na Happy Mollel, Ruangwa
UZALISHAJI duni
wa vyakula wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, unaoambatana na ukosefu wa utaalamu
wa kutumia vyakula vichache vilivyopo, umesababisha watoto wengi kukumbwa na
tatizo la utapiamlo na udumavu.
Changamoto hiyo
ilitolewa na Ofisa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto wa Wilaya, Suleman
Mohamed, na kuongeza kuwa Ruangwa ni moja kati ya wilaya zinazosumbuliwa na
tatizo la lishe.
“Bila kuficha
wilaya yetu bado ina changamoto kubwa ukilinganisha na wilaya nyingine…tatizo
la lishe ni kubwa na hii ni kutokana na familia nyingi za huku kukosa uhakika
wa kupata chakula kwa milo yote mitatu kama tulivyozoea,” alisema.
Alibainisha
kuwa sababu nyingine inayochangia kuwapo kwa utapiamlo ni kukosekana kwa elimu
sahihi ya namna ya kutumia vyakula vya asili vikiwemo vile vyenye virutubisho
vingi.
Akitoa
ufafanuzi juu ya tatizo la lishe wilayani hapa, Ofisa Lishe wa Wilaya, Vaileth
Richard, alisema mbali na kukosekana kwa utaalamu wa kuvitumia vyakula vichache
vilivyopo, ofisi yake tayari imeshajiwekea mikakati ya kuongeza maeneo ya
kilimo kwa mazao ya chakula, ili kukabiliana na ukosefu wa vyakula.
Chanzo: Tanania Daima
0 comments:
Post a Comment