Home » » Deni la walimu lafikia Bil.61

Deni la walimu lafikia Bil.61

SERIKALI imekiri kudaiwa na walimu nchini, sh. bilioni 61.0 zikiwa ni madeni ya malimbikizo mbalimbali zikiwemo fedha za likizo na matibabu.
Hayo yalisemwa juzi na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenister Mhagama, alipokuwa akizungumza na uongozi wa mkoa wa Lindi na wanafunzi wa shule ya msingi wasioona Nyangao, iliyopo katika Halmashauri ya wilaya hiyo.
Akizungumza katika shule hiyo, Mhagama alisema kutokana na tathimini iliyofanyika walimu hapa nchini, wanadai kiasi hicho cha fedha, huku sh.bilioni 53.0 zipo mikononi mwa TAMISEMI na Sh.bilioni 8.0 zilizobaki inadaiwa wizara yake.
"Kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa imebainika walimu wetu wanadai sh. bilioni 61.0 kati ya hizo TAMISEMI wanadaiwa sh. 53.0 bilioni na wizara yangu sh. bilioni 8.0 bili," alisema Mhagama.
Naibu waziri huyo alisema kutokana na tathmini hiyo, Serikali inaendelea kulipa madeni hayo, ili kuwawezesha walimu waendelee na majukumu yao ya ufundishaji kwa moyo mmoja.
Ameueleza uongozi huo wa mkoa kwamba walimu wasipolipwa stahiki zao kwa haraka, kunawafanya waendelee kuvunjika moyo wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa bidii.
Pia naibu waziri huyo alisema wizara yake hivi sasa inajipanga ili kuandaa mafunzo ya mara kwa mara ya walimu yatakayowafanya waendane na hali halisi ya elimu iliyopo kwa wakati huu wa sasa.
Naibu waziri huyo alisema wakati wanaendelea kujipanga, wizara yake imeanza kutatua matatizo yaliyopo ikiwemo kuziingiza baadhi ya shule katika mfumo wa ufundishaji wa kutumia kompyuta.
"Mpaka sasa tayari vituo 50 vimefunguliwa, ambapo mwalimu wa somo la sayansi anakuwa na skrini moja kama TV na kuweza kufundisha madarasa matano kwa wakati mmoja na wanafunzi wakaelewa vizuri," alisema Mhagama.
Mhagama alisema baada ya muda, lengo la Serikali ni kuhakikisha mfumo huo wa mafunzo kwa njia ya kompyuta unaeneo takriban nchi mzima hapa Tanzania, ili kuweza kuwasaidia wanafunzi katika masomo yao ya sayansi.
Awali akimkaribisha Naibu Waziri kuzungumza na wanafunzi pamoja na uongozi wa mkoa huo, mwakilishi kutoka Ofisi ya Idara ya elimu mkoani Lindi, Saluku Kakama alisema, mkoa una shule 122 za sekondari zikiwemo sita za binafsi, unakabiliwa na tatizo kubwa la walimu wa masomo ya sayansi, hali inayowafanya wanafunzi kufanya vibaya katika masomo hayo.

Chanzo;Majira

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa