Home » » CHADEMA,MSAJILI JINO KWA JINO

CHADEMA,MSAJILI JINO KWA JINO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Chadema, John Mnyika
Chama cha Demokrasia na Maedneleo (Chadema) kimemjia juu Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kwa madai kwamba anatumika kisiasa kukivuruga chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Chadema, John Mnyika, alisema Chadema ni chama kinachoongozwa kwa katiba na maamuzi ya wanachama na siyo kauli potofu za Msajili au naibu wake.

Alisema Msajili anatumia katiba ya mwaka 2004, ambayo ilishafanyiwa marekebisho mwaka 2006 na kuwasilishwa kwenye ofisi yake ilipokuwa ikisimamiwa na John Tendwa.

Kauli ya Mnyika imekuja siku chache, baada ya Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, kusema wanaitambua katiba ya Chadema inayoeleza ukomo wa uongozi kuwa ni vipindi viwili na ambayo kutokana na kauli hiyo, Mwenyekiti wa sasa, Freeman Mbowe, na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, hawana sifa ya kugombea nafasi hizo tena.

“Tunamtaka Msajili aache kuingilia mambo ya ndani ya chama yanayofanywa kwa mujibu wa sheria. Wasaliti na mamluki wanatumiwa na CCM. Tunaelewa njama zilizopo nyuma ya pazia. Na tuna hakika zitashindwa kwa kuwa Chadema imejipanga,” alisema.

Mnyika alisema katiba ya Chadema toleo la mwaka 2006, Ibara ya 6 kifungu cha 3 kifungu kidogo cha pili, inasema kiongozi aliyemaliza muda wa uongozi ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena mradi awe anatimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa kiongozi.

Alisema Msajili hana uwezo wa kumzuia Mbowe, Dk. Slaa au mwanachama yoyote kugombea, bali mwenye uwezo wa kuzuia ni katiba na maamuzi ya mkutano mkuu kupitia vikao halali vya chama.

“Katiba ya Chadema ndiyo inayotuongoza. Imepitishwa na mkutano mkuu wa chama…Msajili anaposema tuitishe mkutano mkuu tufanye marekebisho, anataka kutupotezea muda wetu,” alisema Mnyika ambaye pia ni mjumbe wa sekretarieti ya Chadema.

UCHAGUZI MKUU SEPTEMBA
Mnyika, ambaye pia alikuwa Katibu wa kamati iliyohusika na kuandika katiba mpya ya Chadema chini ya marekebisho makubwa mwaka 2006, alisema uchaguzi mkuu wa viongozi wa kitaifa utafanyika Septemba, mwaka huu, baada ya kumaliza ngazi zote za chini.

Alisema uchaguzi huo unafanyika kwa mujibu wa ratiba na siyo kwa sababu ya kauli za Msajili, bali kwa matakwa ya wananchama na vikao vya chama, kama yapo marekebisho yataletwa na wanachama kwenye mkutano mkuu.

“Mkutano mkuu wa Agosti 13, mwaka 2006, walipopitisha kifungu kicho cha muda wa uongozi, mchakato ulianza mapema 2006. Tulipeleka waraka mikoani kutafuta maoni ya wanachama,” alisema.

Alisema kati ya maeneo yaliyotolewa maoni ni kifungu cha ukomo wa uongozi kilichokuwapo kwenye katiba ya mwaka 2004.

Mnyika alisema wanachama wengi walipendekeza kuondolewa kwa kifungu hicho kwa kuwa hakina sababu ya kuwapo na kwamba, haikuwa mawazo ya Mbowe au Dk. Slaa.

Alisema kwa mujibu wa katiba ya Chadema, kabla ya mkutano mkuu kunakuwa na vikao vya kamati kuu na baraza kuu na kwamba, maoni ya marekebisho ya katiba yalipitia hatua hiyo.

“Kwenye masuala, ambayo wanachama hawakutofautiana maoni au hayakuwa na ubishani, yaliandaliwa taarifa, ambayo iliingizwa kwenye mkutano mkuu wa chama kwa ajili ya kuridhiwa na mkutano mkuu, ambao ulifanya hivyo,” alisema.

Alisema mojawapo ya vifungu vilivyoridhiwa ni ukomo wa uongozi na kwamba, hakukuwa na utata wala ubishi, maoni yalipitishwa.
Mnyika alisema maoni yenye mjadala au ubishani yalijadiliwa na kupitishwa, hivyo msajili anapoitambua katiba ya mwaka 2004, anafanya makosa makubwa.

Alisema msajili wa vyama vya siasa kwa wakati huo, Tendwa aliwapongeza kwa mabadiliko makubwa ya katiba na walijaza fomu za kisheria kwenye ofisi ya msajili na kuambatanisha marekebisho Lakini kwa kuwa katiba yote ilifumuliwa, waliambatanisha na katiba husika.

“Yale tuliyorekebisha, yaliwekwa kwa kuwa yalikuwa mengi. Tuliambatanisha katiba mpya na msajili wa wakati huo alijibu kupokea na kutambua marekebisho aliyopata na chama kikaanza kutumia katiba mpya,” alisema.

Alisema uchaguzi mkuu wa mwaka 2009, ilitumika kwa uchaguzi wa ndani ya chama katika ngazi zote na wanachama waliokuwa wamemaliza vipindi viwili, waligombea bila kipingamizi chochote.

Mnyika alisema uchaguzi huo ulifanyika kwa amani na hakukuwa na hoja za katiba kuchakachuliwa na kwamba, zimeibuka hivi sasa kutokana na kuwapo kikundi cha watu kinachoshirikiana na CCM kuihujumu Chadema.

“Kitendo cha mjadala huu kuibuka sasa inakumbusha msemo wa mpige mchungaji na kondoo watatawanyika...wanamshambulia mwenyekiti wetu ili chama kisambaratike. Lakini hawatatuweza,” alisema.

Alisema kauli za viongozi, ambao walitaka Chadema iparaganyike mwaka 2013, ziligonga mwamba, wakaandaa mkakati wa mabadiliko wa usaliti na mamluki, lakini chama kilichukua hatua na kuvuka salama.

Mnyika alisema mwaka 2014 kwa mkakati uleule wa usaliti na mamluki, ukazuka mkakati wa kuwachafua viongozi wa chama kwenye mitandao ya kijamii kuwa hawana sifa za kugombea na hesabu za chama.

Alisema katika hilo, wamevuka salama na watashinda, kwani hadi sasa wamemtaka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuweka bayana mahesabu ya vyama vya siasa.

“Wameshindwa kuvuruga Chadema kwa kauli za propaganda, kugombea. Sasa wanamtumia msajili kuwa viongozi wetu hawana sifa za kugombea,” alisema Mnyika.

Alisema mwanachama yoyote anaruhusiwa kugombea alimradi afuate matakwa ya katiba na kwamba, maamuzi yapo mikononi mwa wananchama, ndiyo wataamua nani anastahili kuchaguliwa na kwamba, kwa sasa hawawezi kusema nani atagombea.

WATISHIA KUTANGAZA MGOGORO NA MSAJILI
Mnyika, ambaye pia mjumbe wa mkutano mkuu, alisema wanamtaka Msajili Jaji Francis Mutungi, kujitokeza na kuthibitisha kama kauli za naibu wake, ndiyo kauli na msimamo wa ofisi yake.

Alisema vinginevyo watatangaza mgogoro na msajili kwa kuwa amekubali ofisi yake kutumiwa kisiasa na mamluki kuivuruga Chadema.

Mwaka 2012, Chadema ilitangaza kususia shughuli zote za msajili wa vyama vya siasa wakati huo, Tendwa, kwa madai ya mfufulizo wa matukio ya kuzuia mikutano ya operesheni ya M4C kwa kisingizo cha sensa ya watu na makazi, kuhusisha Chadema na matukio ya ugaidi na kuzuia kuimarisha kikosi cha Red Bridged, huku CCM ikiachwa kuendelea kuimarisha kikundi cha Blue Guard.

Alisema wanashangazwa na kauli za naibu msajili kuwa viongozi wa Chadema wanatakiwa kuchaguliwa kabla ya Januari, mwakani, jambo ambalo linatoa tafsiri kuwa Chadema haitaki kufanya uchaguzi wake, hivyo anaishurutisha.

Mnyika alisema uchaguzi wa ndani ya chama ulishaanza na kwa mujibu wa katiba haiwezekani kwenda kwenye uchaguzi mkuu kabla ya kuwa na asilimia 50 ya viongozi wa ngazi za chini.

Alisema Chadema inafanya uchaguzi makini kwa lengo la kuimarisha mtandao thabiti wa chama, ambao ndiyo mtaji katika kuiondoa CCM.

Alisema Julai 18 na 19, kamati kuu ya chama itakutana na kwamba, Agosti, mwaka huu, utafanyika uchaguzi wa viongozi wa majimbo, wilaya na mkoa.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa