Home » » SALAMA KIKWETE AWATAKA WANAWAKE KUCHANGAMKIA MKOPO

SALAMA KIKWETE AWATAKA WANAWAKE KUCHANGAMKIA MKOPO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama), Salma Kikwete
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama), Salma Kikwete na wa Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF), Anna Mkapa, wemewataka wanawake nchini kuchangamkia mkopo wa viwanja unaotolewa kwao na Benki ya Wanawake Tanzania (TWB).
Walitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakati wakiipongeza benki hiyo kwa kuanzisha mradi wa kukopesha wanawake nchini viwanja.

Salma, ambaye pia ni mke wa Rais Jakaya Kikwete, na Anna wa Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, walitoa pongezi hizo jana walipotembelea banda la Wama kwenye viwanja vya Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya 38 ya Dar es Salaam, maarufu kama Sabasaba iliyomo benki hiyo. Maonyesho hayo yalifikia kilele chake jana.

Walisema uamuzi wa benki hiyo utawasaidia kupata mikopo kwenye benki na taasisi hizo kwa kutumia hati za viwanja hivyo kama dhamana na kwamba, umekuja wakati mwafaka, ambao wanawake wengi wamejikita katika shughuli za uzalishaji mali na kuanzisha miradi ya ujasiriamali.

Anna, ambaye aliambatana na Salma wakati akitembelea banda hilo, aliwashauri wanawake zaidi kujiunga na benki hiyo ili wanufaike na mradi huo na kutumia hati hizo kupata mikopo.

“Siku zote wanawake wamekuwa walipaji wazuri wa mikopo kwenye benki kuliko wanaume,” alisema Anna. Salma aliipongeza benki hiyo akisema imeonyesha jinsi gani inawajali wanawake na kwamba, mikopo ya viwanja hivyo itaboresha maisha yao kutokana na kuboresha miradi yao ya maendeleo.

Alisema wanawake wengi walikuwa hawakopesheki kwa kushindwa kutimiza masharti magumu ya benki kwa kukosa hati za viwanja kutokana na kujenga nyumba kwenye maeneo ambayo hayajapimwa.

Mkurugenzi wa Benki hiyo, Magreth Chacha, alisema wamebuni mradi huo ili kuwainua wanawake kiuchumi na kuwarahisishia kupata mikopo benki kwa kutumia hati hizo.

Alisema benki hiyo imeweka utaratibu kwa kila mwanamke kuweka asilimia 30 ya gharama ya kiwanja kwenye benki hiyo na nyingine asilimia 70 itawalipia.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa