Sekta ya elimu imetakiwa kupanua na kuinua ubora wa elimu kwa kuajiri walimu wa
kutosha sanjari na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, mishahara
na upatikanaji wake kwa wakati na miundombinu kufikia maeneo ya shule.
Hayo yamesemwa na kaimu mkuu wa mkoa wa lindi alipokuwa akisoma hotuba kwa niaba ya waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi Shukuru Kawambwa katika wiki ya uhamasishaji wa elimu kwa wote duniani iliyofanyika kitaifa mkoani lindi ambapo kaulimbiu ya kampeni hiyo ni kila mwanafunzi anahitaji mwalimu.
Dkt. Nassoro Himidi amesema kwa kutambua umuhimu wa kila mwanafunzi kuwa mwalimu wa kila somo serikali itaendelea kutoa motisha mbalimbali kwenye mafunzo ya elimu ya ualimu ikiwa ni pamoja na kuendelea kuzifanya ada katika vyuo vya ualimu kuwa nafuu na kutoa mikopo kwa nafunzi wa elimu ya juu wanaosomea ualimu.
Amesema pamoja na kuwekwa kwa sera na sheria zinazowezesha wadau kuchangia kujenga mazingira bora ya kutolea elimu, jamii nayo ina umuhimu mkubwa katika kuhakikisha kuwa mwalimu anafanya kazi yake kwa amani na utulivu.
Naye mwenyekiti wa mtandao wa elimu Tanzania Mary Soko amesema kuwa lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha serikali inaliona tatizo la uhaba wa walimu kuwa ni kikwazo kikubwa katika kuwapatia wanafunzi elimu iliyo bora.
Amesema, mlundikano wa wanafunzi katika madarasa hautaifikisha serikali kwenye malengo ya elimu kwa wote ifikapo mwaka 2015 na hivyo kampeni zilenge kwenye kuondoa uhaba wa walimu mashuleni kwa kuboresha maslahi na mazingira ya kufundishia.
Jumla ya nchi 181 ziliunga mkono tamko la ELIMU KWA WOTE kwa kuridhia mkataba wa kimataifa na Tanzania ikiwa ni moja wapo ambapo kampeni hii kwa mwaka 2013 imezinduliwa aprili 21 na kuhitimishwa aprili 27 mkoani Lindi.
0 comments:
Post a Comment