Home » » BALOZI MCHUMO APETA CCM

BALOZI MCHUMO APETA CCM

Na Abdallah Mbonde
MWANASIASA wa siku nyingi nchini, Balozi Ali Mchumo, ameshinda katika uchaguzi wa kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Balozi Mchumo alishinda uchaguzi huo uliofanyika Jumamosi iliyopita, kupitia Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, baada ya kuwabwaga wapinzani wake, Said Mkunga na Njuma Ibrahim.

Akizungumzia ushindi huo, Balozi Mchumo alisema amefurahishwa na maamuzi sahihi na imani kubwa iliyoonyweshwa kwake na wanachama wenzake wilayani humo.

“Nawashukuru sana wanachama wenzangu kwa moyo wa upendo na imani mliyoonyesha kwangu, kwa kunichagua kuwa mjumbe wa NEC.

“Naahidi nitashirikiana nanyi katika kufikisha mawazo yenu na kukitetea na kukilinda chama chetu na wananchi kwa ujumla,” alisema Balozi Mchumo.

Aidha katika uchaguzi huo, viongozi wengine waliochaguliwa wilayani humo ni Yusufu Kopakopa, anayekuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya Kilwa, huku Mkuu wa wilaya hiyo, Abdallah Ulega, akichaguliwa kuwa mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama.

Wengine waliochaguliwa kuwa wajumbe wa mkutano mkuu wa taifa kupitia wilaya hiyo, ni Kinemene Mangosongo, Hasineni Dewji, Saidi Timami na Mohamedi Mtule.

Balozi Mchumo ambaye kitaaluma ni mwanasheria, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za kimataifa, ikiwamo ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Mazao Duniani, wenye makao makuu nchini Uholanzi.

Amewahi pia kuwa Naibu Katibu Mkuu, Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi wa Tanzania katika nchi za Uingereza, Japan, Umoja wa Mataifa na kwingineko duniani.

Hapa nchini kwa nyakati tofauti, Balozi Mchumo amewahi pia kuwa Waziri wa Biashara, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani na Mbunge wa Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa