Home » » ''POWERTILLER' SASA ZABEBA MAHARUSI

''POWERTILLER' SASA ZABEBA MAHARUSI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Trekta dogo (Powertiller) likitumika kubeba abiria

Kwa mara nyingine, jitihada za Serikali kuboresha sekta ya kilimo nchini zinaelekea kugonga mwamba baada ya sera na mpango wake kupitia ununuzi wa treka kubwa na ndogo(powertiller), kutumika kwa matumizi mengine ikiwamo kubebea maharusi.
Kushindwa kufanikiwa kwa mradi huo ulioigharimu Serikali mabilioni ya shilingi, utaiacha pia katika madeni kutokana na kuyaingiza nchini kutoka nje ya nchi ikiwamo India kwa mikopo nafuu, kisha uuzaji wake kubinafsishwa na kuwanufaisha wachache.
Uchunguzi wa gazeti hili katika mikoa mbalimbali nchini umebaini trekta hizo kushindwa kutimiza kilichokusudiwa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ugumu wa ardhi katika baadhi ya maeneo na ubovu wa trekta zenyewe.
Mwaka 2009 Serikali iliagiza trekta 10,000 kutoka nchini India kwa lengo la kuwezesha utekelezaji wa mkakati wa Kilimo Kwanza uliotarajiwa kuongeza uzalishaji katika kilimo kinachotajwa kuajiri wastani wa asilimia 80 ya Watanzania.
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, Nurudin Babu, anakiri tatizo hilo, ambapo alikwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa siyo kubeba mizigo pekee bali hali ilikuwa mbaya sana kwani walikuwa wanabebea abiria na harusi.
Anafafanua kuwa alitoa agizo kuwa atakayekutwa amebeba abiria au mizigo isiyo ya kilimo achukuliwe hatua, kwa kuwa hilo ni kosa na ikiwezekana apelekwe mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
“Ni kosa, tena nimelipiga vita sana na nimeshatoa agizo kwa Polisi wakimkamata mtu anayeendelea kubeba abiria, mizigo na hata sherehe, ziwe harusi, ubatizo, kipaimara na nyinginezo kuwachukulia hatua wote, waliobebwa na aliyebeba kwa kuwa wote wana makosa na wanajua kufanya hivyo ni kosa, ”anasema Babu.
Ofisa Kilimo
Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Bariadi mkoani Simiyu, Golonya Ally anasema kuwa katika halmashauri yake kuna trekta 34, tatu zikiwa za mradi, moja la mtu binafsi na 29 ni ya vikundi mbalimbali.
Anakiri kuwa trekta hizo pia hubebea wagonjwa, wajawazito, harusi na hata kutumika kwa safari mbalimbali za kawaida au kwenye starehe.
Anaeleza kuwa hali hiyo inatokana na miundombinu ya usafiri kukosa uhakika, huku trekta hizo yakiweza kupita maeneo ambayo hata baiskeli ni vigumu kupita na kwamba umbali na hospitali na maeneo wanayoweza kupata bidhaa muhimu, ndiyo huwalazimisha kutumia trekta hizo.
“Mkuu wa Wilaya, hataki watu watumie trekta kwa shughuli tofauti na kilimo, lakini kuna wagonjwa, wajawazito, harusi na hakuna jinsi ya kupata usafiri mwingine wa haraka, zaidi ya trekta hivyo inakuwa vigumu kuwazuia, ingawa tunajaribu kutoa elimu, ” anasema Golonya.
Anaeleza kuwa kwa sasa wanafanya mikutano mbalimbali na mradi wa DASIP ‘District Agricultural Sector Investment Project’ (DASIP) ili kuwapa wananchi elimu juu ya matumizi bora ya trekta hizo.
Gazeti hili lilizungumza na baadhi ya wakulima, wadau wa kilimo, wataalamu na viongozi mbalimbali, walioeleza sababu za kubadili matumizi ya trekta hizo wakisema yamegeuzwa magari ya abiria, badala ya kulimia kwa lengo la kutafuta pesa za marejesho ya mikopo iliyo na riba kubwa.
Julius Kapama Mkazi wa Urambo mkoani Tabora anasema kuwa, aliposikia habari za mikopo ya powertiller alifurahi, kwa kuwa alijua atapata mazao mengi, lakini kwa bahati mbaya hali haikuwa hivyo kutokana na mvua hafifu na zisizokuwa na mpangilio.
“Wakati napambana na adha ya kukosa mazao kwa kiasi nilichokusudia, lakini mkopo wa trekta unanisubiri, kama unavyofahamu mikopo mingi kwa watu maskini kama sisi ilivyo na riba kubwa, ”anasema Kapama.
Kapama aliongeza kuwa licha ya riba kubwa inayomsumbua, lakini ubovu wa mara kwa mara ya trekta lake ndiyo uliomfanya atafute njia mbadala ya kupata fedha zaidi, hivyo kubebea kitu chochote akipata mtu anayetaka kufanyiwa hivyo, ikiwamo abiria, hasa siku za mnada.
“Nikibeba abiria, mizigo napata fedha ya marejesho ya mkopo na matengenezo, kwa kuwa limekuwa likiharibika mara kwa mara. Kwa kulitumia kwa kilimo pekee linanifilisi, badala ya kunitajirisha kama nilivyofikiria awali nilipowaza kukopa,” anasema Kapama.
Abduel Hanzuruni wa anayeishi Kijiji cha Kakola Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, anasema kuwa, wakati wa kiangazi hutafuta riziki kwa kutumia trekta hilo, kwa kuwa hana sababu ya kuliweka ndani wakati linahitaji matengenezo.
Anasema kuwa trekta hilo limekuwa likimgharimu mara kwa mara kwa kulipeleka kwenye matengenezo, jambo linalomlazimu kutafuta namna ya kumudu gharama hizo ili unapofika wakati wa masika liwe zima na kufanya kazi za kilimo kama kawaida.
Anasema kwamba haoni ubaya kulitumia kwa kazi nyingine kwa kuwa kipindi hicho kunakuwa hakuna kilimo, ambacho hata hivyo katika miaka ya karibuni hakina tija, kutokana na mvua kupoteza mwelekeo.
“Hali halisi ya vijijini unaijua, hakuna usafiri wa uhakika na mimi nina trekta ninaloweza kubebea abiria, pia nikalimia tena wakati wa kilimo ukifika, kwa nini nisifanye hivyo, ”anasema Hanzuruni akihoji.
Mohamed Bakari Mkazi wa Kijiji cha Ntomoko, Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, anasema kuwa anatumia trekta lake kubebea maji kutokana na uhaba wa maji kijijini hapo.
Anafafanua kuwa hakuna asiyefahamu uhaba wa maji katika kijiji hicho. Hivyo hulazimika kutumia usafiri huo kufuata maji yanapopatikana, hatimaye sasa umekuwa mradi wake kutokana na wanakijiji kumlipa fedha, ili awaletee maji.
“Maisha ni magumu, kama napata fedha kwa kutumia trekta hili lililonihenyesha kulipa, kwa nini nisilifanyie kazi ya ziada kama hii ya kuchotea maji? Kwa namna moja ama nyingine limekuwa ni msaada pekee kwa wanakijiji, ”anasema Bakari.
Hata hivyo, naye alilalamikia ubovu wa matrekta hayo kwa madai kuwa, kuna baadhi ya vifaa ni rahisi kuvunjika.
Anafafanua kuwa, hata alipokuwa akilitumia kwa kazi za kilimo, bado alilazimika kulikarabati mara kwa mara kutokana na baadhi ya vipuri siyo imara.
Akizindua mradi wa trekta za Kilimo Kwanza kwa kupitia Shirika la Ujasiriamali la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT), mwaka 2010, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema, katika kipindi cha mwaka 2005/2006 hadi 2009/2010 jumla ya trekta kubwa 2,364 na matrekta madogo 3,214 yaliingizwa nchini na kuuzwa na kampuni binafsi.
Wakuu wa Mikoa
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Pascal Mabiti, amethibitisha kuwapo na tatizo hilo katika mkoa wake, huku akieleza kuwa ni vigumu kuwazuia wamiliki wa trekta hizo kwa kuwa ni mali ya wakulima wenyewe.
“Hilo tatizo, lipo na hata jana nilipokuwa nikitoka Meatu, nimekutana na moja limebeba mzigo mkubwa hadi limelemewa na trela lake kusambaratika, lakini ni vigumu kumbana mtu kwa kitu anachokilipia au amekinunua mwenyewe, ”anasema.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Chiku Galawa, anasema kuwa hajawahi kukutana na wakulima wakiwa wamebeba abiria kwenye trekta na kama akiwakuta atachukua hatua bila kujali kama ni lake au la halmashauri.
“Hizi trekta zipo za aina nyingi. Kuna ya mkulima mmoja mmoja na kuna ya vikundi ambayo Halmashauri ilichangia fedha kidogo, lakini hilo halinizuii kumchukulia hatua mtu yeyote nitakayemkuta amebeba abiria kwenye trekta kwa sababu sheria za nchi haziruhusu na hakuna aliyeko juu ya Sheria, Sheria zipo wazi kwamba trekta na malori hayaruhusiwi kubeba abiria, ”anasema Galawa.
Wakuu wa Wilaya
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chemba, mkoani Dodoma, Francis Isack anakiri wakulima kutumia trekta kubebea mizigo na abiria.
“Sioni tatizo katika hilo kutokana na barabara na vyombo vya usafiri kuwa ni tatizo kwa mikoa na wilaya nyingi nchini. Wakulima hulazimika kuyatumia trekta zao kwa matumizi mengine kulingana na hali halisi, lakini unapofika wakati wa kulima wanalima, hapo sioni shida, ”anasema Isack.
Anaongeza kuwa matumizi ya kubeba mizigo na watu ni sahihi kwa trekta na ndiyo maana likawa na trela nyuma Kama kungekuwa na tatizo wasingeweka sehemu ya mizigo.
Mkuu wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Elibariki Kingu, anasema kuwa wakulima wa wilaya yake wanatumia trekta kubebea mazao, lakini hajawahi kuona wakibeba abiria.
“Kwa kuwa kubeba abiria kwa kutumia trekta ni hatari, nikithibitisha kuwapo kwa hali hiyo nitavitaarifu vyombo vya usalama vihakikishe vinalikomesha hilo na kuanzia sasa nitalifuatailia kwa ukaribu ili nijiridhishe kuwapo kwake, ”anasema Kingu.
Mkurugenzi wa Zana za Kilimo katika Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mark Lyimo, alisema powertiller zilizoingizwa nchini kwa mwaka jana kuwa ni 828 ikiwa ni pungufu pia ya powertiller 1,172, huku zilizopo nchini kwa jumla ziko 6,348 hadi kufikia Desemba mwaka jana.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Sophia Kaduma anakanusha matrekta hayo kushindwa kutumika ipasavyo akisema:
“Siyo kwamba wakulima hao wamebadili matumizi ya matrekta na powertiller, bali wanayatumia kubebea mizigo wakati ambao siyo wa kilimo.”
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa