Home » » MBUNGE CCM AWAFUNDA WAPIGA KURA

MBUNGE CCM AWAFUNDA WAPIGA KURA

Na Khamis Mkotya, Lindi
MBUNGE wa Mchinga (CCM), Said Mtanda, amewataka wananchi wa jimbo lake kuhakikisha suala la gesi linaingizwa katika Katiba mpya. Mtanda alitoa wito huo juzi katika mikutano mbalimbali aliyoifanya katika Vijiji vya Mnang’ole, Malo na Mvuleni vilivyopo Kata ya Kilolambwani.

Katika mikutano hiyo, alisema suala la gesi kuingizwa katika Katiba mpya, ni muhimu kuwafanya wananchi wa mikoa ya kusini kutokuwa watazamaji.

Alisema rasilimali ya gesi ndiyo rasilimali inayokuja kwa kasi na akataka Katiba itenge fungu maalumu la gesi kwa ajili ya manufaa ya watu wa Lindi na Mtwara.

“Ndugu zangu Tume ya Katiba mpya inakuja Mchinga Septemba 18, mwaka huu Kata ya Kitomanga, Septemba 22 Kilolambwani.

“Katika mikutano hiyo twendeni kwa wingi tukaseme mambo yetu. Katika mambo hayo suala la gesi ni muhimu tulizingatie tusipoteze hii nafasi.

“Tupendekeze gesi iingizwe katika Katiba mpya tumalize utata, Katiba itenge fungu maalumu kwa ajili ya maendeleo ya watu wa Lindi, tusiwe watazamaji.

“Kule Shinyanga madini yaligunduliwa siku nyingi lakini wananchi wa Shinyanga hawajanufaika na madini yao, hatutaki yaliyotokea Shinyanga yatukute na sisi.

“Hapa Lindi kuna gesi nyingi yenye ujazo wa cubic feet zaidi ya trilioni tatu. Hii ipo hapa Kilolambwani Lindi achilia mbali ya Mnazibay na kwingineko.

“Kwa kutambua uwapo wa rasilimali hii mkoani kwetu, hivi karibuni mimi na baadhi ya wabunge tunakwenda katika nchi za Trinidad na Tobako, kujifunza namna ya matumizi ya gesi ili tuje kutoa elimu,” alisema.

Alisema Serikali imeruhusu asilimia 0.5 ya mapato yote ya gesi kubaki katika wilaya zenye gesi kama mrabaha wa halmashauri husika.

Alisema fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kuboresha miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri kama vile barabara, maji afya na elimu.

Alisema yeye na wabunge wenzake wa mikoa ya kusini wanafanya jitihada kubwa za kuhakikisha rasilimali hiyo inawanufaisha kwanza wananchi wa mikoa hiyo.

Akiwa katika Kijiji cha Mnang’ole, alisikiliza kero mbalimbali za wananchi wa jimbo hilo ambazo ni barabara na ukosefu wa maji na zahanati.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa