Home » » TUNAWATAKIA IDD EL-FITRI NJEMA

TUNAWATAKIA IDD EL-FITRI NJEMAWAISLAMU nchini leo watasherehekea Sikuuu ya Idd el- Fitri ambayo husheherekewa mara baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Tunapenda kuchukua fursa hii kuwatakia sikukuu njema Waislamu wote nchini na kuwaomba washerehekee kwa amani na utulivu kama vile walivyokuwa kwenye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani ni miongoni mwa nguzo tano za Uislamu hivyo katika kipindi chote cha funga ya Ramadhani, mbali na kufunga mchana anatakiwa azidishe swala mbalimbali na kujiepusha kabisa na maovu.
Mwezi mtukufu wa Ramadhani una thamani na historia kubwa kwa Waislamu kwa sababu ndio mwezi kiliposhuka kitabu kitakatifu cha Kurani katika siku inayoitwa Lai latul Kadir usiku ambao ni bora kuliko miezi 1,000.
Si nia yetu kuanza kuzungumzia kwa undani faida za mwezi wa Ramadhani lakini katika kipindi chote cha mwezi huu tuliona idadi kubwa ya Waislamu wakivaa mavazi ya stara, kutenda matendo mema na kualikana kwenye futari.
Tusingependa Idd el- Fitri iwe mwanzo wa ajali, maasi, vifo na maovu mengi ambayo mara kwa mara tumekuwa tukiyashuhudia kwenye sikuu mbalimbali hapa nchini.
Kwa mujibu wa vitabu vya dini, Mwislamu yeyote akayetenda maovu siku ya leo ni sawa na kufanya dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu siku ya kiama.
Tunaamini mafunzo waliyoyapata waumini wa Kiislamu kwenye mwezi mtukufu wa Ramadhani utawasaidia kuishi kulingana na maagizo ya Mwenyezi Mungu na kujiepusha na dhambi mbalimbali.
Tunachukua fursa hii kuwaomba madereva wote wa vyombo vya moto kuchukua tahadhari pamoja na kutoendesha kwa kasi wanapovitumia ili kuepusha ajali zinazozidi kuongezeka kila kukicha.
Wazazi na walezi wasiwaruhusu watoto wao kwenda matembezini, fukwe za bahari na kumbi za disko bila ya uangalizi maalumu.
Tunasema hivyo kwakuwa kila mara tumekuwa tukisikia watoto wakipata madhara kwenye kumbi za disko, kupotea, kuzama baharini na mikasa mbalimbali ambayo chanzo chake ni uangalizi mdogo wa wazazi au walezi.
Kwa wale wanaokwenda matembezini ni vema wakahakikisha majumbani mwao kunakuwa salama kwa kumuacha mtu atakayelinda au kuzifunga vizuri kwa lengo la kuzuia wezi.
Tunaamini kuwa Jeshi la Polisi litazidisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ili kuwadhibiti wale wote waliolenga kufanya uhalifu kwenye sherehe za Idd el- Fitri.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Lindi Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa