Home » » Wanafunzi wamcharaza mwalimu bakora

Wanafunzi wamcharaza mwalimu bakora



Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Mnero Wilayani Nachingwea mkoani Lindi, Andrew Chiunguile, amejeruhiwa vibaya baada ya kushambuliwa kwa kupigwa kwa mawe na magongo na wanafunzi, ambao walimtuhumu kula fedha za walizolipa kwa ajili ya mitihani ya moko na michango mingine.

Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki  majira ya saa 5 asubuhi baada ya wanafunzi hao kukusanyanyika na kuanza kurusha mawe  kwenye majengo ya shule hiyo, ambayo mengine yalimjeruhi mwalimu huyo.

Afisa Elimu ya Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Abdallah Membe, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Baada ya kuona hali inakuwa mbaya, baadhi ya walimu waliokuwa shuleni hapo walimchukua mwalimu mwenzao na kumficha kwenye moja ya vyumba vya shule hiyo hadi askari wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Nachingwea walipofika eneo hilo.

Membe alisema uongozi wa shule hiyo ulichukua uamuzi wa kuwaita askari polisi baada ya jitihada ya kuzuia hasira za wanafunzi hao kugonga mwamba kutokana na kuzidiwa nguvu na wanafunzi hao.

Alisema polisi walifika shuleni hapo na kuanza kufyatua mabomu ya machozi  na ndipo wanafunzi hao walianza kutawanyika kuondoka kwenye maeneo ya shule.

Membe alisema hasira za wanafunzi hao zilianza baada ya  baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne kuzuiwa kufanya mtihani wa (moko) kwa madai ya kutolipa ada ya mtihani huo wakati wenyewe wakisema walishalipa kupitia kwa  mwalimu huyo.

Wanafunzi hao walisema mwalimu huyo alipewa jukumu la kukusanya michango hiyo lakini hakuziwasilisha fedha hizo kwa mkuu wa sekondari hiyo.

Membe alisema vurugu hizo zilisababisha mwalimu huyo kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili ikiwamo na usoni baada ya kupigwa na mawe na magongo.

Alisema vurugu za wanafunzi hao zimesababisha hasara kubwa kutokana na  kuharibu samani mbalimbali  zikiwemo viti, madawati na taa za umeme na  kuvujwa kwa milango.

Akizungumzia malalamiko ya wanafunzi hao, Membe, alisema kuwa ofisi yake inafahamu tatizo hilo na tayari ilikuwa imepanga siku hiyo ya tukio  kukutana nao na kuwapa ufafanuzi.

Alisema  utaratibu ulishafanyika wa kuhakikisha wananfunzi hao hawaathiriki na upotevu wa fedha hizo kwa kuhakikisha wanafanya mitihani hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, George Mwakanjinga amethibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kusema wanafunzi watatu walishikiliwa kwa muda na jeshi hilo na kuachiwa baada ya kuchukuliwa maelezo.

Alisema upelelezi unaendelea ili kubaini chanzo cha vurugu hizo na kuwataka wanafunzi hao kuwa watulivu wakati serikali inashughulikia malalamiko yao.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa