upungufu mkubwa wa maji,” anasema.
Naye Selemani Matajiri, mkazi wa eneo hilo anabainisha kuwa hali ya afya za wananchi wa kijiji hicho zipo hatarini kutokana na wachimbaji hao kujenga vibanda vyao vya kulala karibu na mto;
“hatuvioni vyoo walivyojenga, kitu kinachofanya kuamini wanajisaidia pembeni ya huo mto na kufanya shughuli zingine ikiwamo kufua nguo. Unadhani tutapona na magonjwa? Hapa tutaugua tu hata kama siyo leo(sasa), basi miaka inayokuja maana magonjwa mengine yanachukua muda kujitokeza,” anasema Matajiri.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Makangaga, Muhidin Mkunguru amekiri kuwapo kwa tatizo hilo na kusema mto umepungua kwa kiasi kikubwa.
“Tangu nihamie kijijini hapa mwaka 2011, maji yalikuwa yanafika kiunoni. Lakini sasa maji yanafika chini ya magoti. Maji ya mto huo yanazidi kupungua na ndiyo tegemeo kubwa katika kijiji chetu chenye jumla ya vitongoji vinne vya Makangaga mjini, Mpindiro, Mageuzi na Kikundi,” anasema Mkunguru.
Kuhusu suala la kilimo, Mkunguru anasema katika kijiji hicho chenye wakazi wapatao 4245, wanalima mpunga, ufuta na mahindi. Na wakati wa kiangazi, wanajihusisha na kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia huo mto na hupanda tena mpunga na kulima bustani za nyanya.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Makangaga, Zainabu Mcheni anasema ni kweli watu hao wameharibu sana mto na kwamba licha ya Serikali kupata taarifa juu ya uharibifu huo, bado imekaa kimya hata baada ya kuwaamuru wachimbaji hao kuacha kuchimba karibu na mto Septemba 26, mwaka jana
“Kwa kweli maji yamepungua na kampuni hizi hazina ushirikiano kabisa na sisi. Wanachukua mali hapa kwetu kijijini lakini sisi wenyewe hawatupendi maana wanajua wanaharibu mto ambao ndiyo tegemeo letu,” anasema na kuongeza:
“Tunalia na Serikali kwa nini imekaa kimya kiasi hiki. Viongozi wa vijiji tunapata shida kutokana na kuulizwa mara kwa na wananchi juu ya hatma ya tatizo hili. Wananchi wanatuona kama hatufanyi kazi. Sisi tutafanya nini huku chini wakati Serikali iko kimya,” anasema Zainabu.
Kaimu Mganga wa Afya wa Zahanati ya kijiji cha Makangaga, Hamisi Kachwichwi anasema ni kweli mto umeharibiwa lakini hadi sasa bado zahanati yake haijapokea wagonjwa walioathirika kutokana na matumizi ya maji yaliyoharibiwa na shughuli za uchimbaji wa madini.
Naye Kaimu Ofisa Mazingira wa Wilaya ya Kilwa, Raymond Cholobi hakuwa tayari kuzungumzia utoaji wa cheti cha mazingira akidai kuwa hana mamlaka.
Kamishna wa Madini Kanda ya Kusini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka anasema kuwa bado hajapata taarifa za kuhusu mradi huo.
“Suala hili bado halijaletwa hapa ofisini kwangu. Halijafika bado, sijaliona wala kulisikia hivyo nawashauri wakazi wa kijiji hicho kuleta taarifa hiyo ofisini kwangu ili hatua za haraka zichukuliwe,” anasema Mchawampaka.
Kwa upande wa Ofisa Misitu na Mazingira mkoani Lindi, Zawadi Jilala amekiri kuwapo kwa uharibifu wa mazingira katika eneo hilo na kwamba sheria ya mazingira imekiukwa:
“Sheria ya mazingira ya 2004 (Environmental Management Act, 2004) inatamka wazi kuwa shughuli zozote za kibinadamu zifanyike nje ya mita 60 toka kwenye chanzo cha maji. Ukiwa kama mto, visima, bwawa, hao wamekiuka hiyo sheria, nashangaa uongozi wa Serikali ya kijiji upo kimya kiasi hicho, wakati wanajua hilo ni tatizo kubwa litakalo waathiri hapo baadaye,” alisema Jilala.
Mratibu wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania- Mjumita- Akrei Arbat anasema licha ya kutokufika katika eneo hilo, ameshasikia malalamiko ya wananchi na viongozi wa halmashauri wakilizungumzia.
“Wamekiuka sheria ya mazingira ya 2004 kwa makusudi.”
Anasema ingekuwa jamii tungesema haina uelewa, sasa hao wasomi kabisa watakuwa ni wajeuri tu, lakini Serikali iwaondoe maana huo mto ukikauka itakua shida kwa wakazi wa kijiji hicho,” anasema Akrei.
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Abdallah Ulega amekiri kuwapo kwa tatizo hilo katika Kijiji cha Makangaga la kuharibu mto unaofanywa na wachimbaji wa madini ya jasi.
 “Nimewahi kuzungumza nao, nitakwenda kuzungumza nao tena ili waweze kuondoka na kama watakaidi itabidi tutumie nguvu,” anasema na kuongeza “Cha msingi mimi nashauri hizo mamlaka za juu ziingilie kati suala hilo kwa nguvu”.
chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa