Home » » TAKUKURU YAWABURUZA KORTIN VIONGOZI WA CHAMA CHA USHIRIKA,SACCOS

TAKUKURU YAWABURUZA KORTIN VIONGOZI WA CHAMA CHA USHIRIKA,SACCOS

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Nachingwea, Mkoani Lindi, imewakamata na kuwafikisha mahakamani viongozi watano wa Chama cha Ushirika na Msingi na Chama cha Akiba na Mikopo (Saccos) Kata ya Naipanga, wilayani humo, kwa tuhuma za kuvisababishia hasara ya Sh. 21,978,600.
Viongozi hao ni Diwani wa kata hiyo kupitia CCM, Rashid Issa Chitawala, Katibu wa Chama cha Akiba na Mikopo cha Nandoo Saccos, Simon Phidolini Makwinya na Mhasibu wa chama hicho, Zuhura Mchichira.

Wengine Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Msingi cha Naipanga, Salum Hamisi Tewa na Mhasibu wake Suwedi Kateru, ambao wote wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nachingwea Juni 30 mwaka huu.

Chitawala amekuwa Diwani wa pili wa CCM wilayani Nachingwea kufikishwa mahakamani na Takukuru wilayani humo. Akisoma hati ya mashitaka manne mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Cosmas Hemela, Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Dismas Muganyizi, alidai washitakiwa hao walitenda makosa hayo Januari na Julai 31, 2011.

Alidai kuwa, Chitawala, Makwinya na Mchichjira wakiwa kwenye ofisi za Nando Saccos, huku wakijua wanachokifanya ni kosa, walitumia nyaraka ya benki (Bank Statement) iliyosheheni uongo kuhusu shughuli za mwajiri wao, wakiainisha kupokelewa Sh.10,992,600 kutoka mfuko wa mikopo ya wajasiliamali wadogo, jambo ambalo halikuwa la kweli.

Katika kosa la pili, Mwendesha Mashitaka huyo alidai kuwa, wakiwa ni viongozi washitakiwa walitumia vibaya mamlaka waliyopewa kwa kutoa Sh.10,985,750 kupitia akaunti namba 7042300456 katika benki ya NMB tawi la wilaya ya Nachingwea, hivyo kujipatia manufaa yasiyo halali.

Alidai kosa la tatu, linawahusu washitakiwa Salum Tewa na Suwedi Kateru, ambao wanadaiwa kutumia vibaya mamlaka waliyonayo, kwani Januari 10, 2011, katika benki ya NMB tawi la Nachingwea, wakiwa ni waajiliwa wa Chama cha Ushirika cha Msingi cha Naipanga Amcos, walichukuwa Sh. 10,992,900 kutoka akaunti namba 7046600203 na kuziweka akaunti namba 704300456 inayomilikiwa na Chama cha Nando Saccos, hivyo kukipatia manufaa yasiyo halali.

Kosa la nne linawahusu washitakiwa Chitawala, Makwinya na Mchichira wa Chama cha Akiba na Mikopo cha Nando Saccos, Muganyizi, ambao wanadaiwa kuwa, kati ya Januari Mosi na Julai 31, 2011, wakijua wanachokifanya ni kosa, walifuja na kutapakanya Sh. 10,992,900, mali ya Chama Nando Saccos.

Washitakiwa wote walikana mashitaka waliyosomewa na kupelekwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kutakiwa kuwa na fedha taslimu Sh. milioni tano kila mmoja, na kesi yao namba 02/2014 itafikishwa tena mahakamani hapo Julai 14, mwaka huu.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa