na Salum Mkandemba
FAINALI ya michuano ya soka kwa vijana chini ya miaka 13 ya ‘Lindi Soccer Street’ ilifanyika juzi kwenye Uwanja wa Mtanda Jeshini Manispaa ya Lindi na kushuhudiwa Lindi Soccer Academy (LSA), wakiibuka mabingwa kwa kuwachapa FC Vito mabao 7-3.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa LSA, Hafidh Karongo, mabao saba ya kikosi chake yalifungwa na nyota wawili, Hamdani Saharani aliyepachika matano dakika za 13, 20, 27, 40 na 46, huku Rozitu Pasdu akitupia mawili dakika za 33 na 77.
Karongo aliongeza kuwa wafungaji wa Vito katika fainali hiyo ya michuano hiyo iliyoratibiwa na shirika la kuendeleza michezo la Sports Development Aid (SDA), walikuwa ni Midraji Haji dakika za 9 na 30 na Yunus Juma dakika ya 71.
Licha ya mabao yake matano katika mchezo huo, Saharan alishindwa kumng’oa katika kilele cha wapachika mabao wa michuano hiyo, yoso mwenzake wa LSA, Haji Saidi, ambaye licha ya juzi kutofunga, alitwaa tuzo ya Mfungaji Bora kwa mabao yake nane.
Mabingwa LSA, walitwaa kombe na mipira miwili, huku Vito ikijishindia kombe dogo na mpira mmoja, wakati mfungaji Haji alijipatia jezi, kipa bora Leonard Salvatory wa timu ya Brazil alizawadiwa glovu na tuzo ya mchezaji mdogo zaidi mashindanoni, ilitwaliwa na yoso aliyetajwa kwa jina moja la Karimu, aliyezawadiwa mpira.
Michuano hiyo ilishirikisha timu sita za vijana, ambazo zote zilipatiwa mpira mmoja mmoja, ingawa Shirikishi FC ilitolewa mashindanoni kwa kuchezesha ‘vijeba.’
Mkurugenzi wa SDA, walioandaa michuano hiyo, Mohammed Chigogola, alisema amefurahishwa na vipaji vilivyooneshwa na vijana, huku akiwataka wadau na klabu shiriki kutowatelekeza vijana hao baada ya michuano hiyo, badala yake iwaendeleze.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment