Home » » MBOWE:MOTO WA KUDAI KATIBA MPYA HAUTAZIMIKA

MBOWE:MOTO WA KUDAI KATIBA MPYA HAUTAZIMIKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mwenyekiti wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe
 
Mwenyekiti wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe, amesema moto wa kudai Katiba mpya hautazimwa, kwani kitakachotokana na vikao vya Bunge hilo vinavyoendelea mjini
DODOMA BATILI
Mbowe aliyasema hayo jana katika mazungumzo maalumu na NIPASHE kuhusu mwitikio wa wito wa Ukawa kwa Rais Jakaya Kikwete, kusitisha Bunge hilo mpaka utakapopatikana mwafaka kati ya makundi mawili yaliyotokana nalo kugawanyika.

“Hoja ya msingi ni kwamba, vikao vinavyoendela Dodoma ni batili. Viko kinyume cha mchakato ulioasisiwa kwa misingi ya shirikishi na vinaakisi ubabe, dharau na kejeli za viongozi kwa Watanzania,” alisema.

Pamoja na kufananisha mikutano hiyo na michezo ya kitoto ya kujitekenya na kucheka wenyewe, Mbowe alisema ikifanikiwa kupata Rasimu ya Katiba itakayopendekezwa kuwa Katiba na hata ikipitishwa kwa kura ya maoni kuwa katiba mpya, wao wataendelea kudai katiba bora.

Mbowe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, alisema siyo rahisi kuaminisha umma wa Watanzania kuwa waliobaki Dodoma wana uchungu na nia ya kulipatia taifa katiba mpya kwa sababu kiini cha mchakato huo ni harakati za vyama vya upinzani, ambazo zilibezwa na bado zinabezwa na wana CCM.

Alisema kinachowatia kiwewe wanaoendelea na vikao vya Bunge hilo ni posho wanazopata kila siku, kwa sababu katiba mpya kwa Tanzania siyo ajenda yao wala utashi wa Rais Kikwete, bali ni matakwa ya taifa.

“Wameng’ang’ana kubaki kwenye vikao huku wakifahamu wazi hakuna kitakachopatikana na hata kikilazimishwa kupatikana, hakitakuwa na tija iliyodhamiriwa. Watafsiriweje kama siyo wafujaji wa mali za umma? Wana kiwewe cha posho ya 300,000 kwa siku tu,” alisema Mbowe.

KUHUSU KAULI YA JAJI WEREMA
Kuhusu mpango mbadala uliyoelezwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, kwamba endapo itashindikana kupata katiba mpya, Katiba ya sasa (ya mwaka 1977) itarekebishwa kwa awamu ya 15 ili ikidhi mahitaji ya uchaguzi mkuu ujao, Mbowe aliunga mkono.

Mbowe alisema hayo ni miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema hiyo ililenga kuepusha Bunge Maalumu la Katiba kuendelea kukutana Dodoma ilhali ikifahamika wazi haliwezi kupata katiba mpya na iliyo bora katika muda huu.

“Kujadili na kufanyia marekebisho katiba iliyopo ili tupite salama katika uchaguzi mkuu ujao, ni hoja ya msingi na ndivyo tumekuwa tukipendekeza,” alisema.

Alisema alichoeleza Jaji Werema hakitofautiani sana na pendekezo lililotolewa bungeni na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Mwigulu

Nchemba, siku ya kwanza ya Bunge hilo, kukutana bungeni.Alisema mpango ulioelezewa na Jaji Werema juzi wakati akijibu swali la wamejipanga vipi ikiwa katiba mpya haitapatikana kama inavyokusudiwa, ni ishara kuwa hata kama wanakataa kukiri hadharani kuwa uwezekano wa kufikia lengo ni mdogo, wanafahamu ukweli huo.

Mbowe alisema wenye akili na walio makini kama Nchemba, ambaye ni Naibu Waziri wa Fedha, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Jaji Werema na Rais Kikwete wanaelewa na kwa namna tofauti wameonekana kukiri ukweli huo, tofauti na baadhi (hakutaja jina la mtu) wanaoona ukuta wenye rangi ya bluu, wanang’ang’ana kusema ni wenye rangi nyekundu.

KUHUSU MAANDAMANO YA UKAWA NCHI NZIMA
Ukawa walipotaka Rais asitishe Bunge Maalumu la Katiba, waliahidi kuandamana nchi nzima ikiwa matakwa yao, likiwamo hilo hayatatekelezwa na sasa baada ya Ikulu na kisha Jaji Werema kueleza bayana kuwa Rais hana uwezo wa kisheria kuvunja au kusitisha Bunge hilo, Mbowe alisema jambo hilo kwa sasa linajadiliwa.

“Kuhusu kutoandamana au kuandamana, lini na vipi ni suala, ambalo linashughulikiwa na vikao vya ndani, naamini uamuzi ukifikiwa litatolewa ufafanuzi,” alisema Mbowe.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa