ZAIDI ya kaya 80 za Kijiji cha Nyengedi, kilichoko katika Jimbo la
Mtama, Wilaya ya Lindi Vijijini, hazina mahala pa kuishi baada ya
nyumba zao kuezuliwa na kimbunga kilichoambatana na mvua kubwa
iliyonyesha juzi kijijini hapo.
Akithibitisha kutokea kwa maafa hayo, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha
Nyengedi, Ally Mpili, alisema mvua hiyo ilinyesha takriban dakika 45,
zikiwamo 15 za kimbunga hicho kilichoezua pia paa la darasa la nne la
Shule ya Msingi Nyengedi.
“Wakazi wa hapa walikosa mvua kwa takribani wiki moja, kabla ya
ghafla juzi kuanza kunyesha kuanzia saa 8:30 mchana hadi saa 9:15
alasiri, lakini kwa bahati mbaya mvua hiyo ikaambatana na upepo mkali,
ulioezua na kubomoa nyumba 81 na kuezua paa la darasa la nne,” alisema
Mpili.
Alibainisha uharibifu huo umewaacha bila makazi takriban watu 250
waliokuwa wakiishi katika kaya hizo, ambao kwa sasa wanalala chini ya
miti, kwenye magofu yao na baadhi kujihifadhi kwa ndugu zao.
Kutokana na hali hiyo, wameiomba serikali kuharakisha misaada ya
kibinadamu, ili kuwanusuru na athari zitokanazo na mvua za masika
zinazoendelea.
Mpili alisema Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtama, aliyemtaja kwa jina
moja la Naska, alikuwa wa kwanza kufika kijijini hapo kujionea uharibu
uliotokea, wakati Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, walitarajiwa
kufika kijijini hapo jana.
Mmoja wa waathrika wa kimbunga hicho, Abdallah Amour Mcheu, ambaye
pia ni mwenyekiti wa kijiji, alisema pigo alilolipata na wenzake ni
kwa kuwa wapo katika kipindi cha utayarishaji mashamba.
Said Ghalama Ndambalilo, ambaye ni mstaafu wa Jeshi la Magereza
alisema: “Ni kipindi cha kilimo hatua ya upandaji, hivyo tukio hili ni
pigo kwetu, litakalotufanya tuwe na majukumu mawili mazito ya kilimo na
ujenzi wa nyumba zetu upya. Tunaiomba serikali kutuangalia kwa jicho
la huruma ili kusaidia familia hizi.”
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment