Home » » `Nguvu kubwa ya serikali itumike kudhibiti mafisadi`

`Nguvu kubwa ya serikali itumike kudhibiti mafisadi`

Mbunge wa Lindi Mjini, Salum Khalfan Barwany, (CUF)
 
Mbunge wa Lindi Mjini, Salum Khalfan Barwany, (CUF), amesema nguvu kubwa ya serikali huonekana wakati ikidhibiti maandamano yanayofanywa na wananchi au wanapogusa maeneo yenye maslahi ya serikali.
Akichangia bungeni kuhusu taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Barwany alisema: "Ukitaka kuona nguvu ya mlevi, mwaga pombe yake.”

Vile vile aliongeza: "Ukitaka kuona nguvu ya serikali fanya maandamano au gusa maeneo ya maslahi yake…hapo utaona nguvu yake."
Barwany alitaka nguvu hiyo kubwa ya serikali inayotumika kuzima maandamano ya wananchi sehemu mbalimbali, itumike pia kudhibiti ufisadi ambao umekithiri katika halmashauri mbalimbali.

Alisema anaamini kwamba serikali inaweza kufanya hivyo lakini haijaamua.

Alisema kwa mfano, tangu Halmashauri ya Mji wa Lindi ilipotangazwa kuwa Manispaa miaka mitatu iliyopita kwa kuongezewa kata tatu zaidi, bado ruzuku ya maendeleo inayopata ni ya kata 15 tu, lakini suala hilo limefikishwa Tamisemi bila mafanikio yoyote.

Naye Mbunge Mtambile, Masoud Abdallah Salim (CUF), alisema na kuzitaja halmashauri chache kama za Ruangwa, Temeke na Arusha kuwa zimebainika kuwa na vitendo vingi vya ufisadi kwa mawakala kukusanya kodi mbalimbali bila kuziwasilisha.

Alisema kumekuwa na hati nyingi za kughushi katika Halmashauri ya Jiji la Arusha kuhusu makusanyo yaliyofanywa na mawakala hata katika fedha za makusanyo ya huduma ya vyoo.

Alisema tatizo kubwa linalojitokeza katika Tamisemi ni kulindana na kutaka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya watendaji hao.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa