Tabia ya wananchi kuhamia mashambani na kufanya makazi ya kudumu na kuwa mbali na shule kumetajwa kuwa ni miongoni mwa sababu zinazochangia wilaya ya Nachingwea,mkoa wa Lindi kuwa na mahudhurio duni kwenye Shule zake.
Hayo yamesemwa na Afisa elimu wa shule za msingi wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea, Makwasa Bulenga kwenye taarifa yake aliyoisoma kwenye kikao cha wadau wa elimu
Amesema kuwa baadhi ya wazazi na walezi wamevihama vijiji vyao na kuhamia mashambani wakijishughulisha na Kilimo ambapo ni mbali kabisa na zilipo shule hali inayowawia vigumu watoto kuhudhuria masomo na wengine kukatiza kabisa masomo yao.
Bulenga amewataka wadau hao kufanya juhudi za makusudi za kuishawishi jamii kuishi katika vijiji vyenye shule na kuwa iwapo itashindikana na kulazikima kwenda mashambani wawaache watoto waendelee na masomo badala ya kwenda nao mashambani kwani kwa kufanya hivyo ni kuonesha wazi kuwa wazazi hao hawaoni umuhimu wa elimu kwa watoto wao.
Amesisitiza kuwa Viongozi wa Vijiji na Kata kutumia sheria ndogo zilizopo kwa kuwachukulia hatua kali wazazi na walezi ambao wanasababisha utoro kwa wanafunzi na kwamba endapo Viongozi watatimiza majukumu yao basi tabia hiyo itakoma kabisa.
Akizungumzia ukosefu wa miundombinu mbalimbali ikiwemo Madarasa,madawati matundu ya vyoo Bulenga amewataka watendaji hao kuweka mikakati ya kuboresha miundombinu hiyo kwenye shule zilizo kwenye maeneo yao na kuwa idara itaendelea kuomba bajeti ya kuongeza miundombinu kutoka kwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment