Home » » Jiungeni na NHIF/CHF kulinda mitaji yenu-Mkurugenzi Halmashauri ya Kilwa

Jiungeni na NHIF/CHF kulinda mitaji yenu-Mkurugenzi Halmashauri ya KilwaMkurugenzi wa Halmashauri ya Kilwa, Adolph Mapunda akifungua mafunzo ya akina mama wajasiriamali wilayani Kilwa yaliyoandaliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Raphael Mwamoto akitoa maelezo ya utangulizi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu.
Mkurugenzi wa kitengo cha Uwezeshaji Wanawake katika Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Tabu Likoko akieleza jambo kwa washiriki wa mafunzo.
Meneja wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) Bw. Makalla akitoa mada ya umuhimu wa kujiunga na CHF.
Mmoja wa washiriki akiuliza swali
Washiriki wakiendelea kuuliza maswali ili kutaka ufafanuzi wa namna ya kujiunga.

WANAWAKE wilayani Kilwa hususan wajasiriamali, wametakiwa kuchangamkia fursa ya kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii ili kulinda mitaji yao wakati wanapougua.

Wametakiwa kufanya hivyo kutokana na ukweli kwamba, watanzania wengi hawana utamaduni wa kujiwekea akiba hasa ya matibabu hali inayolazimu kutumia fedha za biashara wakati wanapopatwa na matatizo ya ugonjwa.

Rai hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilwa, Adolph Mapunda wakati akifungua mafunzo ya akina mama wajasiriamali wilayani humo yaliyoandaliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya yanayowaelimisha umuhimu wa kuwa kwenye mfumo wa kupata huduma za matibabu kupitia bima za afya.

Mapunda alisema kuwa kwa sasa gharama za matibabu zimekuwa zikipanda kila kukicha hivyo njia pekee inayoweza kuwakomboa ni kuwa kwenye utaratibu wa NHIF au CHF utaratibu ambao ni wa kuchangia kabla ya kuugua.

Hata hivyo alisema kuwa uongozi wilayani humo utaendelea na jitihada za uelimishaji wananchi ili waweze kutumia fursa hii ambayo ni njia pekee ya kuwakomboa kwenye suala zima la afya.

“Kundi lenu ni muhimu sana siyo tu katika kuinua hali ya uchumi wa nchi hii, bali pia katika kuziwezesha familia zenu katika suala zima la afya, mkijiunga na huduma hizi mtakomboa familia zenu na mtaweza kupanga hata mipango ya familia huku mkiwa na uhakika wa matibabu pale ugonjwa unapotokea,” alisema Mapunda.

”Naamini kuwa wengi wenu hapa mumewahi kupatwa na shida ya kuugua au kuuguliwa wakati mkiwa hamna kitu mfukoni na hivyo kulazimika kuuza vitu vya ndani au kuua mtaji wa biashara ili kumuhudumia mgonjwa hivyo tumieni fursa hii,” alisema.

Kwa upande wa NHIF ambayo iliwakilishwa na Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti, Raphael Mwamoto, alisema kuwa mpango wa kutoa elimu kwa wananchi inayohusu umuhimu wa kuwa na bima za afya ni endelevu kwa nchi nzima ili kuwawezesha Watanzania wengi kuwa na bima ya afya.

Alisema kuwa kuwepo kwa changamoto za ukosefu wa dawa na zingine zisiwe kikwazo kwa wananchi kujiunga kwa kuwa Mfuko kwa kushirikiana na wadau mbalimbali unazidi kuja na mikakati ya kuondoa changamoto hizo.

“Kwa sasa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unasajili maduka muhimu ya dawa katika maeneo mbalimbali ili kukabiliana na tatizo la dawa, lakini pia inatoa mikopo nafuu ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo yote hii ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma nzuri na yenye heshima, hivyo wananchi msiwe na wasi wasi kuhusiana na huduma za NHIF,” alisema.

Kwa upande wa wanavikundi waliohudhuria mafunzo hayo, waliuhakikishia uongozi wa NHIF kuwa watajiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili waweze kunufaika na huduma zake.

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unaendesha mafunzo haya wilayani Kilwa na Lindi Vijijini kwa ushirikiano wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) hivyo zaidi ya wanawake 600 watapata mafunzo hayo.

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa