Home » » WANASIASA LAWAMANI KUKWAMA BUNGE LA KATIBA

WANASIASA LAWAMANI KUKWAMA BUNGE LA KATIBA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Wajumbe wa Bunge la katiba wakiwa katika bunge la katiba.Picha Maktaba.
 
Baadhi ya wakazi wilayani Ruangwa, mkoa wa Lindi, wamewalaumu wanasiasa waliomo katika Bunge la Maalum la Katiba kuwa ndiyo chanzo cha kuvurugika kwa Bunge hilo kwa kuweka mbele maslahi yao ya kisiasa badala ya maslahi mapana ya wananchi na taifa.
Aidha, wamewaomba wajumbe wa Bunge hilo wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kurejea kwenye mjadala Bunge hilo litakapoanza tena vikao vyake Agosti tano mwaka huu, ili Tanzania iweze kupata Katiba mpya.

Wito huo ulitolewa na wananchi hao wakiwamo viongozi wa asasi za kiraia wilayani Ruangwa, kwenye mafunzo kwa makundi maalumu kuhusu mchakato wa Katiba mpya, yaliyoendeshwa na Mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali ya wilaya humo (Mmakiru).

Akizungumza kwenye mafunzo hayo, Katibu  wa asasi ya Rosari, Shakila Ndembo, aliwataka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutotanguliza mbele maslahi ya kisiasa katika kujadili suala hilo muhimu kwa wananchi na taifa.

Alisema licha ya kuwa uamuzi wa wa mwisho wa kupatikana kwa Katiba mpya upo mikononi mwa wananchi, lakini wapo wanasiasa wanaotaka kuhodhi jambo hilo kwa kujilimbikizia mamlaka ya maamuzi.

“Upo umuhimu wa wajumbe wa Bunge la katiba kubadilisha mitizamo yao na kuchukulia suala la katiba mpya kwa mitizamo ya kujali wananchi na si kulinda maslahi yao ya kisiasa” alisema Shakila.

Hata hivyo, aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupigia kura Rasimu itakayowasilishwa baada ya kupitishwa na Bunge hilo kuikataa kama haina maslahi ya umma na kuikubali kama itakuwa imebeba maslahi ya umma na taifa kwani wao ndio wenye uamuzi wa mwisho badala ya kuwaachia wanansiasa ambao wanaweka zaidi maslahi yao ya kisiasa.

Naye Mwenyekiti wa kikundi cha Shukrani cha kijiji cha Namichiga, Crecencia Tindwa, alisema awali mchakato wa Katiba ulienda vizuri ambapo wananchi kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba walipata fursa ya kutoa maoni yao, lakini ilipofikia hatua ya Bunge la Katiba hali imebadilika na kuwa jukwaa la kisiasa kwa malumbano yasiyo na maslahi ya wananchi kutawala.

“Mchakato uendelee si kwa vyama vya siasa kumiliki mchakato mzima kwani licha ya  muungano kuna mambo mengi yanayogusa maisha ya watu yanahitaji kupitiwa” alisema Tindwa.

 Aliwataka Ukawa wakubali  kukaa na serikali na kumaliza tofauti zao ili ipatikane Katiba yenye kujali maslahi ya Watanzania na kama kuna muafaka hautapatikana suala na muundo wa serikali lirudishwe kwa wananchi waamue ni mfumo gani wanautaka kupitia kura ya maoni.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa