Home » » KAMPENI YA MAMA MISITU YATENGEWA MIL. 328/-

KAMPENI YA MAMA MISITU YATENGEWA MIL. 328/-



na Fatuma Mnyeto, Kilwa
OFISA Mradi wa Shirika lisilo la kiserikali la Mpingo Conservationa and Development Initiative, Andrew Mariki, amesema zaidi ya sh milioni 328.4 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza kampeni ya Mama Misitu inayolenga kuboresha utawala bora katika usimamizi wa misitu nchini.
Mariki alibainisha hayo mwishoni mwa wiki mjini hapa kwenye kikao maalumu kwa wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kilwa, alipokuwa akitoa maelezo ya mradi huo unaotekelezwa kwa miaka miwili.
Alisema mradi umeibuliwa kutokana na idadi ya watu, kuongezeka kwa kasi mahitaji ya mazao ya misitu, upungufu katika usimamizi wa misitu na matumizi endelevu ya mazao ya misitu.
Alieleza chimbuko la kampeni hiyo ambayo kwa kuanzia itatekelezwa katika vijiji vya Mavuji, Ngea, Mandawa, Mitole, Ruhatwe, Kiwawa, Hotelitatu, Mtandi na Mchakama ni kuielimisha jamiii juu ya haki ya umiliki wa misitu na ardhi na utekelezaji wa sera na sheria ya misitu na ardhi na usimamizi wa biashara ya mazao ya misitu kwa ujumla.
Alisema kampeni hiyo inatarajia kuona uwezo na uwajibikaji wa taasisi husika katika ngazi za wilaya na vijiji juu ya utunzaji, uhifadhi wa rasilimali za misitu na usimamizi na pia kuwa na uwazi juu ya matumizi na mapato ya mazao ya misitu na kuziwezesha taasisi na jamii kuelewa na kusimamia haki zao za usimamizi wa misitu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Abdallah Ulega, aliwataka wajumbe wa kamati hiyo kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo, ili iweze kufikia lengo lililokusudiwa la kutunza mazingira na kumfanya kila mwananchi kunufaika na rasilimali ya misitu.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa