Home »
» Bima ya afya yaonya watoa huduma
Bima ya afya yaonya watoa huduma
|
|
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya imetoa onyo kwa watoa huduma
ambao si waaminifu kuwa itawachukulia hatua kali ikiwemo kuwafikisha
kwenye vyombo vya sheria kwani kuna wanaojihusisha na kugushi hati na
kujipatia malipo kwa njia ya udanganyifu.
Onyo hilo limetolewa juzi na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya, Charles Kajege, kwenye mkutano wa Kongamano
la wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii
uliofanyika kwenye ukumbi wa Kagwa mjini Lindi.
Alibainisha kuwa kuna baadhi ya wahudumu wamekuwa wadanganyifu kwa lengo la kujipatia fedha kwa kujaza taarifa za uongo.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Kajege alisema kuwa bodi
imeanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuuagiza uongozi wa
mfuko kuwasilisha mapendekezo ya namna ya kulitatua ikiwa ni
pamoja na kuliwekea sera yake na namna ya kulishughulikia.
Mjumbe huyo alitaja changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya wanachama
kutumia kitambulisho kimoja kwa watu wengine ambao si wanachama wa
mfuko na kuwa wamejipanga kuhahakikisha kuwa wanachama wanaostahili
tu ndio wanaopata huduma na katika kuhakikisha hilo na katika kudhitibi
hilo mfuko umeamua kila hospitali kubwa inakuwa na maafisa wa mfuko wa
taifa wa Bima ya Afya kwa ajili ya udhibiti na ufuatiliaji zaidi.
“Tunachukua hatua za kushirikisha vyombo vingine vya dola na mamlaka
nyingine za kisheria na serikali katika suala hili ikiwemo kuwapeleka
katika vyombo vya sheria wahusika wote punde wanapobainika,” alisema
Kajege.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Lindi, Ludovick Mwananzila, ambaye
alikuwa mgeni rasmi, aliwataka viongozi wote wa mkoa huo kuhakikisha
wanaongeza kasi ya uhamasishaji kwa jamii ili wajiunge kwenye mifuko
hiyo.
Alisema kwa sasa mkoa una wanachama wanaonufaika na huduma za mfuko wa afya ya jamii (CHF), Kaya 225,972.
Chanzo;Tanzania Daima
|
|
0 comments:
Post a Comment