Home » » Makali ya mgawo wa umeme yapunguzwa

Makali ya mgawo wa umeme yapunguzwa

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco,Felichesmi Mramba
Wakati  zikiwa zimebaki siku nne kufika mwisho wa matengenezo ya visima vya gesi asilia vilivyopo Songosongo, Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, Shirika la Umeme nchini (Tanesco), limesema marekebisho yamefikia asilimia 80 na hivyo kupunguza makali ya mgawo wa umeme.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felichesmi Mramba, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu tatizo la umeme lililojitokeza tangu mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye mitambo ya visima vya gesi asilia vya Songosongo na tathmini ya matengenezo.

Kwa mujibu wa Mramba, matengenezo hayo yalitakiwa yafanywe ndani ya siku 10 hadi Novemba 26, mwaka huu, lakini kampuni hiyo imejitahidi kufanya kazi na kwamba hadi jana kazi iliyofanyika ni ya kiwango cha asilimia hizo na hivyo kupunguza makali ya mgawo wa umeme uliolikumba taifa kuanzia mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kutokana na hilo, alisema kuanzia jana jioni, umeme katika maeneo mbalimbali nchini ungerejea kama kawaida kwa zaidi ya asilimia 85.

“Visima vya gesi vya Songosongo si mali ya Tanesco, hivyo walikuwa na matengenezo kuanzia tarehe 16 mwezi huu. Matengenezo hayo ambayo hufanyika kila mwaka, yameathiri huduma ya umeme kwa wananchi tangu muda huo,” alisema Mramba.

Aliongeza: “Wale watu wa Pan African wameshamaliza kazi kwa asilimia 80," alisema.

Hata hivyo, alipohojiwa kuhusiana na hasara iliyopatikana kutokana na mgawo huo, alisema atazungumza baada ya kumalizika kwa siku 10 za matengenezo.

Kuhusu hali ya mabwawa yanayozalisha umeme nchini, Mramba alisema siyo nzuri na kwamba kwa sasa shirika hilo halitegemei sana chanzo cha nishati hiyo zaidi ya ile ya mafuta na gesi.

Alisema Bwawa la Mtera, ambalo hutakiwa kuwa na kiasi cha mita za ujazo 69, lakini sasa linazo 60.7.

Mramba pia alipingana na madai ya kwamba shirika hilo linafanya mgawo wa kutoa huduma hiyo kwa Watanzania kimatabaka,  bali huangalia maeneo maalumu kama vile ya hospitali, vyuo ambako umeme unapaswa kuwapo kwa muda mwingi kuliko maeneo mengine.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Tanesco lilitangaza mgawo wa umeme kwa nchi nzima kutokana na zoezi la usafishwaji wa mitambo kwenye visima vya gesi vilivyoko Songosongo kwa siku 10 kuanzia Novemba 16 hadi 26, mwaka huu muda ambao kazi hiyo ingemalizika.
CHANZO: NIPASHE0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa