Home » » MTANDA AAHIDI KULALA VIJIJINI

MTANDA AAHIDI KULALA VIJIJINI

na Mwandishi wetu, Lindi
MBUNGE wa Mchinga, Said Mtanda (CCM), ameahidi kulala vijijini, kama sehemu ya mkakati wa kushughulikia kero za wananchi wake.
Mtanda alitangaza uamuzi huo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mchinga Moja, Wilaya ya Lindi Vijijini.
Mkutano huo uliohudhuriwa na wageni mbalimbali ulikuwa na lengo la kumpongeza baada ya kuchaguliwa hivi karibuni kuwa Mbunge wa Afrika.
Akizungumza katika mkutano huo, Mtanda alisema hivi sasa atalazimika kupanga ratiba za kulala vijijini, baada ya kuombwa kufanya hivyo kwa muda mrefu.
Aidha, alikanusha shutuma zinazotolewa na wapinzani wake kisiasa, kwamba amekuwa haonekani jimboni humo.
“Hakuna kijiji ambacho sijafika, kama kuna mtu anasema sijafika vijijini aje hapa nitamuonesha kwenye kompyuta yangu siku na tarehe niliyofika katika hicho kijiji.
“Wengine wakasema mbunge halali vijijini. Jamani siku zote nimekuwa nikijiuliza, hivi kulala vijijini maana yake nini? Huo usiku unafanya shughuli gani vijijini?
“Halafu nikilala vijijini ndiyo kero za wananchi zitakwisha? Wakaniambia kuwa nikilala vijijini nitapata fursa ya kuzungumza na wazee na kupata mawazo mbadala.
“Sasa nitapanga ratiba ya kulala vijijini, utaratibu huu ni mzuri unasaidia kubaini na kuweka mipango ya maendeleo kwa karibu zaidi na wananchi,” alisema.
Katika ziara hiyo, Mtanda aliongozana na kada kutoka makao makuu ya CCM, ambaye pia ni Msadizi wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Hiza Tambwe.
Tambwe aliwataka wananchi wa jimbo hilo kutembea kifua mbele na kujifariji kutokana na mbunge wao kuchaguliwa kuwa mbunge wa Afrika.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa