Home » » RC aipa somo SSRA

RC aipa somo SSRA

SERIKALI imeitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kujenga utamaduni wa kuhimiza mifuko ya hifadhi za jamii kutembelea mikoani, ili kutatua kero za wanachama ikiwa ni pamoja na kujitangaza.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Ludovick Mwananzila,  alitoa wito huo jana wakati akifunga warsha ya mafunzo ya kutoa elimu kuhusiana na sekta ya hifadhi ya jamii kwa viongozi wa Mkoa wa Lindi  na kusisitiza wananchi kujiunga na mifuko hiyo.
Mkuu huyo wa mkoa (RC), aliwataka waajiriwa wote serikalini na katika mashirika ya umma kuwa na tabia ya kutunza kumbukumbu zao za ajira, ili kupunguza adha zinazoweza kutokea baada ya kufikia ukomo katika ajira na kusababisha kucheleweshwa kupata mafao yao.
Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Lindi, Steven Chami, akitoa mada katika mafunzo hayo, ameiomba mamlaka hiyo kutoishia kuelimisha viongozi wa ngazi za juu pekee na badala yake itafutwe namna ya kuelimisha watu wengi zaidi, ili kupunguza manung’uniko kwa wanachama kwa kuingizwa katika mifuko ambayo hawajui manufaa yake.
Mkuu wa Mawasiliano na Uhamasishaji wa SSRA, Sarah Msika, alisema dhima ya mamlaka hiyo ni kuhakikisha wanachama wa mifuko ya hifadhi za jamii wanapatiwa huduma bora bila ya kujali kazi au kipato chao.
Chanzo;Tanznia Daima

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa