Home » » WATU 60 WAHOFIA KUUGUA DENGUE LINDI

WATU 60 WAHOFIA KUUGUA DENGUE LINDI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Afisa uhusiano wa Manispaa ya Temeke,Joyce Msumba
 
Zaidi ya wagonjwa  60  kutoka wilaya za mkoa wa Lindi wanahofiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa dengue.

Kutokana na hali hiyo, wanatarajiwa  kuchuliwa vipimo na  kufanyiwa uchunguzi  kwenye maabara ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutokana na hospitali ya mkoa huo kukosa vifaa vya kutambua ugonjwa huo.

Kaimu Mganga Mkuu  wa Mkoa wa Lindi, Dk. Theophil Malibiche, alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.Dk. Malibiche watachukua wagonjwa wanaoonyesha dalili za dengue.

Alisema hadi sasa hakuna mtu aliyebainika kuwa na homa hiyo wala aliyefariki na kwamba mkoa umejipanga kutoa mafunzo kwa  wataalamu wa afya katika wilaya zote za mkoa huo.

Aliwaomba wananchi mkoani  humo kuchukua tahadhari  ya ugonjwa huo kwa kufanya usafi wa mazingira na kuangamiza  maeneo ya mazalia ya mbu wakati utaratibu wa kupata madawa za chanjo na kinga ukisubiriwa.

Wakati huo huo, idadi  ya wagonjwa waliogundulika na ugonjwa huo katika Hospitali ya Amana, jijini Dar es Salaam, sasa imefikia 79 tangu ugonjwa huo uibuke.

Akizungumza na NIPASHE,  Daktari Kiongozi wa Hospitali hiyo, Andrew Method, alisema kati ya wagonjwa hao 73 waliruhusiwa na sita bado wamelazwa.

Aidha, Dk. Method alisema katika hospitali hiyo hakuna kifo kilichotokana na ugonjwa huo.

Katika Hospitali ya Temeke idadi ya wagonjwa ambao wameugua ugonjwa huo tangu  kuibuka mwaka huu ni 72 na kati ya hao, 62 wameruhusiwa.

Afisa uhusiano wa Manispaa ya Temeke, Joyce Msumba, alisema wagonjwa 10 bado wamelazwa na kuwa kati ya hao, sita ni wanawake na wanne ni wanaume.

Msumba alisema pia hospitali hiyo inachukua tahadhari ya kuendelea kupuliza dawa na wagonjwa kulazwa ndani ya vyandarua kwa ajili ya kuzuia kuambukiza wengine.

Katika Hospitali ya Mwananyamala, idadi ya wagonjwa mpaka imefikia 144, wapya ni wanne na mmoja ndiye amelazwa, kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo,  Dk. Faustinias Ngonyani.

Katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hadi jana hapakuwapo na mgonjwa wa dengue.

SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa