KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimetakiwa kufuatilia wawekezaji wote ili kuona kama mikataba waliyoingia inafuatwa.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, alipokuwa akijibu swali
la nyongeza la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM).
Katika swali lake, mbunge huyo alisema hivi sasa kuna wawekezaji
kutoka China, Marekani na Hong Kong na imefikia hatua wameingia kwenye
biashara ya uuzaji wa bidhaa ikiwa ni pamoja na kufungua maduka.
Alitaka kujua ni uwekezaji wa aina gani unaofanyika na ni lini uhakiki wa wageni hao utafanywa.
Akijibu swali hilo, Dk. Nagu alisema kufanya biashara si uwekezaji
ila uwekezaji ni kwenye kilimo, viwanda na maeneo mengine ya
uzalishaji.
Alisema uwekezaji wowote lazima ulete masilahi kwenye nchi ambayo inapokea wawekezaji.
Katika swali la msingi, mbunge huyo alitaka kujua ni sababu zipi
zinazochangia raia wa kigeni kuzagaa hovyo katika maeneo ya vijijini na
kushindania fursa kibiashara na wazawa.
Pia, alihoji kwa nini serikali isiamuru raia hao kubaki katika maeneo ya miji mikuu pekee.
Akijibu swali hilo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla,
alimuomba mbunge na wananchi kwa ujumla kutoa taarifa za raia yeyote wa
kigeni anayezagaa nchini bila kibali kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama,
ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
CHANZO;MWANANCHI
|
0 comments:
Post a Comment