JIBU LA SWALI LA MBUNGE Liwale
na Mwandishi wetu, Dodoma
SERIKALI imekiri kuwepo na tatizo la uhaba wa magari ya kubebea wagonjwa (ambulance) katika Wilaya ya Liwale mkoani Lindi.
Kauli hiyo imetolewa jana bungeni na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Liwale, Faith Mitambo (CCM).
Mbunge huyo alitaka kujua kama serikali inaweza kutoa gari la kubebea wagonjwa kwa wananchi wa vijiji hivyo.
Pia, alihoji kama serikali haioni umuhimu wa kuiongezea Hospitali ya Wilaya ya Liwale gari la wagonjwa ili liweze kuhudumia vijiji vingine vilivyo mbali na hospitali hiyo.
Akijibu swali hilo, Mwanri alisema halmashauri hiyo ina magari mawili ya kubebea wagonjwa ambayo ni DFP 6393 na SM 4997.
Alisema magari hayo yapo katika hospitali ya wilaya yakihudumia tarafa mbili za Liwale na Makata.
“Hata hivyo, gari Na. 4997 halifanyi kazi kutokana na kuharibika,” alisema.
Aidha, alisema mwaka wa fedha wa 2011/12 Halmashauri ya Liwale ilipata mgawo wa pikipiki nne za miguu mitatu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment