Nilishawahi kuandika kuwa tunapozungumzia utalii, mojawapo ya
mambo muhimu ni ile ya kuwatembeza maeneo mbalimbali ili kujionea
vivutio.
Watalii wamegawanyika katika makundi mbalimbali
ikitegemea uwezo wao wa fedha, vitu wanavyohitaji kuviona, na wapi
viliko, na pengine kama wanataka kujenga urafiki na jamii
wanayoitembelea, kuuliza maswali na kujenga ufahamu zaidi kutoka kwa
wenyeji.
Kuna wale ambao wangetaka kutumia fursa ya utalii kupiga picha vivutio au na watu, na kadhalika.
Jambo muhimu kwa utalii ni kuweza kufika mahali kwa urahisi na bila kuwa na hofu ya kuwa na usalama mdogo.
Na hapa sasa kwa watalii waendao au wanaotembea
kwa miguu usalama wao barabarani ni muhimu sana, katika hili ni kwamba
tunapaswa kudhibiti tabia za waendesha magari. Watalii hawazunguki tu
kwa kuangalia ramani, bali kwa kuhakikisha wanapotembea hawapatwi na
ajali.
Pia wanahitaji kuheshimiwa kama sehemu ya
watumiaji ya barabara. Watalii wanaotoka nchi nyingi zilizoendelea wana
utamaduni tofauti kabisa wa matumizi ya barabara.
Waendesha magari wanaheshimu watembea kwa miguu,
waendesha magari wanaheshimu taa za barabarani kiasi kwamba hata kama ni
usiku wa manane, dereva yuko peke yake barabarani atasimama kwenye taa
kama hajaruhusiwa, atapunguza mwendo sehemu wanakopita waenda kwa miguu
hata kama hakuna anayevuka.
Atasimama kumpisha mwenda kwa miguu akiona dalili kuwa anataka kuvuka barabara.
Hapa ni vurugu tupu; waendesha magari ndio wenye
haki, hawasimami kwenye vivuko vya watembea kwa miguu; wengi wa watembea
kwa miguu hulazimika kusimama hadi miguu iwaume wakisubiri kuvuka. Ni
kawaida kuona wakipigiwa honi na kutukanwa wakiwa katikati ya barabara,
na wapo waliopondwa na kufa. Madereva hawaheshimu taa za barabarani, na
wanasahau kwamba wengine pia wana haki ya kutumia barabara.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment