Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Matibabu mengine hayahitaji tiba za dawa kali au
kuchomwa sindano, mtindo wako wa maisha waweza kuwa tiba bora kabisa.
Wataalamu wa afya wanasema, kupumzika, kupima afya na kula mlo kamili
vyaweza kuwa tiba.
Tabia na mienendo ya watu kimaisha imekuwa ni
sababu ya matatizo kwao, jamii na hata kwa uchumi wa nchi ambao
unahitaji sana nguvu kazi inayotokana na afya njema.
Afya ya mtu yeyote inategemea sana namna
anavyokula, anavyoishi na kujiweka katika mazingira yanayomzunguka ili
kujikinga na maradhi.
Miongoni mwa mambo yanayohatarisha afya za watu
wengi nchini ni ulaji usiofaa, kutofanya mazoezi au kazi ngumu, utumiaji
wa tumbaku, vileo na vipodozi visivyo salama.
Tabia nyingine mbaya kwa afya ni uchafuzi wa mazingira, hewa, maji na uzalishaji wa kelele zisizokuwa ya lazima.
Mambo mengine ni ile hali ya mtu kujiweka katika
mazingira hatarishi kiusalama kama vile ngono zembe na mwendo kasi wa
vyombo vya usafiri kiasi cha kuweza kusababisha ajali na kujeruhiwa au
kufa.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa magonjwa ya yasiyoambukiza yanaongezeka kwa kasi katika jamii ya Watanzania.
Shirika la Afya la Dunia (WHO) linakadiria kuwa magonjwa yasiyoambukiza yataongezeka zaidi katika Bara la Afrika.
Magonjwa hayo ni kama vile kisukari, maradhi ya moyo, saratani na kuongezeka kwa uzito.
Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2020 kiwango cha
magonjwa hayo yasiyo ya kuambukiza yataongezeka katika Bara la Afrika
kutokana na mabadiliko ya teknolojia kubadilisha mitindo ya kuishi.
Utafiti uliofanywa na Sayoki G.M Mfinanga na
wenzake juu ya magonjwa ya kuambukiza kwa kuyalinganisha na yale yasiyo
ya kuambukiza, umegundua jambo ambalo Watanzania hawana budi kuanza
kuchukua tahadhari.
Utafiti huo umebaini kuwa ugonjwa wa shinikizo la
juu la damu sasa unafikia kiasi cha asilimia 45 ya magonjwa yote kwa
watu wenye umri zaidi ya miaka 25.
Magonjwa ya kisukari na saratani nayo pia yanaongezeka kwa kasi.
Afya inaweza kuboreshwa na kudumishwa kwa njia rahisi kupitia mtindo wa maisha unaofaa.
Jambo la kuzingatia ni kufahamu kwamba hakuna ugonjwa ambao hauna chanzo.
Wataalamu wa afya ya jamii wanasema kuwa takribani
asilimia 53 ya magonjwa ya binadamu husababishwa na mtindo wa maisha
usiofaa kwa mfano: ulafi, ulevi, kubweteka bila kufanya kazi ngumu,
kutofanya mazoezi na ngono zembe.
Wataalamu wanaongeza kusema kuwa asilimia 21 ya
magonjwa hutokana na uchafu wa mazingira na mwili na asilimia 16
hutokana na yale ya kurithi kupitia vinasaba (DNA).
Utafiti huo umebaini kuwa asilimia 10 ya magonjwa
husababishwa na makosa yatokanayo na tiba kwa mfano matumizi mabaya ya
dawa, vipimo vikubwa vya dawa na tiba zisizofaa.
Mambo ya kuepukwa
Kituo cha kwanza kwa ajili ya kutunza afya ya mtu
ni mahali anapoishi. Hii inatokana na ukweli kwamba tunatumia saa nane
kwa kulala usiku.
Inakadiriwa pia binadamu hutumia saa nane nyingine
baada ya kutoka kazini kwa kujipumzisha ndani au nje ya nyumba zetu
mahali tunapoishi.
Sehemu ya muda huo pia huweza kutumiwa kwa ajili
ya kukutana na marafiki kubadilishana mawazo. Inaweza kuwa ni ufukweni,
uwanjani au baa ama vijiweni. Huko nako vihatarishi vya kiafya vipo.
Saa nane nyingine zinakadiriwa kuwa mtu anakuwa kazini ambako nako kunahitajika mazingira ya usalama.
Hii ina maana kwamba kama nyumbani, kazini au
sehemu anazoenda kupumzika, kustarehe au kubadilishana kuna chochote
kinachodhuru afya, ni rahisi kutusababishia magonjwa.
Magonjwa mengi huchukua muda mrefu kuanza kuonyesha dalili na mfano mzuri ni saratani.
Njia pekeee iliyo bora zaidi ya kukabiliana na
magonjwa haya ni kuyatibu kwa dawa-lishe na njia nyingine kama vile
mazoezi, kunywa maji mengi, ulaji unaofaa na kuvuta hewa safi kwa wingi.
Baadhi ya magonjwa siyo lazima yatibiwe kwa dawa
hospitalini kwa mfano mafua na kikohozi kikavu huweza kutibiwa nyumbani
kwa kutumia limau au asali.
Mapumziko na maji ya vuguvugu yanaweza kuwa tiba nzuri kwa maumivu ya kichwa yatokanayo na msongo wa mawezo.
Maji ya dafu yanaweza kuwa dawa nzuri kwa tatizo
la kuharisha na kupiga mswaki angalau mara mbili kwa siku, hupunguza
hatari ya magonjwa ya kinywa, meno na maradhi ya moyo.
Kuoga kila siku na kuvaa mavazi safi huzuia magonjwa ya ngozi na kuishi mazingira safi ya nyumbani hurefusha maisha.
Bustani za maua mazuri husaidia akili kufanya kazi vizuri na kuimarisha uwezo wa kujifunza mambo.
Mlo kamili na lishe bora
Watu wengi hawazingatii kanuni za ulaji na lishe bora.
Mlo kamili kwa kawaida una mchanganyiko wa viini
lishe vya makundi yote ya vyakula ambavyo ni wanga, protini, vitamin,
mafuta, madini, nyuzilishe na maji.
Chakula bora pia ni kile hai ambacho
hakijakobolewa, hakijaungua, hakijaharibika au kuchemshwa sana isipokuwa
nyama na maharage makavu.
Watanzania wengi hawali kiasi cha kutosha cha
matunda na mbogamboga. Waingereza wana msemo: “An apple a day will keep
the doctor away…An apple before bed makes the doctor beg his bread”.
Huu ni msemo ambao unahimiza watu kutumia matunda mara kwa mara
ili kuepuka maradhi na wala siyo uone kwamba unaanza kudhoofu ndiyo
utumie maana kama ni ugonjwa lazima itakulazimisha ukatafute tiba.
Wanatumia msemo huo kuonyesha umuhimu wa kula
vyakula vyenye asili ya mimea hasa matunda. Matunda pamoja na mambo
mengine, huupatia mwili vitamin C ambayo ni ya muhimu kwa ajili ya kinga
ya mwili.
Ni muhimu kupunguza ulaji wa nyama na kuongeza mboga na matunda ili kuzuia magonjwa ya moyo, kansa, kisukari na kitambi.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment