WANANCHI wa Kilwa Masoko, mkoani Lindi,
wameshauriwa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), ili waweze kutibiwa kirahisi
pale wanapopatwa na maradhi mbalimbali.
Ushauri huo ulitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya
Kilwa, Abdalah Ulega, kwenye hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Ado Mapunda, wakati wa uzinduzi wa
kampeni ya kuhamasisha shughuli za CHF.
Alisema mfuko huo ni msaada na mkombozi wa kweli wa
afya za jamii, lakini wananchi wengi bado hawajaelewa faida na manufaa yake.
“Nimetaarifiwa wananchi wanaoufaidika na huduma za
mfuko huu hadi Juni 30, mwaka huu hapa Kilwa ilikuwa ni kaya 365 wakati wenzetu
wa Liwale waliojiunga ni kaya 9,137. Jitihada za makusudi lazima zifanyike sasa
ili kuibadilisha Kilwa,” alisema.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya ya Jamii, Hamisi Mdee, alisema jumla ya halmashauri 120 zinatekeleza
huduma za CHF na kaya zinazochangia ni 543,621 sawa na wanufaika milioni 3.2
ambayo ni asilimia 7.5 ya walengwa.
“Uandikishaji wa wanachama wa CHF katika daftari
maalumu kwa ajili ya kuwapatia namba za huduma za uanachama wa CHF nchi nzima
tayari limekwishaanza katika halmashauri 10 kabla ya kufanyika nchi
nzima…tunaomba wadau wetu watupe ushirikiano ili kuboresha kumbukumbu na
taarifa hizo,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment