Serikali imeitaka mamlaka ya usimamizi wa sekta ya hifadhi za
jamii SSRA kujenga utamaduni wa kuhimiza mifuko ya hifadhi za jamii kutembelea
mikoani ili kutatua kero za wanachama ikiwa ni pamoja na kujitangaza ili
kuhamasisha wafanyakazi wa serikali na mashirika ya umma kujiunga na mifuko
hiyo.
Hayo yamesemwa na mkuu wa mkoa wa Lindi Ludovick Mwananzila
wakati akifunga warsha ya mafunzo ya kutoa elimu kuhusiana na sekta ya hifadhi
ya jamii kwa viongozi wa mkoa wa Lindi ambapo amesisitiza juu ya wananchi
kujiunga na mifuko ya namna hiyo.
Amewataka waajiriwa wote wa serikalini na katika mashirika
ya umma kuwa na tabia ya kutunza kumbukumbu zao za ajira ili kupunguza adha
ambazo huweza kutokea mara baada ya kufikia ukomo katika ajira na kusababisha
kucheleweshwa kupata mafao yake.
Afisa TAKUKURU mkoa wa Lindi Steven Chami akitoa hoja katika
mafunzo hayo ameiomba mamlaka hiyo kutoishia kuelimisha viongozi wa ngazi za
juu pekee na badala yake itafutwe namna ya kuelimisha watu wengi zaidi ili
kupunguza manung’uniko kwa wanachama kwa kuingizwa katika mifuko
hawaifahamu wala kujua manufaa watakayopata kutokana na mfuko huo.
Naye mkuu wa mawasiliano na uhamasishaji wa SSRA Sarah
Kibonde Msika amesema kuwa dhima ya mamlaka hiyo ni kuhakikisha wanachama wa
mifuko ya hifadhi za jamii wanapatiwa huduma zilizo bora bila ya kujali kazi au
kipato chake.
Mpaka sasa Tanzania bara kuna mifuko mitano ya hifadhi ya
jamii na Tanzania visiwani mfuko mmoja ambapo takwimu zinaonesha kuwa wanachama
zaidi ya milioni moja na nusu wananufaika na mifuko hiyo.
0 comments:
Post a Comment