Home » » JAMII YATAKIWA KUPIMA AFYA ZAO MARA KWA MARA

JAMII YATAKIWA KUPIMA AFYA ZAO MARA KWA MARA

Jamii imetakiwa kuacha woga wa kupima afya na badala yake   kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara kwa lengo la kuweza kuchukua hatua stahiki mara baada ya kugundulika kwa ugonjwa kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kupunguza gharama za matibabu.
                                    
Mwito huo umetolewa na Askofu wa kanisa Katoliki jimbo la Lindi,mhashamu Bruno Ngonyani  wakati wa uzinduzi wa  jengo la kliniki kwa waathirika wa VVU(CTC) lililopo kwenye hospitali ya kanisa katoliki ya Mnero,wilaya ya Nachingwea,mkoa wa Lindi ambalo litatumika pia kutoa huduma za ushauri nasaha na upimaji wa hiari wa Virus vya ukimwi. 

Hata hivyo imeelezwa kuwa  jamii nyingi zimekuwa na uoga wa  kuchunguza afya  kila wakati hali ambayo kwa kiasi kikubwa  inachangia vifo visivyo vya lazima na hivyo  waganga kwenye vituo vya kutolea tiba  kwa nafasi zao watoe elimu ya umuhimu wa kupima afya  kwani tabia ya kusubiri hadi ugonjwa unajitokeza kwa kiasi kikubwa inaongeza gharama za matibabu.


Awali akisoma  taarifa ya ujenzi wa jengo hilo,Afisa Utawala wa  hospitali hiyo ya Mnero, Bertina Mnali  amesema kuwa  kukamilika kwa jengo hilo  licha ya kutoa ushauri nasaha  pia litatoa huduma mbadala kwa magonjwa yanayoambatana na ukimwi na litasaidia pia  watoa huduma ya afya kuweza kutoa huduma katika mazinggira mazuri na yenye mandhari ya kuvutia.

Pia amesema kuwa   wateja watakaotumia kituo hicho watapata sehemu nzuri ya kupata huduma huku akisisitiza kuwepo kwa mwamko chanya kwa wanakijiji wa maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kupima afya zao.


Jengo hilo limegharimu kiasi cha shilingi milioni 124 kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani kupitia shirika la Kuzuia maambukizi ya ukimwi kutoka kwa Mama mjauzito   kwenda kwa mtoto (EGPAF) kwa lengo la kupata sehemu ya kutolea huduma kwa watu wanaoishi na virus vya ukimwi kwa wakazi wa wilaya ya Nachingwea hususani kwa wananchi wa Kata ya Mnero Mngongo na kata zinazozunguka hospitali hiyo.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa