Home » » WANAWAKE WACHARUKA WENZAO KUUAWA

WANAWAKE WACHARUKA WENZAO KUUAWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Rais Jakaya Kikwete
 
Wanawake wa Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi, wamemuomba Rais Jakaya Kikwete kumuondoa wilayani humo Mkuu wao wa wilaya, Regina Chonjo, kwa madai kwamba, hana ushirikiano mzuri hasa kwa wanawake na kutoa lugha za kuwadhalilisha.
Aidha, wamesema Mkuu huyo wa wilaya ameshindwa kudhibiti vitendo vya kinyama wanavyofanyiwa wanawake wilayani humo, ikiwamo kubakwa na kuuawa, badala yake amekuwa akiwatolea maneno ya kwakejekeli kuhusiana na vitendo hivyo.

Wanawake hao, wakiwamo vijana na watu wazima walipaza sauti zao juzi, wakati wa kikao cha pamoja kati yao na Kamanda wa Polisi Mkoani Lindi, Renata Mzinga, kilichofanyika mjini hapa.

Kikao hicho ambacho mkuu huyo wa wilaya hakuhudhuria, kiliitishwa na Kamanda Mzinga kwa lengo la kujadili vitendo vya mauaji ya wanawake vinavyoendelea kufanyika wilayani humo.

Baadhi ya wanawake hao wakizungumza mbele ya Kamanda huyo wa polisi, Sauda Kaisi, Aisha Hamisi, Magreth Joseph na Fatuma Umbili, kwa nyakati tofauti walisema tangu mauaji hayo yaanze kutokea wilayani humo mwishoni mwa mwaka jana hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya watuhumiwa.

Walisema licha ya kukithiri kwa vitendo hivyo, Mkuu huyo wa wilaya akiwa ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya, ameshindwa kusimamia na kudhibiti matukio hayo wakati vyombo vya ulinzi na usalama wilaya vikiwa chini yake.

“Mama Kamanda, tangu mauaji haya yaanze kufanyika mwaka jana hadi leo, kiongozi huyu (mkuu wa wilaya) akiwa ni mwanamke mwenzetu, hajawahi kuitisha kikao na sisi ili kujadili tatizo hili. Badala yake amekuwa akitukebehi eti mauaji hayo yanatokana na umalaya,” alidai Kaisi.

Alidai tangu kuanza kwa vitendo vya mauaji mwishoni mwa mwaka jana, Mkuu huyo wa wilaya alifanya mkutano mmoja tu.

Kaisi alidai katika mkutano huo, Mkuu huyo wa wilaya alitoa kauli za kejeli dhidi yao, ikiwa ni pamoja na kueleza kuwa mauaji hayo yanachangiwa zaidi na kukithiri kwa vitendo vya umalaya.

Kamanda wa Polisi Mkoani Lindi, Mzinga, akijibu malalamiko hayo,  aliwaeleza wanawake hao kwamba, yeye hana uwezo wa kumchukulia hatua mkuu wa wilaya, kwani hayupo chini ya mamlaka yake.

“Kwa hili la Mkuu wa wilaya, akina mama wenzangu sina uwezo nalo, kwani hayupo chini yangu, yupo kwenye mamlaka nyingine,” alisema Kamanda Mzinga.

Hata hivyo, aliwataka wanawake wa wilaya hiyo na mkoa kwa jumla kushirikiana na Jeshi la Polisi kutokemeza mauaji hao, ikiwamo kusaidia kufichua vitendo vya kihalifu.

NIPASHE iliwasiliana na Mkuu huyo wa wilaya, Chonjo, kuhusiana na madai ya wanawake hao, lakini akasema hawezi kuzungumza jambo lolote, kwani hakuwapo kwenye mkutano huo.

“Ndugu yangu mwandishi, mimi sijakuwapo kwenye kikao hicho. Hivyo, wala sielewi kilichozungumzwa. Ndiyo kwanza nakusikia wewe. Hivyo, sitaweza kukupa coment (kusema) yeyote,” alisema Chonjo.

Wilaya ya Nachingwea na mkoa wa Lindi kwa ujumla umekumbwa na matukio mengi ya mauaji ya wanawake, kubakwa na kufanyiwa vitendo vingine vya kikatili, huku wananchi hasa wanawake wakilalamika kuwa hakuna jitihada za dhati zinazofanywa kukomesha matukio hayo ikiwamo kuwatia mbaroni wanaohusika ili sheria ichukue mkondo wake.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa