Home » » Wabunge Kusini washangazwa kasi ya utandikaji bomba la gesi

Wabunge Kusini washangazwa kasi ya utandikaji bomba la gesi

Mbunge wa Chama cha Wananchi (CUF), Salum Barwany
 
Mbunge wa Chama cha Wananchi (CUF), Salum Barwany (Lindi Mjini) na Saidi Mtanda (Mchinga –CCM), wamesema wanashangaa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam ukifanywa kwa kasi na kukaribia kumalizika wakati ujenzi wa sehemu ya barabara ya kilomita 10 bado kukamilika ikiwa imechukua miaka zaidi ya 10.
Walikuwa wakichangia kwa nyakati tofauti Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na Kamati ya Miundombinu, kuhusu utekelezaji wa shughuli za kamati hizo kipindi cha Machi hadi Novemba, mwaka huu.

Barwany alisema kauli inayotolewa kwamba wakazi wa Mtwara hawataki gesi itoke huko na kupelekwa Dar es Salaam kwa matumizi ya Watanzania wengine siyo za kweli.

“Kauli gesi haitoki si kweli – wanachodai wao ni mikataba hiyo ya gesi ipo wapi, tunataka tuione. Kauli kwamba gesi haitoki ni ya kuwagombanisha wananchi wa Mtwara na wananchi wengine na serikali yao.

“Wananchi wa Kusini sasa tunataka kuona tunanufaika vipi na gesi hiyo. Leo shughuli za kisiasa zimepigwa marufuku kwa sababu tu ya ujenzi wa bomba la gesi na kauli kwamba wakazi wa kule wamesema gesi yao haitoki.

“Watazame wananchi katika maeneo yenye raslimali kubwa ndio wanaoishi katika maisha duni na kukosa elimu,” alisema.

Kwa upande wake, Mtanda alisema: “Wananchi wa Lindi na Mtwara hawana tatizo na kutoa gesi kwenda Dar es Salaam.”

Aliongeza: “Isipokuwa wanahoji namna gani miradi waliyoahidiwa haijatekelezwa wakati mradi huu wa bomba la gesi unakaribia kumalizika.

Leo tunaomba watu wanaolinda bomba hili linalokwenda Dar es Salaam wapate umeme, lakini wenyewe wanaolinda hawana umeme.”
Pia alitaka wananchi wanaotoa ardhi yao kupisha ujenzi wa bomba la mafuta ni lazima walipwe fidia ya kutosha.

Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), mapema alitaka serikali kuhakikisha kwamba bomba la gesi linalojengwa kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam linalindwa ili liweze kuwa salama zaidi.

Alitaka serikali iwasomeshe Watanzania wengi ili kushika nafasi katika sekta ya mafuta na gesi baada ya  wawekezaji wa nje kumaliza muda wake.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa